Jumanne, tarehe 11 Februari, 2025
Leo ni Jumanne tarehe 12 Shaaban 1446 Hijria sawa na Februari 11 mwaka 2025.
Siku kama ya leo miaka 948 iliyopita aliaga dunia Hassan bin Hafiz Andalusi, mpokezi wa Hadithi na tabibu mashuhuri wa Andalusia, sehemu ya Uhispania ya leo.
Hassan bin Hafiz Andalusi aliyejuliikana kwa jina la Ghassani, alikuwa mwanafasihi mahiri na tabibu mweledi. Alikuwa na hati za kuvutia sana na kipaji kikubwa cha kutunga mashairi.
Kitabu cha 'Tamjiidul-Muhmal' ni miongoni mwa kazi za thamani za Hassan bin Hafiz al Andalusi na kinazungumzia na kufafanua maisha ya wapokezi wa Hadithi za Mtume (saw).

Siku kama ya leo miaka 375 iliyopita alifariki dunia René Descartes, mwanafalsafa na mtaalamu wa hisabati wa nchini Ufaransa.
Alizaliwa tarehe 31 Machi 1596 Miladia na baada ya masomo yake ya msingi alianza kusomea hisabati na tiba. Baadaye Descartes alibobea katika taaluma za hisabati na uhandisi na baadaye akianzisha utafiti katika uga wa falsafa.
Msomi huyo wa Kifaransa alifanya safari kwa kipindi fulani katika nchi mbalimbali na baadaye aliishi Uholanzi na kuanza kufanya utafiti. Rene Descartes aliitambua hisabati kuwa elimu kamili miongoni mwa elimu nyinginezo.
Miongoni mwa vitabu vya mwanafalsafa huyo ni Principles Of Philosophy, The Passions of the Soul na Discourse on the Method. *

Siku kama ya leo miaka 46 iliyopita serikali ya mpito ya Mapinduzi ya Kiislamu ilianza rasmi kazi zake katika siku za mwanzo kabisa za umri wa Mapinduzi ya Kiislamu hapa nchini.
Wakati huo huo wananchi waliendeleza mapambano ya kuangamiza kikamilifu mabaki ya utawala wa Shah. Baadhi ya makundi ya wananchi yalichukua jukumu la kulinda taasisi muhimu za serikali katika miji mbalimbali. Wakati huo ulidhihiri udharura wa kuwepo chombo cha kushughulikia kadhia hiyo na kukabiliana na vibaraka na mabaki ya utawala wa Shah.
Kwa msingi huo Mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu hayati Imam Khomeini alitoa amri ya kuundwa Kamati ya Mapinduzi ya Kiislamu.

Siku kama ya leo miaka 35 iliyopita sawa na tarehe 11 Februari 1990, Mzee Nelson Mandela kiongozi wa harakati ya kupambana na ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini aliachiwa huru baada ya kufungwa jela kwa miaka 27.
Mandela alikamatwa na kuhukumiwa kifungo cha maisha jela mwaka 1963 kwa sababu ya mapambano yake dhidi ya utawala wa kibaguzi wa Afrika Kusini.
Baada ya miaka kadhaa aliachiliwa huru kutokana na msimamo wake thabiti akiwa jela, mapambano ya wananchi wa nchi hiyo pamoja na mashinikizo yaliyotokana na fikra za waliowengi ulimwenguni.
