Hadithi ya Uongofu (47)
Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh. Natumai hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. Kipindi chetu kilichiopita kilijadili na kuzungumzia amana na utunzaji amana. Kipindi chetu cha leo ambacho ni sehemu ya 47 ya mfululizo huu kitazungumzia baadhi ya athari za utunzaji amana. Kuweni nami hadi mwisho wa kipindi hiki.
Utunzaji amana ni miongoni mwa sifa njema za kiakhlaqi na kimaadili ambazo zina faida na athari nyingi ambazo zimetajwa katika hadithi na mafundisho matukufu ya Kiislamu. Miongoni mwa hadithi hizo ni ile iliyonukuliwa kutoka kwa Bwana Mtume SAW akisema: Kuhifadhi na kutekeleza amana huleta uwezo.
Kwa maneno hayo mbora huyo wa viumbe amebainisha faida za utunzaji amana yaani kuongezeka mali na kuwashajiisha watu kuelekea katika hilo. Katika Qur’ani Tukufu Mwenyezi Mungu anabainisha sifa za baadhi ya Mitume na kuwataja kwa majina kama Rasulun Amin (Mtume Mwaminifu), Naasihun Amin (Mwenye kunasihi ambaye ni mwaminifu, Swadiq al-Wa’ad (Mkweli katika ahadi) na kadhalika. Kwa mfano katika aya ya 107 ya Surat Shuaraa Mtukufu Nabii Nuhu AS anaiambia kaumu yake akisema:
“Hakika mimi kwenu ni Mtume muaminifu.” Maneno kama hayo pia tunayashuhudia kwa Mitume kama Hud, Swaleh na Mussa AS.
Utunzaji amana wa Mtume SAW ulikuwa maarufu kiasi kwamba, katika kipindi cha kabla ya kubaathiwa kwake alikuwa akijulikana baina ya Washirikina wa Makka kwa jina la Muhammad Amin yaani Muhammad Mwaminifu. Engo muhimu zaidi ya uaminifu wa Mitume wa Allah ilikuwa ni ukweli na utunzaji amana katika kuhifadhi na kufikisha ujumbe na risala ya Wahyi. Mtume SAW amenukuliwa katika hadithi inayopatikana katika Kitabu cha Kanzul Ummal akisema kwamba: Ninaapa kwa Mwenyezi Mungu kwa hakika mimi ni mtunza amana mbinguni na ardhini.
“Hakika mimi kwenu ni Mtume muaminifu.” Maneno kama hayo pia tunayashuhudia kwa Mitume kama Hud, Swaleh na Mussa AS.
Kwa hakika utunzaji amana ni kitendo chenye faida nyingi kwa mtu binafsi na kwa jamii kwa ujuma. Moja ya faida hizo muhimu ni kupata radhi ya Mwenyezi Mungu. Mtu mwenye kutunza amana mbali na kupata radhi na kuridhiwa na Mwenyezi Mungu hupata pia ujira wa kimaanawi wa kidunia hupata pia thawabu na ujira wa Kiakhera na mafikio yake yatakuwa ni peponi. Mtume SAW amenukuliwa katika hadithi inayopatikana katika Kitabu cha Bihar al-Anwar akisema kuwa: Kesho katika medani ya Kiyama mtu ambaye atakuwa karibu zaidi na mimi kuliko watu wengine ni yule ambaye ji mkweli zaidi, mtunzaji zaidi wa amana, mwenye kuchunga na kuheshimuzaidi makubaliano, mwenye tabia njema zaidi na ambaye yuko karibu zaidi na watu.
Katika sehemu nyingi Bwana Mtume SAW anaelezea jinsi utulivu na usalama wa umma wake na jamii kwa ujumla unavyoweza kupatikana kwa kusema:
Umma wangu utakuwa katika raha na salama madhali baina yao hawafanyiana hiana (usaliti) na ni wenye kutunza amana.
Kwa hakika kwa mtu muumini hakuna ombi na takwa la juu zaidi kama kupata radhi za Mwenyezi Mungu; kwani katika hali hii mwanadamu mwenye kutafuta ukamilifu na uhakika ataweza kufikia katika matumaini yake.
Imam Ali bin Abi Twalib AS anasema kuwa: Mwenyezi Mungu anapompenda mja basi hulifanya suala la utunzaji amana kuwa ni jambo analolipenda.
