Jumapili 16 Machi 2025
Leo ni Jumapili tarehe 15 Ramadhani 1446 Hijria, sawa na tarehe 16 Machi 2025.
Siku kama ya leo miaka 1443 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Hijria, alizaliwa Imam Hassan al-Mujtaba (as), mjukuu wa Mtume Muhammad (saw).
Imam Hassan (as) alikulia katika malezi na usimamizi wa Mtume, Bibi Fatmatu al Zahra, binti wa Mtume, na Imam Ali bin Abi Twalib (as).
Baada ya kuuawa shahidi baba yake, yaani Imam Ali hapo mwaka wa 40 Hijria, mtukufu huyo alifanya kazi kubwa ya kusimamia na kuwaongoza Waislamu. Mwanzoni, Waislamu wengi walimbai na kumpa mkono wa utiifu Imam Hassan, lakini utawala wa Bani Umayyah uliokuwa ukiongozwa na Muawiya mwana wa Abu Sufiyan ambao wakati huo ulikuwa na nguvu kubwa, ulianzisha uadui na chuki dhidi ya mjukuu huyo a Mtume.
Hatimaye Imam Hassan (as) alijiandaa kukabiliana na utawala dhalimu wa Bani Umayyah, lakini viongozi wengi wa jeshi lake walidanganyika na ahadi za uongo za Muawiya na kumuacha peke yake, hali iliyomlazimu mtukufu huyo kufanya suluhu na mtawala huyo wa Bani Umayyah kwa lengo la kuhifadhi dini tukufu ya Uislamu.

Miaka 86 iliyopita katika siku kama ya leo, katika hali ambayo Vita vya Pili vya Dunia havikuwa vimeanza, nchi ya Czechoslovakia ilivamiwa na kukaliwa kwa mabavu na Ujerumani ya Kinazi.
Kwa utaratibu huu, Jamhuri ya Czechoslovakia ikawa nchi ya pili baada ya Austria kukaliwa kwa mabavu na Adolph Hitler.

Siku kama ya leo miaka 85 iliyopita, alifariki dunia Bi Selma Lagerlof mwandishi wa Sweden.
Lagerlof alizaliwa mwaka 1858 na baada ya kumaliza masomo yake akaanza kujishughulisha na ukufunzi na uandishi wa hadithi na hekaya.
Selma Lagerlof alikuwa mwanamke wa kwanza kutunukiwa tuzo ya Nobel katika taaluma ya fasihi mwaka 1909.
Siku kama ya leo miaka 48 iliyopita, Kamal Fouad Jumblatt mwanasiasa mahiri wa Lebanon aliuawa.
Alizaliwa Disemba 6 mwaka 1917 huko Moukhtara kusini mwa Beirut. Mwaka 1952 na kuendelea, Kamal Fouad Jumblatt alikuwa mwanasiasa wa mrengo wa upinzani na akafanikiwa kumuondoa madarakani Bechara El Khoury Rais wa muda wa wakati huo wa Lebanon.
Hatimaye Kamal Fouad Jumblatt aliuawa na wapinzani wake katika siku ma ya leo akiwa na umri wa miaka 60.
Na katika siku kama ya leo miaka 30 iliyopita, sawa na tarehe 26 mwezi Esfand mwaka 1373 Hijria Shamsiya aliaga dunia Hujjatul Islam Walmuslimin Sayyid Ahmad Khomeini, mwana wa Imam Ruhullah Khomeini, Mwenyezi Mungu amrehemu, mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Sayyid Ahmad Khomeini alizaliwa mwaka 1324 Hijria Shamsiya katika mji mtukufu wa Qum nchini Iran na kuanza kujifunza elimu ya kidini kwa baba yake.
Sayyid Ahmad Khomeini alikuwa na nafasi muhimu katika kuwaunganisha wanamapinduzi na Imam Khomeini wakati wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran.