Ijumaa, tarehe 14 Machi, 2025
Leo ni Ijumaa tarehe13 Ramadhani 1446 Hijria sawa na Machi 14 mwaka 2025.
Siku kama ya leo miaka 1351 iliyopita inayosadifiana na tarehe 13 Ramadhani mwaka 95 Hijria, alifariki dunia Hajjaj bin Yussuf Thaqafi liwali katili na dhalimu wa Iraq katika kipindi cha utawala wa Bani Umayyah.
Hajjaj bin Yussuf Thaqafi aliyeishi katika kipindi cha wafalme wa Bani Umayyah, Abdul Malik Marwan na Hisham bin Marwan, alikuwa katili na mashuhuri kwa kuwatesa na kuwaua wapinzani wa utawala wa Bani Umayyah, hasa wafuasi wa Imam Ali bin Abi Talib AS na watu wa familia ya Mtume Muhammad SAW. Baadhi ya wanahistoria wameandika kuwa, zaidi ya watu 120,000 waliuawa kutokana na amri iliyotolewa moja kwa moja na Hajjaj bin Yussuf Thaqafi.
Miongoni mwa jinai zilizowahi kufanywa na Hajjaj bin Yusuf ni kuushambulia mji mtakatifu wa Makka na kuharibu al Kaaba mwaka 74 Hijria.

Siku kama ya leo miaka 146 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 14 Machi 1879 alizaliwa Albert Einstein, msomi mashuhuri wa fizikia na hisabati nchini Ujerumani.
Mnamo mwaka 1921 msomi huyo alipewa tuzo ya Nobel katika taaluma ya fizikia, baada ya kufanya juhudi kubwa za kiutafiti. Utafiti na nadharia za Einstein katika uwanja wa nyuklia zilikuwa na taathira kubwa duniani. Hata hivyo Einstein alisikitika sana baada ya kugundua kwamba uchunguzi na utafiti wake katika uwanja wa atomu umetumiwa na baadhi ya nchi kwa ajili ya kutengeneza silaha hatari za nyuklia.
Albert Einstein alifariki dunia 1955.
Katika siku kama ya leo miaka 142 iliyopita alifariki dunia Karl Heinrich Max mwanafalsafa wa Kijerumani na mwasisi wa nadharia ya Umaksi.
Karl Max aliyezaliwa katika familia ya Kiyahudi alisomea sheria na baadaye historia na falsafa. Kwa muda fulani mwanafalsafa huyo wa Kijerumani alikuwa mkuu wa jarida moja na mwaka 1848 alishirikiana na mwanafalsafa mwenzake wa Kijerumani na kubainisha imani, maoni na mitazamo yake katika kitabu walichokiandika na kukipa jina la "Manifesto ya Ukomonisti."
Miaka miwili baadaye Max alibaidishwa kutokana na kujishughulisha na harakati za kisiasa.
Miaka 71 iliyopita yaani mnamo mwaka 1954 tarehe 14 mwezi Machi vilianza vita vya kihistoria na vikubwa vilivyojulikana kwa jina la vita vya" Dien Bien Phu" ambavyo viliainisha mustakbali wa wanajeshi wa kikoloni wa Ufaransa huko Indochina.
Katika vita hivyo wapiganaji wa harakati ya wanamapinduzi ya Viet Minh waliokuwa wakipigania ukombozi wa Vietnam walipambana na jeshi la wakoloni wa Kifaransa waliokuwa katika ngome ngumu kudhibitiwa ya Dien Bien Phu.
Hatimaye tarehe 7 Mei mwaka huo huo vita hivyo vilifikia tamati kwa kusalimu amri kamanda wa majeshi ya Ufaransa aliyekuwa katika ngome ya Dien Bien Phu.
Vita hivyo viliwafungisha virago wakoloni wa Ufaransa nchini Vietnam.

Katika siku kama ya leo miaka 47 iliyopita, yaani tarehe 14 Machi 1978, jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel lilianza kuivamia na kuikalia kwa mabavu ardhi ya Lebanon kwa kisingizio cha kukabiliana na operesheni iliyofanywa na wanamapambano wa Kipalestina pambizoni mwa Tel Aviv.
Katika mashambulio hayo jeshi la Israel liliua raia wengi wasio na hatia wa Lebanon na Palestina na kuikalia kwa mabavu sehemu ya ardhi ya Lebanon.
Hata hivyo utawala huo ghasibu uliondoka kwa fedheha katika maeneo ya kusini mwa Lebanon mwaka 2000 baada ya kupata kipigo kikali kutoka kwa wanamapambano shupavu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Hizbullah na kuondoka kwenye eneo hilo.

Siku kama ya leo miaka 45 iliyopita uchaguzi wa Majlisi ya kwanza ya Ushauri ya Kiislamu yaani Bunge la kwanza la Iran baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ulifanyika hapa nchini na hivyo kutimiza moja ya malengo ya mapinduzi hayo.
Kwa sasa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran ina wawakilishi 290 ambao huhudumu bungeni kwa kipindi cha miaka 4.
Wafuasi wa dini za waliowachache nchini Iran kama Wakristo na Wayahudi pia kwa uchache huwa na mwakilishi mmoja katika Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu.
Miaka 40 iliyopita katika siku kama ya leo, vibaraka wa madola ya kigeni walilipua bomu katika hadhara kubwa ya waumini waliokuwa wamekusanyika kwa ajili ya ibada muhimu ya Sala ya Ijumaa mjini Tehran na kuwaua shahidi waumini kadhaa pamoja na kuwajeruhi wengine wengi.
Sambamba na kutekelezwa kwa kitendo hicho cha kigaidi dhidi ya raia wasio na hatia, ndege za kivita za Iraq ziliruka na kuingia katika anga ya mji mkuu Tehran kama tishio la kuonyesha kwamba, mji huu ulikuwa chini ya mashambulio.
