Alkhamisi, 13 Februari, 2025
Leo ni Akhamisi 14 Sha'ban 1446 Hijria sawa na 13 Februari 2025 Milaadia.
Miaka 807 iliyopita katika siku kama ya leo, inayosadifiana na tarehe 14 Shaaban mwaka 639 Hijria, alifariki dunia Ibn Yunus, faqihi, tabibu na mwanahesabati mashuhuri wa Kiislamu.
Msomi huyo wa Kiislamu alitumia sehemu kubwa ya umri wake kujifunza elimu kutoka kwa baba yake na wanazuoni wengine wa zama hizo. Baada ya kustafidi na elimu katika zama ambazo wasomi wa Kiislamu walitia fora katika elimu ya sayansi na sanaa, Ibn Yunus alianza kufunza katika vyuo mbali mbali mjini Cairo nchini Misri.
Mbali na kutabahari katika nyuga za fiqhi, sayansi na utabibu, msomi huyo wa Kiislamu alikuwa mtaalamu wa muziki. Miongoni mwa athari muhimu za mwanazuoni huyo wa Kiislamu, ni kitabu alichokipa jina la "Al-Asraaru Sultaniya" kinachozungumzia masuala ya unajimu.
Katika siku kama ya leo miaka 336 iliyopita tangazo lililojulikana kama Tangazo la Sheria lilisomwa katika sherehe za kumvika taji Mfalme William wa Tatu na Malkia Marry wa Pili wa Uingereza na kuanzia hapo mfumo wa utawala wa nchi hiyo ukabadilika na kuwa utawala wa kifalme wa kikatiba.
Kwa mujibu wa tangazo hilo, madaraka ya Mfalme wa Uingereza yalipunguzwa na kukabidhiwa bunge la nchi hiyo. ***
Siku kama ya leo mwaka 1946 wakati wa Vita vya Pili vya Dunia, ndege za kivita za Uingereza na Marekani zilianza kudondosha zaidi ya tani 3900 za mabomu katika mji wa Dresden nchini Ujerumani.
Mashambulizi hayo yaliua zaidi ya watu 25,000 na kusababisha majonzi na vilio kote duniani. ****
Siku kama ya leo miaka 36 iliyopita, mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Imam Ruhullah Khomeini alitoa fatuwa iliyomtambua Salman Rushdie mwandishi wa kitabu cha "Aya za Shetani" Satanic Verses kuwa ameritadi au kuondoka katika dini ya Kiislamu.
Katika kitabu hicho Rushdie alimvunjia heshima na kudhalilisha Mtume Muhammad (saw), kitabu kitukufu cha Qur'ani na matukufu mengine ya Kiislamu. Uandishi na uchapishaji wa kitabu hicho ulifanyika kwa njama na msaada wa nchi za Magharibi.
Hata hivyo fatuwa ya Imam Khomeini dhidi ya murtadi Salman Rushdie, iliwaamsha Waislamu na kuwatahadharisha kuhusu njama hiyo. Fatuwa hiyo ya Imam iliungwa mkono na waandishi wengi huru duniani, maulamaa wa Kiislamu na Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC).