Jumamosi, 19 Julai, 2025
Leo ni Jumamosi 23 Mfunguo Nne Muharram 1447 Hijria sawa na 19 Julai 2025 Miladia.
Katika siku kama ya leo miaka 238 iliyopita aliaga dunia Allamah Mulla Muhammad Mahdi Naraqi, mwanazuoni na msomi mkubwa wa Kiislamu. Baada ya kuhitimu masomo yake ya awali nchini Iran, msomi huyo mkubwa alielekea Hauza ya Najaf nchini Iraq kwa lengo la kuzidisha elimu ya kidini na alipata elimu kwa walimu mashuhuri wa zama hizo. Baada ya hapo Allamah Mulla Mahdi Naraqi alianza kufanya utafiti, kufundisha na kuandika vitabu. Miongoni mwa vitabu mashuhuri vya Allamah Naraqi ni "Jamiul Sa'adat" na " Anisul Muwahhidin".

Miaka 132 iliyopita alizaliwa malenga wa Russia kwa jina la Vladimir Mayakovsky. Mashairi ya Mayakovsky yalikuwa na nafasi kuu wakati wa mapinduzi ya Kikomonisti ya Urusi ya zamani mwaka 1917. Vladimir Mayakovsky alikuwa akiamini kuwa fasihi inapasa kuwa lugha ya watu wengi na inayobainisha maisha yao ya kijamii.

Siku kama ya leo miaka 76 iliyopita, nchi ya Laos iliyopo katikati mwa Asia, ilipata uhuru kutoka kwa Ufaransa. Nchi ya Laos yenye milima mingi, ipo baina ya Vietnam, Cambodia, Thailand, Myanmar na China huku ikiwa na jamii ya watu milioni tano. Kwa miaka mingi, nchi hiyo ilikuwa ikitawaliwa na uongozi wa kifalme. Mji mkuu wa nchi hiyo Vientiane una ukubwa wa kilometa 237 huku ukiwa kando ya mto maarufu wa Mekong. Laos haipakani na bahari yoyote, na chanzo chake kikuu cha maji ni mto huo wa Mekong.

Katika siku kama ya leo miaka 64 iliyopita, Kuwait ilipata uhuru kutoka kwa mkoloni Mwingereza. Katika kipindi cha utawala wa Achaemenid, Kuwait ilikuwa ikihesabiwa kuwa sehemu ya ardhi ya Iran. Mwaka 1899 Miladia, Kuwait iliwekeana saini na Uingereza, suala lililoifungulia London mlango wa kuikoloni nchi hiyo. Mwenendo huo uliendelea hadi baada ya Vita vya Pili vya Dunia. Kuwepo kwa visima vya mafuta kulipanua uingiliaji mkubwa wa mashirika mengi ya Uingereza na Marekani katika taifa hilo. Hatimaye mwaka 1961 Kuwait na Uingereza zilitiliana saini makubaliano yaliyoifanya nchi hiyo kujipatia uhuru wake.

Miaka 46 iliyopita katika siku kama ya leo mapinduzi ya wananchi wa Nicaragua yalipata ushindi dhidi ya dikteta Anastasio Somoza wa nchi hiyo na muitifaki wake mkubwa yaani Marekani. Dikteta huyo kibaraka wa Marekani alichukua hatamu za uongozi wa Nicaragua mwaka 1967 na tangu wakati huo wimbi kubwa la upinzani lilianza kuenea nchini kote na katika America ya Kati dhidi ya kiongozi huyo. Mapambano ya silaha ya wapiganaji wa msituni ya Harakati ya Ukombozi wa Kitaifa ya Sandinista (FSLN) yaliyoanza mwaka 1963 yalipamba moto zaidi katikati ya muongo wa 1970 na kuungwa mkono na wananchi. Hatimaye Somoza alilazimika kukimbia nchi baada ya jeshi la Sandinista kuingia Managua mji mkuu wa Nicaragua katika siku kama ya leo. Karibu watu elfu 40 waliuawa katika mapinduzi ya Nicaragua.

Katika siku kama hii ya leo miaka 20 iliyopita, Haram ya maimamu wawili, Ali al Hadi na Hassan al Askakri (as) huko Samarra, nchini Iraq walikozikwa wajukuu hao wawili wa Mtume Muhammad (saw) iliharibiwa na Mawahabi wa Kitakfiri wenye mafungamano na al-Qaeda. Magaidi wa kitakfiri, wakiongozwa na Abu Musab al Zarqawi, siku ya Jumatano, tarehe 23 ya Muharram 1427 mwendo wa saa 7:00 asubuhi, wakiwa wamevalia sare za askari wa Iraq, waliingia kwenye haram ya maimamu hao wawili na kuteka silaha za walinzi na pamoja na watumishi wa eneo hilo takatifu, na kulipua eneo hilo kwa kutumia milipuko ya TNT yenye uzito wa kilo 200. Nguvu ya mlipuko huu ilikuwa kubwa sana kiasi kwamba baadhi ya vifaa na jengo hilo nje vilirushwa umbali wa nusu kilomita.
