Feb 27, 2025 02:31 UTC
  • Alkhamisi, Februari 27, 2025

Leo ni Alkhamisi tarehe 28 Shaaban 1446 Hijria inayosadifiana na tarehe 27 Februari mwaka 2025 Milaadia.

Katika siku kama ya leo miaka 816 iliyopita alifariki dunia Ibn Hajib, mtaalamu wa Hadithi na mwanahistoria maarufu wa Kiislamu.

Ibn Hajib alizaliwa mwaka 593 Hijiria huko Damascus, Syria na kuelekea kwenye miji tofauti kwa ajili ya kusomea elimu ya Hadithi kutoka kwa wasomi wakubwa wa wakati huo.

Alitambuliwa kuwa gwiji wa elimu ya Hadithi katika zama zake kutokana na umahiri wake mkubwa katika taaluma hiyo. Mwanazuoni huyo ameandika vitabu kadhaa.

Katika siku kama ya leo miaka 123 iliyopita, alizaliwa John Steinbeck mwandishi wa riwaya wa Kimarekani.

Katika kipindi cha ujana wake alijishughulisha na kazi mbalimbali kabla ya kuchagua kazi ya uandishi ambako alionesha kipawa kikubwa. Mashaka ya kimaisha yalimtayarishia John Steinbeck mazingira mazuri ya kueleza kwa ufasaha maisha ya watu dhaifu na maskini katika jamii ya Marekani.

Alikuwa hodari mno katika kueleza mandhari, matukio na hali mbalimbali. Steinbech ameandika vitabu vingi kama Of Mice and Men, Bombs Away na Cup of Gold. 

John Steinbeck

Miaka 49 iliyopita katika siku kama hii ya leo harakati ya Polisario ilitangaza uhuru wa Jamhuri ya Kiarabu ya Sahara. Jamhuri hiyo iko kaskazini magharibi mwa Afrika katika pwani ya Bahari ya Atlantic na ina ukubwa wa kilomita mraba laki mbili na 84 elfu na jamii ya watu karibu laki sita.

Jamii ya Jamhuri ya Kiarabu ya Sahara inaundwa na watu wa kaumu mbalimbali za kiarabu, Barbar, Hassaniya na Tuareg. Mwaka 1975 wakoloni wa kihispania waliikabidhi ardhi ya Sahara kwa Morocco baada ya mapambano ya miaka mingi ya watu wa eneo hilo.

Baada ya kuondoka wakoloni wa Kihispania, harakati ya Polisario ilitangaza uhuru wa nchi hiyo kwa kuunda Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kiarabu na kukataa utawala wa Morocco na Mauritania katika ardhi ya eneo hilo. Mwaka 1979 Mauritania pia ilitupia mbali madai ya kumiliki eneo hilo la Sahara lakini Morocco ingali inadai kuwa ni sehemu ya ardhi yake.

Lugha rasmi ya watu wa Sahara ni Kiarabu na asilimia 99 ya wakazi wake ni Waislamu.   ***

Katika siku kama ya leo miaka 14 iliyopita, alifariki dunia Waziri Mkuu wa zamani wa Uturuki Najmuddin Erbakan akiwa na umri wa miaka 84.

Baada ya kuhitimu katika Chuo Kikuu cha Istanbul, Erbakan alijiunga na Chuo Kikuu cha Aachen nchini Ujerumani ambako alipata shahada ya uzamivu. Mwaka 1969 Najmuddin Erbakan aliingia katika uwanja wa siasa na kuchaguliwa kuwa Mbunge.

Mwaka 1987 aliongoza chama chenye mielekeo ya Kiislamu cha Refah ambacho kilipata viti vingi vya bunge na kumteuwa kuwa Waziri Mkuu mwaka 1996. Tukio hilo liliwakasirisha mno wanasiasa wa kilaiki wa Uturuki, Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Serikali ya Erbakan ilipigwa vita na jeshi la Uturuki na miezi 10 baadaye chama cha Refah kilivunjwa na wanajeshi, na mwanasiasa huyo akapigwa marufuku kujishughulisha na masuala ya kisiasa kwa kipindi cha miaka 5. Profesa Najmuddin Erbakan anatambuliwa kuwa baba wa harakati ya Kiislamu ya Uturuki.   

Najmuddin Erbakan