Kwa msingi huo kila mtu ambaye anapenda kuwa mwaminifu na ni mwenye kutunza amana anapendwa na Mwenyezi Mungu. Imam Mussa al-Kadhim AS anaitambua saada na ufanisi wa watu kuwa upo katika utunzaji amana na kuifanyia kazi haki. Anasema: Watu wa dunia watakuwa na maisha mazuri endapo wataogopa kufanya dhambi, wakalipa kipaumbele suala la utunzaji wa amana na wakaifanyia kazi haki.
Kupata radhi za watu na mafanikio katika dunia na akhera ni athari nyingine ya utunzaji wa amana. Mtu mwaminifu ni mwenye kuaminiwa na watu na kutokana na kufanya juhudi katika kutunza amana anazopatiwa na watu husifiwa na kuheshimiwa.
Kama ilivyotajwa ni kuwa, moja ya sifa mashuhuri za Mtume SAW ni tabia yake ya utunzaji amana, kiasi kwamba, hata Washirikina wa Makka walikuwa wakimuamini kupitia sifa na tabia hii na katika safari walizokuwa wakisafiri walikuwa wakiweka amana zao na ma;li zao kwa mbora huyo wa viumbe. Fauka ya hayo kitajiriba na kiakili, kikawaida watu ambao ni mashuhuri na watajika katika utunzaji amana hupendwa na kuaminiwa na watu. Imenukuliwa katika hadithi kutoka kwa Imam Ja’afar Swadiq AS kwamba alimwambia Abdul Rahman bin Siyabah:
Je nikuusia jambo jema? Abdul Rahman akasema, ndio ewe mjukuu wa Mtume SAW. Imam akasema: Hongera kwa kuwa mkweli na mtunzaji wa amana kwani katika hali hii utakuwa ni mshirika wa mali za watu.
Luqman al-Hakim, ni mmoja ya watu waliotajwa katika Qur’ani na kusifiwa na Mwenyezi Mungu. Katika hadithi zimenukuliwa hadithi na hekima zenye thamani kubwa kutoka kwa Luqman al-Hakim.
Luqman al-Hakim amenukuliwa katika Kitab cha Maan al-Akhbar akimuusia mwanawe kwa kusema:
Ewe mwanangu! Kuwa ni mwenye kutunza amana ili dunia na akhera yako ibakia kuwa salama. Kuwa ni mtunza amana ili uwe na uwezo.
Kwa hakika mtu ambaye ni mwaminifu kutokana na kulitanguliza mbele suala la utunzaji amana katika kila kazi yake na katika kila mazingira, hufanikiwa kufikiwa katika malerngo pamoja na natija inayofaa na katu hakumbwi na kuchanganyikiwa au kushindwa katika malengo yake. Imam Ali bin Abi Twalib AS anasema kuwa:
Ewe mwanangu! Kuwa ni mwenye kutunza amana ili dunia na akhera yako ibakia kuwa salama. Kuwa ni mtunza amana ili uwe na uwezo.
Utunzaji amana ni jukumu la Kimwenyezi Mungu, kwani kila mtu ambaye ambaye hatakuwa ni mtunza amana atakuwa amepata hasara na hawezi kufikia katika malengo.
Kwa mujibu wa mafundisho ya dini tukufu ya Kiislamu, utunzaji amana ni chimbuko la kuenea ukweli na usafgi wa kiroho wa mtu na jamii kwa ujumla. Mtume SAW anasema kuwa unapoona sifa tatu zimetimia kwa ndugu yako basi kuwa na matumainio naye. Haya, utunzaji amana na ukweli. Na kama hana sifa hizi basi usiwe na matumaini nae.
Nukta muhimu tunayopaswa kuiashiria ni hii kwamba, kama ambavyo katika Uislamu utunzaji amana inahesabiwa kuwa miongoni mwa sifa nzuri na inayosifiwa, hiana na usaliti pia katika amana ni jambo baya na linalokemewa na lipo katika orodha ya madhambi makubwa.
Mytume SAW anasema kuwa: Sio katika sisi mtu ambaye anafanya hiana katika amana.
Imam Ali bin Abi Twalib AS anasema kuwa: Mtu mbaya kabisa miongoni mwa waru ni yule ambaye hana imani na amana na utunzaji amana na hajiepushi na kufanya hiana katika amana.
Wapenzi wasikilizaji muda wa kipindi chetu kwa juma hili umefikia tamati, hivyo sina budi kukomea hapa tukutane tena wiki ijayo. Asanteni kwa kunitegea sikio na kwaherini.