Jumanne, 25 Februari, 2025
Leo ni Jumanne 26 Shaaban 1446 Hijria sawa na 25 Februari 2025.
Siku kama ya leo miaka 1341 iliyopita, alifariki dunia, Yazid bin Abdul-Malik bin Marwan, khalifa dhalimu wa wakati huo.
Yazid bin Abdul-Malik aliingia madarakani baada ya kufariki dunia Omar bin Abdul-Aziz hapo mwaka 101 Hijiria.
Kiongozi huyo mbali na kufanya dhulma na ukandamizaji, hakuzingatia pia masuala ya Waislamu. Kwa kuzingatia kuwa alikuwa ni mtu wa karibu na ukoo wa Hajjaj Thaqafi, hivyo aliwapa umuhimu mkubwa watu wa ukoo huo.

Katika siku kama ya leo miaka 691 iliyopita, alifariki dunia Ibn Fasih, aliyekuwa faqihi, malenga na mtaalamu mashuhuri wa lugha ya Kiarabu, huko mjini Damascus, Syria.
Baada ya kusoma elimu ya sheria za Kiislamu na lugha ya Kiarabu, alianza kujifunza elimu ya Hadithi na kuwa gwiji katika uwanja huo. Msomi huyo wa Kiislamu alikuwa na kiwapa kikubwa cha kutunga mashairi. Ameandika vitabu mbalimbali kuhusu maudhui tofauti.

Miaka 69 iliyopita siku kama ya leo mwaka 1334 Hijiria Shamsia, alifariki dunia mtaalamu wa fasihi na malenga mkubwa wa Iran, Allamah Ali-Akbar Dehkhoda.
Alizaliwa mjini Tehran mwaka 1258 Hijiria Shamsia na akawa miongoni mwa wanafunzi wa awali wa chuo cha zamani cha siasa mjini Tehran. Baada ya kukamilisha masomo yake ya awali Dehkhoda alikwenda Ulaya na kufanya utafiti kwa miaka 5.
Alirudi Iran katika kipindi cha kuchipua fikra za kupigania uhuru, kipindi ambacho alikitumia kufanya kazi za kishairi dhidi ya utawala wa wakati huo. Kazi kubwa zaidi ya msomi huyo ni kamusi maarufu ya Dehkhoda.

Tarehe 25 Februari miaka 39 iliyopita dikteta wa zamani wa Ufilipino aliyekuwa amejitangaza rais wa maisha, Ferdinand Marcos, alikimbia nchi hiyo akiwa pamoja na familia yake.
Marcos alichukua hatamu za uongozi mwaka 1965. Alidumisha utawala wake wa kidikteta na ukandamizaji nchini Ufilipino kwa himaya na uungaji mkono wa nchi za Magharibi hususan Marekani. Mwaka 1973 Ferdinand Marcos alijitangaza kuwa rais wa maisha wa Ufilipino. Wakati huo wananchi katika maeneo mbalimbali walikuwa tayari wameanzisha harakati za mapambano ya kisiasa na kijeshi dhidi ya dikteta huyo.
Mapambano hayo yalishika kasi zaidi katikati ya mwongo wa 1980, na Februari 25 1986 Marcos alilazimika kukimbia Ufilipino.

Siku kama ya leo miaka 31 iliyopita Mzayuni aliyekuwa na misimamo ya kufurutu ada kwa jina la Baruch Goldstein aliwashambulia na kuwamiminia risasi Waislamu waliokuwa wakitekeleza ibada ya Swala katika Msikiti wa Haram ya Nabii Ibrahim mjini al Khalil, Palestina inayokaliwa kwa mabavu na kuua shahidi 29 miongoni mwao.
Mauaji hayo yalitokea wakati Waislamu hao walipokuwa katika ibada ya funga ya mwezi mtukufu wa Ramadhani. Waislamu wengine wengi walijeruhiwa katika shambulizi hilo la kikatili. Mauaji hayo ambayo yalidhihirisha tena uhasama na chuki za Wazayuni wa Israel dhidi ya Waislamu, yalilaaniwa na Waislamu kote duniani.
Ukatili huo ulizusha wimbi kubwa la machafuko katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu za Palestina ambapo wananchi walizidisha mapambano dhidi ya maghasibu wa Tel Aviv. Israel ilimshika kwa muda na kumuachia huru mhalifu huyo katili kwa kisingizio kwamba alikuwa punguani! ***
Na siku kama ya leo miaka 26 iliyopita sawa na tarehe 7 Isfand 1377 Hijria Shamsia, duru ya kwanza ya uchaguzi wa Mabaraza ya Kiislamu ya Miji na Vijiji ulifanyika katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kwa muktadha huo kukawa kumefikiwa moja ya lengo jingine miongoni mwa malengo matukufu ya taifa la Kiislamu la Iran.
Kwa kufanyika uchaguzi huo kwa hamasa, asasi na ngome ya wananchi ya Mabaraza ya Kiislamu ya Miji na Vijiji katika uga wa kiutawala ikawa imepata dhihirisho la kivitendo.
Kuundwa Mabaraza ya Kiislamu ya Miji na Vijiji zaidi ya 33,000 katika maeneo mbalimbali ya Iran, ikawa ni hatua moja mbele katika uga wa kuingia na kuweko ushiriki wa wazi wa wananchi wote katika uchukuaji maamuzi ya nchi.
