Jumatano, tarehe Pili Aprili, 2025
Leo ni Jumatano tarehe 3 Shawwal 1446 Hijria sawa na Aprili Pili mwaka 2025.
Katika siku kama ya leo miaka 220 iliyopita, alizaliwa huko nchini Denmark, Hans Christian Andersen malenga, mwandishi na msimulizi wa visa maarufu vya watoto.
Andersen ambaye alikuwa mtoto wa bwana mmoja maskini na fundi viatu, alihamia Copenhagen mji mkuu wa Denmark na kuanza kucheza michezo ya kuigiza. Baada ya muda, Hans Andersen alianza kutunga visa na kuwa mashuhuri baada ya kuandika kitabu chake cha kwanza cha hadithi alichokipa jina la "Fairy Tales, Told for Children" mnamo mwaka 1838.

Miaka 423 iliyopita katika siku kama hii ya leo, vikosi vya jeshi la majini la Argentina vilivamia visiwa vya Falkland kwa jina jingine (Malvinas) na kuvidhibiti visiwa hivyo vya kiistratejia vilivyoko kusini mashariki mwa nchi hiyo.
Visiwa vya Falkland ambavyo kwa lugha ya Kiargentina vinatamkwa kama Malvinas, viligunduliwa katika karne ya 16 na kukaliwa kwa mabavu na Uingereza mwaka 1832.

Siku kama ya leo miaka 20 iliyopita, aliaga dunia Papa John Paul II aliyekuwa kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani.
Papa John Paul II alizaliwa mwaka 1920 huko Poland na kufikia daraja ya uchungaji baada ya kuhitimu masomo ya dini. Mwaka 1964 Papa John Paul alikuwa askofu wa mji wa Kraku huko Poland na miaka mitatu baadaye akawa Kadinali. Hatimaye mwaka 1978 John Paul wa Pili aliteuliwa kushika wadhifa wa ngazi ya juu zaidi wa kanisa Katoliki, yaani Papa.
Papa John Paul wa Pili alikuwa mfuasi wa mazungumzo baina ya dini mbalimbali hususan kati ya Uislamu na Ukristo. Alikuwa akipinga vikali utoaji mimba na ndoa za watu wa jinsia moja na ufisadi wa kimaadili kwa ujumla uliotanda katika ulimwengu wa Magharibi. Aidha alikosoa vikali mashambulio ya kijeshi ya Marekani dhidi ya Iraq.

Leo tarehe 13 Farvardin kwa mwaka wa Kiirani wa Hijria Shamsia ni "Siku ya Maumbile" nchini Iran
Wananchi katika kila pembe ya Iran leo Jumatano ya tarehe Pili Aprili inayosadifiana na tarehe 13 Farvardin kwa mujibu wa kalenda ya Hijria Shamsia wanapitisha kutwa ya siku yao katika maeneo ya wazi ya mandhari za maumbile ikiwa ni moja ya mila na desturi zao za jadi.
Katika kalenda rasmi ya Iran, tarehe 13 Farvardin imepewa jina la Siku ya Maumbile; maumbile ambayo tokea tangu na tangu yamekuwa yakienziwa na kutunzwa kwa unadhifu na kuheshimiwa na watu wa Iran.
Lakini pia tarehe 13 Farvardin, ambao ni mwezi wa kwanza katika mwaka wa Hijria Shamsia, ni siku ya mwisho ya mapumziko ya Sikukuu ya Nairuzi, na inajulikana kama Sizda Bedar. Tokea enzi za kale, baada ya siku 12 za furaha na sherehe kwa mnasaba wa kukamilisha miezi 12 ya mwaka, katika siku ya 13 ya Nairuzi, Wairani wamekuwa wakielekea kwenye maeneo ya mabustanini na uwandani ili kuipitisha siku ya mwisho ya Sikukuu katika mandhari za maumbile ya kijanikibichi kando ya mimea, mito na chemchemi za maji.
Katika zama tofauti za historia, watu wa Iran wamekuwa wakiiitambua Sikukuu ya Nairuzi kuwa ni sherehe ya kuadhimisha adhama ya uumbaji na kuhuika tena kwa maumbile katika msimu wa Machipuo (Spring) baada ya kufifia katika msimu wa Baridi Kali (Winter); na mwisho wa sherehe hizo huwa ni tarehe 13 Farvardin, ambayo kwao wao ni siku ya baraka na furaha kubwa
