Feb 01, 2025 02:32 UTC
  • Jumamosi, Mosi Februari, 2025

Leo ni Jumamosi Pili Shaaban 1446 Hijria mwafaka na Mosi Februari 2025 Miladia.

Katika siku kama ya leo miaka 211 iliyopita, kulitokea vita vikali na vya umwagaji damu mkubwa maarufu kwa jina la Routier katika eneo lenye jina kama hilo karibu na Mto Ob kati ya jeshi lililokuwa na askari laki moja na 60 elfu la vikosi vya waitifaki wa nchi za Prussia, Austria na Sweden na jeshi lililokuwa na askari elfu 42 la Ufaransa chini ya uongozi wa Napoleon. Katika vita hivyo jeshi la Ufaransa lilishindwa vibaya na waitifaki kutokana na kutokuwa na moyo wa kupigana na uchache wa wapiganaji wake.  

 

Siku kama ya leo miaka 105 iliyopita alizaliwa Ayatullah Murtadha Mutahhari, msomi na mwanafikra mkubwa wa Kiislamu wa zama hizi. Alizaliwa katika eneo la Fariman tarehe 13 Bahman, 1298 Hijiria Shamsia, na baada ya kupata elimu ya msingi alijiunga na chuo kikuu cha kidini cha Qum nchini Iran na kuhudhuria darsa za wasomi wakubwa kama Ayatullahil Udhma Boroujerdi, Allameh Tabatabai na Imam Ruhullah Khomeini. Katika kipindi cha kutafuta elimu ya juu, Shahidi Murtadhaa Mutahhari alifanya jitihada kubwa za kutakasa nafsi na kuruzukiwa kipaji cha aina yake katika masuala ya elimu.  Mwanzoni mwa harakati ya Kiislamu ya Iran mnamo 1341 na  1342 Hijria Shamsia, Shahidi Mutahhari alijiunga na safu ya harakati hiyo na kilele cha harakati zake kilikuwa tarehe 5 Juni 1963, wakati alipokamatwa na kufungwa na shirika la ujasusi la Shah, SAVAK. Baada ya kuachiwa huru aliendeleza mapambano kwa kuunda makundi ya wanaharakati na kulinda harakati hiyo ya mapinduzi ya kiislamu. Aliendeleza harakati zake kupitia njia ya kuwazindua vijana na matabaka mengine ya jamii kupitia kumbi na majukwaa mbalimbali hususan misikiti na vituo vya kidini. Alikamatwa tena na kufungwa na utawala wa Shah na kupigwa marufuku kuhutubia umma. Wakati wa kukaribia ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Shahidi Mutahhari alikuwa mmoja kati ya shakhsia muhimu wa kidini, kielimu na kisiasa katika harakati ya Kiislamu. Imam Khomeini, mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alimteua Shahid Mutahhari kuwa mwanachama na mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ya Kiislamu. Ayatullah Murtadha Mutahhari ameandika karibu vitabu 80 katika nyanja mbalimbali. 

Ayatullah Murtadha Mutahhari

 

Tarehe Mosi Februari miaka 67 iliyopita iliundwa Jamhuri ya Muungano wa Kiarabu ya Syria na Misri. Baada ya kumalizika vita vya Suez na kurudi nyuma askari wa Uingereza, Ufaransa na utawala ghasibu wa Israel kutoka katika ardhi ya Misri, Gamal Abdul Nasser alitambuliwa kuwa kiongozi dhidi ya ukoloni wa Magharibi na dhidi ya Uzayuni katika ulimwengu wa Kiarabu na kupata umashuhuri mkubwa. Hatua ya kwanza ya kuanzisha muungano wa nchi za Kiarabu dhidi ya utawala haramu wa Israel na waungaji mkono wake wa Magharibi ilichukuliwa tarehe Mosi Februari 1958 baada ya Syria kutia saini makubaliano ya kuungana na Misri na muungano huo ulianza rasmi baada ya kura ya maamuzi ya tarehe 22 Februari 1958 katika nchi hizo mbili.

 

Siku kama ya leo miaka 46 iliyopita, Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, ambayo ilikuwa muungaji mkono mkubwa wa utawala wa kidhalimu wa Shah nchini Iran, iliitambua hotuba ya hamasa iliyotolewa na hayati Imam Khomeini MA mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu katika makaburi ya Beheshti Zahra mnamo tarehe 12 Bahman, baada ya kurejea kwake nchini kuwa, ilikuwa dhidi ya Marekani. Katika hotuba hiyo Imam Khomeini alibainisha misimamo yake mkabala wa siasa za kibeberu na uingiliaji wa Marekani katika masuala ya Iran. Kwa upande wake utawala wa Kizayuni wa Israel ulielezea wasiwasi wake kuhusu kurejea Imam Khomeini nchini Iran kwa sababu ulitambua kwamba, Imam na wananchi Waislamu wa Iran ni wapinzani wakubwa wa utawala huo ghasibu na vamizi. Aidha shirika la habari la Russia, Itar-Tass liliripoti kuwa kurejea Ayatullah Ruhullah Khomeini nchini Iran, kumeyafanya mapambano ya wananchi wa nchi hiyo kuingia katika hatua yenye kuainisha mustakabali.