Feb 22, 2025 02:29 UTC
  • Jumamosi, 22 Februari, 2025

Leo ni Jumamosi 23 Shaaban 1446 Hijria mwafaka na 22 Februari 2025

Siku kama ya leo miaka 1142 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria, alifariki dunia Abu Muhammad Hassan Ibn Ali Atroosh, maarufu kwa lakabu ya Nasser Kabir, alimu na mwanamapambano mkubwa miongoni mwa wajukuu wa Mtume Muhammad (saw). lizaliwa mwaka 230 Hijiria mjini Madina, na baada ya watawala wa Bani Abbas kuwaua na kuwabaidisha watu wa familia ya Mtume SAW akiwemo Imamu Hassan Askari (as), Ali Atroosh alipelekwa mjini Samarra, kaskazini mwa mji wa Baghdad, Iraq kwa amri ya watawala hao ikiwa ni baada ya baba yake kubaidishwa mjini hapo. Abu Muhammad Hassan Ibn Ali Atroosh alijifunza elimu ya dini mjini Baghdad na Kufa na kutokea kuwa msomi mkubwa huku akitabahari pia katika uwanja wa mashairi. Mbali na hayo alijihusisha na harakati za kisiasa ambapo katika kipindi cha mwamko wa Maalawi mjini Tabarestan, kaskazini mwa Iran, Atroosh alikimbilia katika eneo hilo. Baada ya kuanguka utawala huo, aliufufua huku akitawala sehemu kubwa ya maeneo ya kaskazini mwa Iran kwa uadilifu na usawa, sambamba na kueneza mafundisho ya dini ya Mtume Muhammad (saw). Katika harakati zake alifanikiwa kuwaingiza maelfu ya watu katika dini ya Uislamu. 'Al-Bisat' 'Tafsir al-Atroosh' na 'Imamatul-Kabir' ni miongoni mwa makumi ya vitabu vilivyoandikwa na msomi huyo. 

Mali alipozikwa Abu Muhammad Hassan Ibn Ali Atroosh

 

Miaka 713 iliyopita na katika siku kama ya leo kulingana na kalenda ya Hijria Hussein bin Abdullah Tayyebi aliyekuwa na lakabu ya Sharafuddin aliaga dunia. Alikuwa mpokezi wa hadithi na na mwanafasihi mkubwa. Abdullah Tayyebi alibobea katika elimu za fasihi ya lugha ya Kiarabu na alihesabiwa kuwa miongoni mwa wasomi wakubwa wa Kiislamu katika zama zake. Mwanazuoni huyo alikuwa akitilia mkazo suala la kufundisha tafsiri ya Qur'ani pamoja na Hadithi. Miongoni mwa vitabu vya msomi huyo ni 'Tafsirul-Qur'an' na 'Sherh al Meshkat'. 

 

Miaka 629 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Hijria, alizaliwa Nuruddin Abdul-Rahman Jami, mshairi na mwanafasihi mkubwa wa Kiirani wa karne ya 9 Hijria. Alizaliwa katika mji wa Jam ulioko katika mkoa wa Khorasan kaskazini mashariki mwa Iran. Alianza kujifunza elimu mbalimbali akiwa katika rika la ujana. Alikuwa na mapenzi na itikadi thabiti na watu wa Nyumba ya Bwana Mtume SAW na katu hakuwahi kuwasifu wafalme na watawala. Silsilat al-Dhahab na Baharestan ni baadhi ya athari za Nuruddin Abdul Rahaman Jami.

Mali alipozikwa Nuruddin Abdul-Rahman Jami

 

Siku kama ya leo miaka 80 iliyopita sawa na tarehe 4 Esfand 1323 Hijiria Shamsia, alifariki dunia Ayatullah Sayyid Muhammad Mahdi Dorchei, faqihi na alimu mkubwa. Alizaliwa yapata mwaka 1240 Hijiria Shamsia katika kijiji cha Dorchei karibu na mkoa wa Isfahan ndani ya familia ya kisomi na uchaji-Mungu. Ayatullah Sayyid Muhammad Mahdi alijifunza kwa baba yake elimu mbalimbali hadi mzazi wake huyo alipofariki dunia, na baada ya hapo akiwa na kaka yake, alifunga safari hadi mjini Isfahan kwa ajili ya kujifunza masomo ya kidini. Licha ya kukabiliwa na hali ngumu ya kimaisha Ayatullah Dorchei alifanya juhudi kubwa katika kusomea elimu za fiqhi na usulu fiqhi ambapo mwaka 1271 Hijiria Shamsia alielekea mjini Najaf, Iraq kwa ajili ya kukamilisha masomo yake ya ngazi ya juu. Aliishi mjini Najaf kwa kipindi cha miaka saba akisoma kwa maulama wakubwa kisha akarejea mjini Isfahan na kujishughulisha na ufundishaji wa elimu za Kiislamu ambapo alikuwa na makumi ya wanafunzi mashuhuri. Ayatullah Sayyid Muhammad Mahdi Dorchei ameacha turathi kama vile kitabu cha 'Kitabut-Twaharah' 'Kitabus-Swalat' na 'Usulul Fiqh.' 

