Mar 31, 2025 02:38 UTC
  • Jumatatu, tarehe 31 machi, 2025

Leo ni tarehe Mosi Shawwal 1446 Hijria inayosadifiana na tarehe 31 Machi 2025.

Tarehe Mosi Shawwal inayosadifiana na sikukuu ya Idul Fitr.

Idul Fitri ni miongoni mwa sikukuu kubwa katika dini tukufu ya Kiislamu. Baada ya kukamilisha ibada ya funga, kuomba na kujipinda kwa ibada katika mwezi mtukufu wa Ramadhani, Waislamu hufanya sherehe katika siku hii kubwa wakimshukuru Mola Manani kwa kuwawezesha kukamilisha ibada huyo.

Iddi al Fitr ni kuuaga mwezi mtukufu wa Ramadhani ambao ni mwezi wa ibada na kujisafisha. Katika siku kama hii ya leo ni haramu kufunga saumu yoyote na Waislamu baada ya juhudi za mwezi mzima za kupambana na nafsi na kuchuma matunda ya ucha-Mungu hukusanyika pamoja na kusali Sala ya Iddul Fitr.

Kuhusiana na utukufu wa siku hii Mtukufu Mtume (saw) anasema: "Mtu yeyote atakayemuasi Mwenyezi Mungu katika siku ya Idi, basi ni kama mtu aliyemuasi Mwenyezi Mungu siku ya miadi, yaani Siku ya Kiama." Kwa mnasaba wa siku hii adhimu, Redio Tehran inatoa mkono wa pongezi, heri na fanaka kwa Waislamu wote duniani.

Swala ya Iddi mjini Tehran

Siku kama ya leo miaka 1193 iliyopita yaani tarehe Mosi Shawwal mwaka 253, Hijria alifariki dunia mpokezi mashuhuri wa Hadithi wa Ahlusunna, Imam Muhammad Ismail Bukhari.

Abu Abdullah Muhammad Ismail aliyekuwa mashuhuri kwa jina la Imam Bukhari ni miongoni mwa wanazuoni wakubwa wa Hadithi wanaoaminiwa na Ahlusunna. Alisafiri sana kwa ajili ya kutafuta Hadithi za Mtume (saw).

Kitabu mashuhuri zaidi cha mwanazuoni huyo ni kile cha ‘Jamius Swahih’ maarufu kama Sahihi Bukhari. Vitabu vingine mashuhuri vya mwanazuoni huyo ni ‘Al-Adabul Mufrad’, ‘Al-Jaamiul-Kabiir’ na ‘Tarikhul-Kabir an Taraajam Rijaal-Sanad.’ 

Siku kama ya leo miaka 877 iliyopita, sawa na tarehe Mosi Shawwal mwaka 569 Hijiria alifariki dunia Said Bin Mubarak maarufu kwa jina la Ibn Dahhan, mfasiri, mwanafasihi na malenga wa Kiislamu.

Ibn Dahhan alizaliwa mjini Baghdad na baada ya kumaliza masomo yake ya awali, alianza kusoma lugha sambamba na kupokea hadithi kutoka kwa wanazuoni wakubwa wa zama zake.

Mtaalamu huyo mkubwa wa lugha alitilia maanani taaluma ya fasihi hususan katika kusoma mashairi na hivyo kuwa mfano wa kuigwa na wanafunzi wake katika usomaji mashairi. Aidha alilipa umuhimu mkubwa suala la kuhuisha baadhi ya vitabu vilivyosahaulika kiasi kwamba mwishoni alipoteza uwezo wake wa kuona katika kazi hiyo.

Miaka 840 iliyopita katika siku kama hii ya leo ya tarehe Mosi Shawwal alifariki dunia Abu Abdallah Muhammad bin Omar Razi mashuhuri kwa jina la Fakhrurazi msomi na mwanazuoni mashuhuri wa Kiislamu.

Alizaliwa katika mji wa Rey jirani na Tehran na alifanikiwa kwa haraka kujifunza elimu mbalimbali za Kiislamu kama fiqihi, tafsiri ya Qur'ani, falsafa na mantiki kutokana na kipaji kikubwa alichokuwa nacho.

Mwanazuoni huyo ameandika vitabu vingi. Kitabu muhimu zaidi cha Fakhrurazi ni Attafsirul Kabir. Vitabu vingine vya msomi huyu wa Kiislamu ni "Asrarul Tanzil", "Nahayatul-Uquul" na "Sirajul-Qulub". 

Miaka 429 iliyopita katika siku kama ya leo yaani tarehe 31 Machi mwaka 1596, alizaliwa Rene Descartes mwanafalsafa, mwanahisabati na mwanafizikia wa Kifaransa.

Descartes alifikia daraja ya uhadhiri wa chuo kikuu baada ya kuhitimu masomo ya falsafa na hisabati. Msomi huyo wa Kifaransa alifanya safari kwa kipindi fulani katika nchi mbalimbali na baadaye aliishi Uholanzi na kuanza kufanya utafiti.

Rene Descartes aliitambua hisabati kuwa ni elimu kamili miongoni mwa elimu nyinginezo na kutaka kutumiwa elimu hiyo katika taaluma nyinginezo. Miongoni mwa vitabu vya mwanafalsafa huyo ni Principles Of Philosophy, The Passions of the Soul na Discourse on the Method.

Rene Descartes

Siku kama ya leo miaka 77 iliyopita, garimoshi lililokuwa likitoka Cairo, Misri likielekea katika bandari ya Haifa huko Palestina lililipuriwa kwa bomu, ikiwa ni katika mwendelezo wa mauaji ya umati yaliyokuwa yakifanywa na Wazayuni maghasibu dhidi ya Wapalestina.

Wapalestina 40 waliuawa na wengine 60 kujeruhiwa katika jinai hiyo iliyofanywa na kundi moja la Kizayuni. Siku nne kabla ya mlipuko huo, garimoshi jingine lililipuliwa huko Palestina na Wazayuni waliokuwa na silaha na kuuwa Wapalestina 24. Wapalestina wengine 61 walijeruhiwa.  ***

Na siku kama ya leo miaka 46 iliyopita, nchi wanachama wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu zilisimamisha uanachama wa Misri katika jumuiya hiyo na nchi nyingi wanachama zikakata uhusiano wao na Cairo. Nchi za Kiarabu zilichukua msimamo huo mkali baada ya rais wa zamani wa Misri, Anwar Sadat, kusaini hati ya mapatano ya Camp David na utawala wa Kizayuni wa Israel mwezi Januari mwaka 1978.