Jumatano, tarehe 21 Mei, 2025
Leo ni Jumatano tarehe 23 Mfunguo Pili Dhulqaada 1446 Hijria mwafaka na tarehe 21 Mei 2025.
Siku kama ya leo miaka 2241 iliyopita, yaani tarehe 21 Mei mwaka 216 kabla ya kuzaliwa Nabii Isa (as), jeshi la mtawala wa Carthage chini ya uongozi wa Hannibal, lilishindwa vibaya huko kaskazini mwa Italia.
Hivyo vilikuwa vita vya pili baina ya utawala wa Carthage na Roma kwa anwani ya vita vya 'Punic.' Hannibal alishiriki vita hivyo kwa kutumia tembo na wapandaji tembo mahiri kabla ya kushindwa vibaya.

Siku kama ya leo miaka 104 iliyopita, alizaliwa Andrei Sakharov, mwanafizikia mashuhuri wa Russia.
Sakharov alihitimu taaluma ya fizikia katika chuo kikuu cha Moscow mwaka 1941 na kisha akaanza kufanya utafiti wa kina kuhusiana na nishati ya nyuklia. Alikuwa na nafsi muhimu katika utengenezaji wa bomu la hydrogen nchini Russia. Sakharov pia alikuwa muungaji mkono mkubwa wa harakati za kutokomeza silaha za nyuklia na ndio maana akatunukiwa zawadi ya amani ya Nobel hapo mwaka 1975.
Miaka mitano baadaye Sakharov alibaidishiwa katika mji wa Gorky, mashariki mwa Moscow kutokana na upinzani wake dhidi ya siasa za utawala wa kikomonisti wa Russia. Hata hivyo ubaidishaji huo ulifikia kikomo mwaka 1986 baada ya Mikhail Gorbachev kutwaa madaraka. Mwanzoni mwa mwaka 1989 Sakharov alichaguliwa kuwa mbunge katika bunge la Russia lakini akaaga dunia baadaye mwezi Disemba mwaka huohuo.

Katika siku kama ya leo miaka 34 iliyopita, Rajiv Gandhi, Waziri Mkuu wa zamani wa India, aliuawa kigaidi.
Rajiv Gandhi alikuwa mwanawe Indira Gandhi Waziri Mkuu wa zamani pia wa nchi hiyo. Alizaliwa tarehe 20 Agosti 1944 mjini Bombay na kulelewa katika nyumba ya babu yake Jawaharlal Nehru, Waziri Mkuu wa kwanza wa India. Rajiv Gandhi aliingia katika ulingo wa siasa baada ya kuaga dunia mdogo wake ambaye alikuwa akitayarishwa kumrithi kisiasa mama yake Indira Gandhi. Alichukua hatamu za kuiongoza India baada ya kuuliwa kigaidi mama yake hapo tarehe 31 Oktoba 1989.
Rajiv Gandhi alikuwa na nia ya kushiriki katika uchaguzi mkuu wa bunge lakini aliuawa na magaidi tarehe 21 Mei 1991 akiwa na umri wa miaka 47 alipokuwa akifanya kampeni za uchaguzi huo huko kusini mwa India.

Miaka 27 iliyopita na katika siku kama ya leo, Jenerali Muhammad Suharto wa Indonesia alilazimika kujiuzulu baada ya kuitawala nchi hiyo kwa mkono wa chuma kwa miaka 33.
Aliingia madarakani mwaka 1965 baada ya kumpindua Ahmad Sukarno, mwanzilishi wa Indonesia huru ambaye alikuwa amechaguliwa na wananchi wa nchi hiyo. Uhuru wa kisiasa ulibanwa sana katika kipindi cha utawala wa Suharto. Hata hivyo nchi hiyo ilishuhudia maendeleo makubwa ya kiuchumi katika utawala wake katika miongo ya 80 na 90. Pamoja na hayo lakini mgogoro wa kiuchumi uliozikumba nchi za Asia Mashariki katika mwaka wa 1997 ulianzisha malalamiko na maandamano makubwa ya wanafunzi wa Indonesia na taratibu yakachukua mkondo wa kisiasa uliopelekea Suharto kuondolewa madarakani.
Ufisadi wa kiuchumi uliofanywa na Suharto pamoja na familia yake ulichochea zaidi kuanguka kwa utawala wake, ambako kulitanguliwa na kujiuzulu kwake madarakani.