 

Siku kama hii ya leo miaka 67 iliyopita aliaga dunia Abul Kalaam Ahmad Azad, aalim, khatibu hodari na mwanasiasa wa India akiwa na umri wa miaka 70. Abul Kalaam Azad alianzisha harakati za kisiasa dhidi ya ukoloni wa Uingereza na kwa lengo la kuwaamsha Waislamu wa India akiwa na umri wa miaka 17. Mwanasiasa huyo aliwekwa gerezani mara kadhaa kutokana na kuchapisha makala na kutoa hotuba zenye kufichua njama za wakoloni wa Kiingereza.

 

Katika siku kama ya leo miaka 45 iliyopita, yaani tarehe 4 Esfand 1358 Hijiria Shamsia, Ayatullah Dakta Muhammad Husseini Beheshti aliteuliwa kuwa mkuu wa kwanza wa Mahakama Kuu ya Iran baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu. Hatua hiyo ilichukuliwa na Imam Ruhullah Khomeini MA baada ya kupasishwa Katiba ya Jamhuri ya Kiislamu na kuundwa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu yaani Bunge. Dakta Beheshti alikuwa miongoni mwa wanafikra wakubwa na shakhsia mashuhuri wa Mapinduzi ya Kiislamu. Msomi huyo aliuawa kigaidi katika shambulizi la bomu lililotekelezwa na kundi la kigaidi la MKO mwaka 1360 Hijria Shamsia.   

 

Siku kama ya leo miaka 19 iliyopita miripuko mikubwa ya mabomu ilitokea katika haram mbili tukufu za Maimamu Hadi na Hassan al Askari (as) huko katika mji wa Samarra, kaskazini mwa Baghdad mji mkuu wa Iraq na kusababisha hasara kubwa katika eneo hilo tukufu la Waislamu. Uharibifu mkubwa uliosababishwa na miripuko hiyo katika haram hizo tukufu uliwakasirisha Waislamu duniani na hasa wa wafuasi wa madhehebu ya Shia. Maimamu hao wawili ni miongoni mwa wajukuu wa Mtume wa Mwenyezi Mungu Muhammad (saw). 

 

Siku kama ya leo miaka 15 iliyopita, Abdul-Malik Rigi kiongozi wa kundi la kigaidi la Jundullah lenye makao yake huko Pakistan, alitiwa mbaroni katika oparesheni ya kipekee na ngumu ya kiintelijinsia iliyofanywa na maafisa wa Wizara ya Usalama wa Ndani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Baada ya kufanya mashambulizi mengi ya kigaidi, gaidi huyo katili alikuwa safarini kuelekea nchini Kyrgyzstan akitokea Dubai, Imarati, kwenda kukutana na kufanya mazungumzo na kiongozi mmoja wa ngazi ya juu wa Marekani. Hata hivyo maafisa usalama wa Iran waliokuwa wakifuatilia kwa karibu nyendo zake waliweza kuitambua ndege iliyokuwa imembeba gaidi huyo na kuisubiri iingie katika anga ya Iran na hivyo kuilazimisha kutua katika uwanja wa ndege wa Bandar Abbas, kusini mwa Iran na baadaye wakamtia mbaroni kiongozi huyo wa kundi la kigaidi la Jundullah. Rubani wa ndege hiyo alifanya jitihada kubwa za kutoroka na kutoka nje ya anga ya Iran, lakini alizidiwa nguvu na maafisa usalama wa Iran, na kulazimishwa kuiteremsha. Abdulmalik Rigi alifanya jinai nyingi ikiwa ni pamoja na kutega na kuripua mabomu katika maeneo ya umma nchini Iran, kuwauwa kwa umati raia pamoja na kuwateka nyara. Rigi hakuwa na huruma hata kwa watu wake wa karibu. Alikiri kwamba alikuwa anapata misaada ya kila namna ikiwemo ya kifedha na kisilaha kutoka kwa Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel kama njia ya kuliwezesha kundi lake kufanye mauaji ya watu ndani ya Iran hususan katika maeneo ya kusini mashariki mwa Iran na kusababisha mizozo ya kimadhehebu katika maeneo hayo. Gaidi huyo alinyongwa tarehe 30 Khordad mwaka 1389 Hijria Shamsia sawa na tarehe 20 Juni, 2010 yaani miezi minne baada ya kutiwa mbaroni. Kukiri huko kwa Rigi kunaonyesha wazi madai ya uwongo ya serikali ya Marekani ya eti kupambana na ugaidi duniani.