Mar 11, 2025 02:33 UTC
  • Jumanne, Machi 11, 2025

Leo ni Jumanne tarehe 10 Ramadhani 1446 Hijria inayosadifiana na tarehe 11 Machi mwaka 2025.

Siku kama ya leo miaka 1449 iliyopita yaani tarehe 10 Ramadhani miaka mitatu kabla ya Hijra, alifariki dunia Bibi Khadija binti Khuwailid mke mwema na kipenzi wa Mtume Muhammad (saw) katika mji wa Makka.

Bibi Khadija ambaye alikuwa mmoja wa wanawake mashuhuri na tajiri wa Makka, aliolewa na Mtume Muhammad (saw) miaka 15 kabla ya kubaathiwa mtukufu huyo. Bibi Khadija alikuwa mtu wa kwanza kuamini ujumbe wa Mtume Muhammad (saw) na alitumia uwezo na utajiri wake katika kuisaidia dini ya Uislamu. Kuweko Bibi Khadija (as) pamoja na Mtume wa Uislamu kulikuwa na umuhimu mkubwa kiasi kwamba Mtume (saw) alikitaja kifo cha mkewe huyo kipenzi kuwa ni msiba mkubwa.

Mtume aliutaja mwaka aliofariki dunia Bibi Khadija na msaidizi wake mwingine mkubwa yaani Abu Talib, kuwa mwaka wa majonzi na huzuni. Hii ni kwa sababu Abu Talib, ami yake Mtume (saw), pia alifariki dunia mwaka huo huo. 

Siku kama ya leo miaka 1121 iliyopita kisiwa cha Malta maarufu kama "Herini ya Mediterania" kilitwaliwa na Waislamu na kuunganishwa na mamlaka ya nchi za Kiislamu.

Utawala wa Waislamu wa kisiwa cha Malta uliendelea hadi mwaka 1091 yaani hadi zama za udhibiti wa kaumu ya Norman kisiwani humo.

Malta ambayo inaundwa na visiwa vingi vidogo na vikubwa ina ukubwa wa kilomita mraba 316 na jamii ya watu karibu nusu milioni. 

Siku kama ya leo miaka 40 iliyopita, mgogoro mkubwa katika ngazi za uongozi wa Urusi ya zamani ulifikia kikomo kufuatia kutangazwa kifo cha Konstantin Chernenko na badala yake Mikhail Gorbachev ambaye wakati huo alikuwa mwanachama kijana zaidi katika Idara ya Siasa ya Chama cha Kikomunisti akatangazwa kuchukua nafasi ya Chernenko.

Hatua ya kuchaguliwa Gorbachev kuongoza chama hicho cha Kikomunisti ilikwenda sambamba na kujiri mabadiliko makubwa, ambayo hatimaye yalipelekea kusambaratika Umoja wa Kisovieti.  ***

Siku kama ya leo miaka 21 iliyopita yaani mwaka 2004, watu karibu 200 waliuliwa na wengine 1000 kujeruhiwa kufuatia miripuko 5 ya mabomu iliyotokea kwenye vituo kadhaa vya treni ya chini ya ardhi (Metro) mjini Madrid, Uhispania.

Miripuko hiyo inahesabiwa kuwa ni miongoni mwa vitendo vikubwa vya kigaidi kuwahi kutokea Uhispania na Ulaya tangu mwishoni mwa vita vya Pili vya Dunia.

Baada ya kutokea miripuko hiyo serikali ya wakati huo nchini humo iliituhumu kundi la Eta Basque ambalo linadai kujitenga na utawala wa nchi hiyo, kwamba ndilo lililohusika na miripuko, hata hivyo kundi la Al Qaida lilitangaza kuhusika katika miripuko hiyo.

Miripuko hiyo ya Machi 11 ilitokea wakati chama cha Socialist kikiwa kimeshinda katika uchaguzi wa Bunge nchini humo na kuondoka vikosi vya Uhispania nchini Iraq. ****

Na miaka 14 iliopita katika siku kama ya leo yaani Machi 11 mwaka 2011, tetemeko la ardhi lililokuwa na ukubwa daraja 9 kwa kipimo cha Rishta lililikumba eneo la Tohoku lililopo mkoa wa Miyagi Mashariki mwa Japan.

Tetemeko hilo lilipelekea kuuawa kwa watu elfu 12 na malaki kadhaa ya wengine kubakia bila makazi kufuatia tetemeko hilo ambalo halijawahi kutokea mfano wake tangu makumi ya miaka yaliyopita nchini humo. Tetemeko hilo lilibomoa miundombinu, makazi ya raia na taasisi mbalimbali na kuiletea hasara ya mabilioni ya pesa nchi hiyo, kiasi kwamba kwa muda kadhaa Japan ilikuwa katika hali mbaya ya kiuchumi.

Tetemeko hilo lilizua mawimbi ya Tsunami yaliyokuwa na mwinuko wa mita 15, huku mawimbi mengine madogo madogo yakizikumba nchi nyingine za jirani kufuatia tetemeko hilo.   

Zilzala ya Fukushima