Feb 24, 2025 03:07 UTC
  • Jumatatu, 24 Februari, 2025

Leo ni Jumatatu 25 Shaaban 1446 Hijria ambayo inasadifiana na 24 Februari 2025.

Siku kama ya leo miaka 1309 iliyopita, aliuawa kamanda wa Kiiran, Abu Muslim Khorasani, kwa amri ya Mansur, aliyekuwa mtawala wa wakati huo wa Bani Abbasi.

Abu Muslim Khorasani alikuwa kiongozi wa harakati liyopewa jina la 'Siah Jamegan' huko Khorasan ambayo ilianzisha uasi dhidi ya mtawala dhalimu wa Bani Umayyah. Katika kipindi kifupi watu wengi wa vijiji na miji mingi ya Khorasan walijiunga na kundi hilo.

Baada ya vita vingi Abu Muslim na wafuasi wake walifanikiwa kuwashinda watawala hao wa Bani Umayyah. Kwa utaratibu huo kuliandaliwa uwanja wa kuhitimisha kabisa utawala wa Bani Umayyah na kuingia madarakani watawala wa Bani Abbas.

Katika kipindi hicho Abu Muslim Khorasani alikuwa na nafasi kubwa kiasi cha kumfanya Mansur, mtawala wa ukoo wa Bani Abbas kujawa na hofu kubwa. Kwa sababu hiyo alipanga njama ya kumuua.

Baada ya mauaji hayo wafuasi wa Abu Muslim Khurasani walianzisha mapambano na kulipiza kisasi cha damu yake na mapimbano hayo yaliendelea kwa muda mrefu.

Miaka 491 iliyopita katika siku kama hii ya leo alizaliwa Luis Vaz de Camoens, malenga mkubwa wa Kireno na mmoja wa wanafasihi wakubwa wa Ulaya huko Lisbon mji mkuu wa Ureno.

Mbali na kuwa mshairi, De Camoens alikuwa mpiganaji jasiri. Moja ya kazi muhimu za utunzi za Luis Vaz de Camoens ni ile aliyoipa jina la" The Lusiads." 

Miaka 177 iliyopita katika siku kama ya leo utawala wa muda au duru ya pili ya mfumo wa jamhuri ulianza huko Ufaransa baada ya wananchi kufanya mapambano ya ukombozi na kumuondoa madarakani Luis Phillipe Mfalme mbeberu wa nchi hiyo.

Utawala wa aina hiyo unajulikana pia katika historia ya Ufaransa kwa jina la "Utawala wa Waandishi wa Habari". Hii ni kwa sababu waandishi habari 11 waliokuwa wakipigania mfumo wa jamhuri chini ya uongozi wa Alphonse de Lamartine malenga na mwandishi wa Kifaransa, ndio waliokuwa wakisimamia utawala huo. 

Siku kama ya leo miaka 76 iliyopita sawa na tarehe 24 Februari 1949 wawakilishi wa Misri na utawala wa Kizayuni wa Israel walisaini mkataba wa kusitisha mapigano kati ya pande mbili hizo huko katika kisiwa cha Rhodes kilichoko katika bahari ya Aegean.

Ni vyema kutaja hapa kuwa baada ya kuundwa serikali ya Kizayuni mwaka 1948 huko katika Palestina inayokaliwa kwa mabavu, Misri ilishirikiana bega kwa bega na baadhi ya nchi za Kiarabu katika kupigana vita dhidi ya utawala wa Kizayuni.

Hata hivyo wanajeshi wa utawala huo walifanikiwa kuingia katika ardhi ya Misri na Lebanon baada ya kuishambulia safu ya vikosi vya mapambano vya Waarabu ambavyo vilikuwa na zana chache za kisasa za kivita na hivyo kutoa pigo kwa vikosi vya nchi za Kiarabu.

Katika siku kama hii ya leo miaka 41 iliyopita ndege za kivita za utawala wa dikteta wa zamani wa Iraq, Saddam Hussein zilishambulia miji ya Saqz, Pol-e Dokhtar na Mahabad.

Utawala wa Saddam Hussein uliamua kushambulia makazi ya raia katika miji mbalimbali ya Iran sambamba na ushindi mkubwa wa wapiganaji wa Kiislamu hususan katika operesheni ya jeshi la Iran iliyopewa jina la Khaibar na kipigo cha jeshi la Iraq katika visiwa vya Majnun. Makumi ya raia waliuawa na wengine wengi kujeruhiwa katika mashambulizi hayo.