Jumapili, 09 Februari, 2025
Leo ni Jumapili tarehe 10 Shaaban 1446 Hijria mwafaka na 9 Februari 2025
Siku kama ya leo miaka 1024 iliyopita, alifariki dunia mjini Baghdad, Iraq Abu Abdillah Abdul-Baqi, mmoja wa malenga mashuhuri wa karne ya tano Hijiria. Mbali na kusoma kwa maulama wakubwa wa fasihi, pia alipata fursa ya kushiriki masomo ya kidini kwa maulama wakubwa wa mji huo na kuweza kustafidi na elimu tofauti, hususan elimu ya hadithi na kadhalika. Mashairi ya Abu Abdillah Abdul-Baqi yalikuwa ya kipekee kiusomaji mashairi na ameacha athari nyingi katika uwanja huo.
Siku kama ya leo miaka 692 iliyopita, alifariki dunia Majdud-Din Abul-Fawaaris, mmoja wa maulama wakubwa wa Kiislamu. Alizaliwa nchini Iraq na baada ya kuhitimu elimu ya msingi, alianza kusoma kwa maulama wakubwa na kufanikiwa kufikia daraja ya juu kielimu na kutokea kuwa mwalimu. Majdud-Din Abul-Fawaaris, alitabahari sana katika elimu za fiqhi, usulu fiqhi, hadithi, theolojia, tafsiri ya Qur'ani na fasihi ya lugha ya Kiarabu. Kuna athari nyingi kutoka kwa msomi huyo mkubwa wa Kiislamu na mojawapo ni kitabu kinachoitwa 'Kanzul-Fawaaidi.'
Siku kama ya leo miaka 46 iliyopita majenerali wa utawala wa Shah waliongeza muda wa serikali ya kijeshi katika mji wa Tehran. Majenerali hao walichukua hatua hiyo ili kuwazuia wananchi kuwaunga mkono na kuwasadia wanajeshi wa kikosi cha anga ambao walikuwa wakishambuliwa na kikosi cha gadi ya Shah, na kwa njia hiyo waweze kumtia mbaroni Imam Khomeini Mwenyezi Mungu amrehemu pamoja na shakhsiya wengine muhimu waliokuwa katika harakati za Mapinduzi au kuwauwa. Hata hivyo Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa kuona mbali na kusoma vyema alama za nyakati, aliwatolea mwito wananchi kupuuza kizuizi hicho kilichowekwa na majenerali wa Shah cha kuongeza muda wa serikali ya kijeshi au sheria za kutotoka nje. Wananchi wanamapinduzi wa Iran pia waliitikia agizo hilo la Imam Khomeini Mwenyezi Mungu amrehemu na kumininika katika mitaa mbalimbali na kueneza mapambano yao katika vituo vingine vya kijeshi vya utawala wa kidikteta wa Shah katika mji wa Tehran na miji mingineo. ***
Katika siku kama ya leo miaka 41 iliyopita sawa na tarehe 9 Februari 1984, alifariki dunia Yuri Andropov, mmoja wa viongozi wa Urusi ya zamani. Andropov ambaye alikuwa mwanasiasa mkubwa wa Urusi ya zamani alizaliwa tarehe 15 Juni 1914 ambapo akiwa kijana alijiunga na harakati za kisiasa na Chama cha Kikomonisti. Mwaka 1953 Yuri Andropov aliteuliwa kuwa balozi wa Urusi ya zamani nchini Hungary ambapo wakati nchi yake ilipoivamia Hungary mwaka 1956, alitwaa uongozi wa operesheni hiyo ya kijeshi dhidi ya nchi hiyo na kutekeleza ukandamizaji na umwagaji damu dhidi ya wapigania uhuru wa Hungary. Mwaka 1967 Yuri Andropov aliteuliwa kuwa mkuu wa shirika la ujasusi la Urusi ya zamani KGB ambapo aliendelea kuliongoza shirika hilo kwa kipindi cha miaka 15 yaani hadi alipofariki dunia Leonid Brezhnev, Kiongozi wa wakati huo wa Urusi ya zamani hapo mwaka 1982. Miezi saba tangu kiongozi huyo afariki dunia, Andropov aliteuliwa kuwa katibu mkuu wa Chama cha Kikomonisti cha Urusi ya zamani, ambacho ni cheo cha juu kabisa nchini humo. Aliendelea kusimamia uongozi wa chama hicho kwa kipindi cha miaka 15, hadi alipofariki dunia. Katika kipindi chake kuliongezeka mashindano ya uundaji wa silaha za nyuklia.
Siku kama ya leo miaka 33 iliyopita, baada ya Chama cha Wokovu wa Kiislamu cha Algeria (FIS) kupata ushindi mkubwa katika uchaguzi wa Bunge, wanajeshi waliokuwa wakitawala nchini humo, walibatilisha matokeo ya uchaguzi huo na kukipiga marufuku chama hicho, hali iliyopelekea kuzuka machafuko makubwa. Machafuko hayo yalipelekea kuuawa watu wengi nchini Algeria.
