Ijumaa, tarehe 11 Aprili, 2025
Leo ni Ijumaa tarehe 12 Shawwal 1446 Hijria sawa na tarehe 11 Aprili 2025.
Siku kama ya leo miaka 416 iliyopita aliaga dunia alimu na mwanazuoni mkubwa wa Kiislamu Sheikh Bahauddin Muhammad bin Hussein Amili maarufu kwa jina la Sheikh Bahai.
Sheikh Bahai ambaye alikuwa mtaalamu wa fiqhi, nujumu na hesabati alifariki dunia katika mji wa Isfahan nchini Iran. Alizaliwa mwaka 952 Hijria katika mji wa Baalabak huko Lebanon katika familia ya Kiirani.
Baba yake alikuwa miongoni mwa mashekhe wakubwa wa zama hizo. Sheikh Bahai ameandika vitabu vingi ikiwa ni pamoja na Tashrihul Aflak, Kashkul na Hablul Matin.

Tarehe 11 Aprili miaka 165 iliyopita chombo cha kuzalisha baridi kilibuniwa na mwanakemia wa Kifaransa kwa jina la Ferdinand Carre.
Kifaa hicho kilikuwa kikizalisha baridi kwa kutumia gesi ya ammonia. Ubunifu huo wa Carre ulikuwa hatua muhimu katika kuhifadhi vyakula ili visiharibike hususan katika maeneo yenye joto.
Uvumbuzi wa msomi huyo hatimaye ulipelekea kutengenezwa kwa majokofu na vifaa vingine vikubwa vya kuzalisha baridi kwa ajili ya shughuli mbalimbali.

Miaka 40 iliyopita katika siku inayosadifiana na hii ya leo aliaga dunia Enver Hoxha Rais wa zamani wa Albania.
Hoxha alikuwa kiongozi wa wapiganaji wa mrengo wa kushoto baada ya Italia kuivamia na kuikalia kwa mabavu Albania mwaka 1939. Enver Hoxha alichukua madaraka ya nchi mwaka 1944 kwa kusaidiwa na jeshi la Urusi ya zamani baada ya kushindwa Italia katika Vita vya Pili vya Dunia.
Rais huyo wa zamani wa Albania miaka miwili baadaye aliitangaza nchi hiyo kuwa ni Jamhuri ya Kikomonisti.
Siku kama ya leo miaka 28 iliyopita, siku moja tu baada ya mahakama moja ya Ujerumani kutoa hukumu dhidi ya viongozi kadhaa wa ngazi za juu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya ziliwaita nyumbani mabalozi wao kutoka mjini Tehran.
Jaji wa mahakama hiyo iliyopata umaarufu kwa jina la Mykonos aliathiriwa mno na misimamo ya Kizayuni na kutangaza kuwa viongozi wa Iran walihusika katika mauaji ya mpinzani wa utawala wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aliyekuwa akiishi Ujerumani.
Iran ilikadhibisha madai hayo na ikajibu hatua ya nchi hizo kwa kuwaita nyumbani mabalozi wake wote katika nchi za Umoja wa Ulaya. Uamuzi wa mahakama ya Mykonos kwa hakika ulikuwa sehemu ya hujuma ya kisiasa ilikuwa ikiongozwa na Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Takribani miezi kumi baadaye mabalozi wa Umoja wa Ulaya walianza kurejea hapa Tehran mmoja baada ya mwingine.
