Mar 17, 2025 02:38 UTC
  • Jumatatu, tarehe 17 Machi, mwaka 2025

Leo ni Jumatatu tarehe 16 Ramadhani 1446 Hijria sawa na tarehe 17 Machi mwaka 2025.

Miaka 1389 iliyopita katika siku kama hii ya leo, ardhi ya Baitul Muqaddas huko Palestina ilikombolewa na Waislamu.

Vita vya kwanza kati ya Waislamu na Warumi vilijiri huko kaskazini mwa Bahari Nyekundu baada ya kudhihiri Uislamu. Jeshi la Waislamu lilitoa pigo kwa Warumi na eneo la kusini mwa Palestina likakombolewa katika zama za utawala wa Umar bin Khattab.

Baada ya kushindwa huko, mfalme wa Roma alituma jeshi kubwa katika ardhi za Palestina. Warumi walishindwa vibaya na jeshi la Kiislamu katika vita vilivyojiri huko Palestina na mwishoni mwa mapigano hayo, kamanda wa jeshi la Roma aliuawa na Damascus ikadhibitiwa na Waislamu.

Katika siku kama hii ya leo miaka 600 iliyopita alifariki dunia mwanazuoni na mwanahistoria wa Kiislamu, Taqiyyuddin Abul Abbas Maqrizi.

Maqrizi alizaliwa Cairo nchini Misri na alifanya safari katika miji mingi ya Ulimwengu wa Kiislamu kwa shabaha ya kutafuta elimu na maarifa. Alikuwa hodari katika taaluma mbalimbali za Kiislamu. Kwa muda, Taqiyuddi al Maqrizi alijihusisha na kazi ya ukadhi mjini Cairo.

Alipendelea sana elimu ya historia na ameandika vitabu kadhaa katika taaluma hiyo. Miongoni mwa vitabu vya mwanahistoria huyo wa Kiislamu ni al Suluuk Limaarifati al Muluuk.

Siku kama ya leo miaka 77 iliyopita, wawakilishi wa nchi za Uingereza, Ufaransa, Ubelgiji, Uholanzi na Luxembourg, walitia saini mkataba  wa ushirikiano mjini Brussels, Ubelgiji.

Katika mkataba huo uliojulikana kwa jina la "Mkataba wa Brussels", nchi hizo zilikubaliana kuanzisha mfumo wa ulinzi wa pamoja na kupanua uhusiano wao wa kiuchumi na kiutamaduni. 

Mkataba huo pia ndio uliokuwa chachu ya kuanzishwa kwa Shirika la Kijeshi la Nchi za Magharibi NATO. Kwani ni baada ya hapo ndipo yalipofanyika mazungumzo kati ya Marekani, Canada na baadhi ya nchi wanachama wa Mkataba wa Brussels huko Washington, Marekani ambapo baadaye kuliundwa Shirika hilo la NATO mwezi Aprili 1949.