Feb 28, 2025 02:42 UTC
  • Ijumaa, tarehe 28 Februari, 2025

Leo ni Ijumaa tarehe 29 Shaaban 1446 Hijria sawa 28 Februari 2026.

Siku kama ya leo miaka 1219 iliyopita, yaani 29 Shaaban mwaka 219 Hijria Qamaria alifariki dunia Fadhlu Bin Dukin maarufu kwa jina la Ibn Naim, mtaalamu wa hadithi, fiq'hi na mwanahistoria.

Ibn Naim aliyezaliwa mwaka 130 Hijiria nchini Iraq, alikuwa mmoja wa wapokezi wa hadithi huku akipewa heshima na maulama wakubwa wa Kiislamu wa enzi hizo. Kitabu cha 'al-Swalat' ni miongoni mwa vitabu vya msomi huyo mkubwa wa Kiislamu.   

Tarehe 29 Shaaban miaka 1128 iliyopita sawa alifariki dunia Ibn Mundhir, mtaalamu wa sheria za Kiislamu, mfasiri wa Qur'ani Tukufu na mtaalamu wa hadithi wa Kiislamu.

Ibn Mundhir alijifunza elimu ya fiq'hi na hadithi kutoka kwa wasomi wakubwa wa zama zake huku akifanya safari pia kuelekea mjini Makkah, ambapo alisikiliza na kujifunza elimu ya hadithi hadi mwisho wa uhai wake. Aidha akiwa mjini Makkah alijishughulisha na uandishi wa vitabu tofauti.

Katika kitabu cha 'Al-Ijmaa' alibainisha na kufafanua nadharia tofauti za wasomi katika uwanja wa sheria za Kiislamu. 

Siku kama ya leo miaka 503 iliyopita, ilianza harakati ya mapinduzi ya wananchi wa Sweden dhidi ya utawala wa Christiane wa Pili, mtawala wa Denmark ambaye alizikalia kwa mabavu Sweden na Norway.

Kiongozi wa harakati hiyo alikuwa Gustav Vasa. Hatimaye kwa msaada wa wakulima, wananchi na wafuasi wa Uprotestanti, Vasa alifanikiwa kuikomboa nchi hiyo kutoka mikononi mwa mtawala Christiane wa Denmark. Baada ya mapinduzi hayo, Gustav Vasa akawa kiongozi wa Sweden.

Silsila ya utawala wa Vasa ulioendelea kwa karibu karne tatu, iliondolewa madarakani mwaka 1818 na Marshall Baptiste Bernadotte, mmoja wa makamanda wa jeshi la Ufaransa.

Gustav Vasa

Siku kama ya leo miaka 492 iliyopita, alizaliwa Michel de Montaigne, mtaalamu wa falsafa wa Ufaransa.

Akiwa kijana mwenye umri wa miaka 13, Montaigne alijiunga na chuo kikuu cha Toulouse na kusomea taaluma la sheria. Baada ya masomo yake alianza kufanya kazi za mahakama huku akifanya utafiti juu ya falsafa.

Montaigne ameandika vitabu kadhaa, muhimu zaidi kikiwa ni kitabu cha ‘Makala’ chenye juzuu tatu kinachozungumzia masuala mbalimbali. Michel de Montaigne alifariki dunia mwaka 1592. 

Siku kama ya leo miaka 103 iliyopita sawa na tarehe 28 Februari 1922, nchi kongwe ya Misri ilipata uhuru.

Misri ilikombolewa na Waislamu miaka 20 baada ya kudhihiri dini tukufu ya Kiislamu. Mwaka 969 nchi hiyo ilidhibitiwa na kutawaliwa na silsila ya wafalme wa Fatimiyya hadi mwaka 1172 ambapo utawala huo ulipinduliwa na Maayyubi.

Baada ya hapo Misri ilidhibitiwa na tawala tofauti. Waingereza walianza kuwa na ushawishi huko Misri katika miongo ya mwishoni mwa karne ya 19. Hata hivyo wananchi wa Misri walikabiliana na ukoloni wa Uingereza na mwanzoni mwa Vita vya Kwanza vya Dunia hapo mwaka 1914 Uingereza iliitangaza Misri kuwa chini ya himaya yake.

Wananchi wa Misri walidumisha mapambano ya uhuru baada ya Vita vya Kwanza vya Dunia na kuilazimisha Uingereza kuutambua rasmi uhuru wa nchi hiyo hapo mwaka 1922. 

Miaka 40 iliyopita katika siku kama ya leo, inayosadifiana na tarehe 28 Februari 1986, aliuawa Olof Palme Waziri Mkuu wa zamani wa Sweden baada ya kufyatuliwa risasi tumboni kwenye shambulio lililofanyika barabarani katikati mwa Stockholm, mji mkuu wa nchi hiyo.

Katika shambulio hilo, Bi. Lisberth mke wa Olof pia alijeruhiwa mgongoni. 

Olof Palme

Na siku kama ya leo miaka 35 iliyopita inayosadifiana na 28 Februari 1991, George Bush "baba" alitangaza usitishaji vita vya Ghuba ya Uajemi vilivyoendelea kwa muda wa siku 40.

Mgogoro huo ulianza mwezi Agosti 1990 baada ya majeshi ya Iraq kushambulia ghafla sehemu ya ardhi ya Kuwait na kuikalia kwa mabavu.

Ndege za kijeshi za Marekani, Uingereza na Ufaransa zilianza kuyashambulia majeshi ya Iraq baada ya utawala wa Saddam Hussein kukataa amri ya kuyaondoa majeshi yake nchini Kuwait.