Jumatano, tarehe 26 Februari, 2025
Leo ni Jumatano 27 ya Sha'ban 1446 Hijria mwafaka na 26 Februari 2025.
Tarehe 26 Februari miaka 223 iliyopita alizaliwa mshairi na mwandishi mashuhuri Mfaransa, Victor Hugo.
Hugo alikuwa akitetea uhuru na usawa kwa ajili ya matabaka ya watu wote masikini. Hugo alikubaliwa kujiunga na chuo kikuu na wakati huo huo akawa mwanachama wa Baraza la Kutunga Sheria akiwa na umri wa miaka 25.
Kutokana na upinzani wake dhidi ya utawala wa ukandamizaji wa Napoeleon wa Tatu alilazimika kuachana na masuala ya siasa na akaishi uhamishoni kwa kipindi cha miaka 20. Katika kipindi hicho Hugo aliandika vitabu muhimu na vya thamani.
Miongoni mwa vitabu hivyo ni "Watu Masikini," "The Hunchback of Notre-Dame," " The Man Who Laughs" na "Toilers of the Sea". Victor Hugo alifariki mwaka 1885.

Miaka 180 iliyopita katika siku kama ya leo aliuawa Sayyid Ali Muhammad Shirazi aliyekuwa mashuhuri kwa lakabu ya “Bab” ambaye alidai kuwa ndiye Imam Mahdi (AF) na baadaye akadai kuwa ni Mtume.
Alizaliwa mwaka 1235 Hijria Qamariya katika mji wa Shiraz nchini Iran na alionekana kuwa na itikadi potofu akiwa bado shuleni. Muhammad Ali Bab ambaye hakuwa na elimu ya juu, alifuatwa na watu majahili na kuungwa mkono na wakoloni. Baada ya kudai kuwa ndiye Imam wa mwisho katika kizazi cha Mtume Muhammad (saw) yaani Imam Mahdi (AF), Bab alikwenda mbali zaidi na kudai kuwa ni Mtume wa Mwenyezi Mungu na kwamba dini ya Uislamu imefutwa.
Wanazuoni wa zama hizo walifichua urongo wake na kuchukulia hatua. Hata hivyo aliendelea kulingania itikadi zake potofu na katika siku kama ya leo, Amir Kabiir aliyekuwa kiongozi wa zama za Qajar, alitoa amri ya kunyongwa kwake.
Siku kama ya leo miaka 122 iliyopita, alifariki dunia, mvumbuzi wa Marekani kwa jina la Richard Jordan Gatling.
Getling alizaliwa mwaka 1818 na katika umri wake alivumbua vitu kadhaa moja wapo ikiwa ni bunduki iliyopewa jina lake ya Getling.
Bunduki ya Getling ina mabomba kadhaa ambayo baada ya ufyatuaji kila moja huzunguka na kuachia risasi kwa hatua, na kuipa uwezo wa kufyatua risasi nyingi kwa wakati mmoja. Mzunguko wa mabomba hayo ulitengenezwa na Richard Jordan Gatling mwenyewe.
Katika siku kama hii ya leo miaka 9 iliyopita aliaga dunia mtengezaji filamu mashuhuri wa Iran, Farajullah Salahshur. Alizaliwa mwaka 1331 Hijria Shamsia katika mji wa Qazvin.
Farajullah Salahshur, ametengeneza filamu nyingi maarufu kama ile ya kisa cha Maisha ya Nabii Yusuf (as), kisa cha As’habul Kahf na maisha ya Nabii Ayyub (as). Filamu hizo hasa ile ya kisa cha maisha ya Nabii Yusuf (as) zimewavutia watazamaji wengi duniani.
Kabla ya kufariki dunia, Salahshur alikuwa ameshaandika kisa cha filamu ya maisha ya Nabii Musa AS. Uchukuaji filamu ya kisa hicho ulipangwa kuanza miezi michache kabla ya kifo chake, lakini hilo halikuwezekana kutokana na ugonjwa wa saratani ya mapafu ulioishia kwenye kifo chake. ****
Na leo tarehe 8 Esfand katika kalenda ya mwaka wa Kiirabu ni siku ya kumbukumbuka na kumuenzi mwanafalsafa mkubwa wa Kiislamu na Kiirani, Mulla Hadi Sabzevari.
Mulla Sabzevari anatambuliwa kuwa mwanafalsafa mkubwa zaidi wa Kiislamu wa karne ya 13.
Mulla Hadi Sabzevari alizaliwa mwaka 1212 Hijria na alitumiwa umri wake ulijaa baraka katika zuhdi na uchamungu. Athari za Mulla Hadi Sabzevari zinaonyesha kwamba, alimu huyo mkubwa wa Kiislamu mbali na kwamba alikuwa mmoja wa wanafalsafa wakubwa, pia alitabahari katika uwanja wa elimu ya sheria za Kiislamu (fiq'hi), tafsiri ya Qur'ani, mantiki, hisabati, fasihi na elimu ya tiba.
Miongoni mwa athari za mwazuoni huyo ni pamoja na 'Mandhumah' katika uwanja wa elimu ya mantiki, 'Asraarul-Hikam' na 'al-Jabru Wal-Ikhtiyaar.'
