Ulimwengu wa Michezo, Agosti 8
Kwa matukio kemkem ya spoti yaliyogonga vichwa vya habari ndani ya siku saba zilizopita yakiwemo mashindano ya Olimpiki ya Rio..........
Kuanza kwa Olimpiki ya Rio
Mashindano ya Olimpiki ya Rio yaling'oa nanga siku ya Ijumaa katika uwanja wa Maracana mjini Rio de Janairo nchini Brazil, kwa mbwembwe ya aina yake huku nchi zinazoshiriki zikiwa na matarajio mengi ya kuvuna medali kochokocho. Hii ni duru ya 28 ya mashindano ya Olimpiki, ambapo jumla ya wachezaji 10,500 kutoka nchi 205 wanashiriki. Cha kuvutia zaidi, mashindano ya mara hii kwa mara ya kwanza yamezikaribisha timu za wakimbizi kutoka Kosovo na Sudan Kusini. Michezo 42 inaachezwa huku medali 306 zikishindaniwa katika michuano hiyo. Mbali na uwanja wa Maracana palipofanyika ufunguzi wa aina yake, michezo hiyo itapigwa katika viwanja 33 mjini Rio de Janairo na 5 katika miji ya Sao Paulo, Belo Horizonte, Salvador, Brasilia na Manaus. Mambo yalikuwa hivi katika siku ya ufunguzi wa mashindano hayo katika uwanja wa Maracana.
Hata hivyo, kuarifishwa kwa nguli mkongwe wa mbio za nyika kutoka Kenya Kipchoge Keino, mafanikio yake na namna alivyolea vipaji kuliteka fikra za wengi katika ufunguzi wa mashindano hayo.
Haya yanajiri huku Kenya ambayo imekuwa ikiaminika kuwa kitovu cha mabingwa wa mbio za marathon inakabiliwa na kizungumkuti. Hii ni baada ya meneja wa timu ya taifa ya riadha ya nchi hiyo inayoshiriki katika Michezo ya Olimpiki nchini Brazil, Michael Rotich, kuagizwa kurejea nyumbani baada ya kudaiwa kuitisha fedha ili kuwalinda wanariadha wa nchi hiyo wanaodaiwa kutumia pufya. Mwandishi wetu wa Kenya Seifullah Murtadha ana maelezo zaidi kutoka….
Muirani aibuka wa 6 Ulengaji Shabaha
Elaheh Ahmadi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amemaliza katika nafasi ya 6 katika mashindano ya Ulengaji Shabaha kwa bunduki katika kitengo cha wanawake kwenye mashindano ya Rio. Ahmadi alijikusanyia alama 122.5 katika mchezo wa kulenga shabaha kwa bunduki umbali wa mita 10 siku ya Jumamosi na kuibuka wa sita.
Amesema kama tunavyomnukuu: "Nilifanya bidii na mazoezi kwa muda wa miaka miwili ili nishinde medali yangu ya kwanza katika mashindano ya Olimpiki, lakini kutokana na ushindani mkubwa uliokuwepo, ndoto yangu haikutimia." Ginny Thrasher mwenye umri wa miaka 19 ndiye aliyeibuka kidedea na kuipa Marekani medali ya kwanza ya dhahabu baada ya kujizolea jumla ya pointi 208. Mchina Du Li alijinyakulia medali ya fedha baada ya kuibuka wa pili kwa alama 207 huku Mchina mwingine Yi Siling akitwaa medali ya shaba kwa kupata alama 185. Wakati huohuo, Wairani watatu waliokuwa wakililiwakilisha taifa hili katika mchezo wa tenisi ya mezani Nima Alamian, Noshad Alamyan na Neda Shahsavari wamebanduliwa nje ya mashindano hayo baada ya kushindwa kufurukuta mbele ya mahasimu wao.
Iran yatwaa Taji la Dunia katika soka huko Denmark
Kwengineko timu ya taifa ya soka ya wachezaji saba kila upande ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetwaa taji la mchezo huo kwa upande wa wanaume huko Denmark. Katika kipute cha Jumamosi, vijana wa Iran waliibamiza Scotland mabao 4-0 katika mchuano wa fainali wa mashindano hayo yanayaojulikana kama International Federation of CP Football (IFCPF) World Championships Qualification Tournament, uliopigwa katika uwanja wa Vejen Idrætscenter mjini Vejen nchini Denmark. Vijana wa Iran waliuanza mchezo kwa kasi nzuri ambapo kiungo Jasem Bakhshi aliipa timu hiyo ya Iran bao la kwanza kunako dakika ya 19.
Mehdi Jamali aliipa Iran bao la pili huku Bakhshi akiongeza la tatu katika dakika ya 58. Ehsan Masoumzadeh alipigilia msumari wa mwisho kwenye jeneza la vijana wa Kiskoti sekunde chache kabla ya kupigwa kipenga cha kumaliza mchezo.
Siku ya Jumamosi Iran ya Kiislamu iliichachawiza Ureno mabao 5-1 katika mchezo wa nusu fainali wa mashindano hayo ya dunia. Mashindano hayo ya kimataifa ya soka ya wachezaji saba kila upande yalianza Julai 29 na kufunga pazia lake Agosti 6. Wachezaji wa soka hii huwa watu wenye utindio wa ubongo CP na matatizo mengine ya ubongo.
Mchuano wa Ngao ya Jamii huku Pogba akisajiliwa Man U wiki ijayo
Tugeukie mchuano wa Ngao ya Jamii ambapo uwanja wa Wembley Jumapili ulishuhudia kivumbi baada ya Leicester City ambaye ni Bingwa wa Ligi Kuu ya Uingereza EPL na Manchester United ambaye ni bingwa wa Kombe la FA kutoana jasho na hatimaye Mashetani Wekundu kuibuka washindi wa mabao 2-1. Man U walikuwa wa kwanza kupata goli kunako dakika ya 31 kupitia kwa Jesse Lingard ila Leicester City walisawazisha goli hilo dakika ya 52 kupitia mshambuliaji wao aliyeng’ara msimu uliopita Jarmie Vardy.
Furaha ya Leicester City ilimalizwa na nguvu mpya Zlatan Ibrahimovic dakika ya 83 na kuipa Man U ubingwa wa Ngao ya Jamii/Hisani.
Huo ulikuwa mchezo wa kwanza wa mashindano kwa kocha Jose Mourinho aliyejiunga na Man United msimu huu sambamba na nyota Zlatan Ibrahimovic aliyetumia mechi hiyo kudhihirisha umbuji wake wa kucheka na nyavu.
Nikudokeze kuwa, sasa ni dhahiri shahiri kwamba klabu ya soka ya Man U inaelekea kumsajili kiungo mahiri Paul Pogba kutoka klabu ya Juventus ya Italia. Raia huyo wa Ufaransa mwenye umri wa miaka 23, anatarajiwa kufanyiwa vipimo vya afya wiki ijayo. Pogba anarejea katika klabu yake ya zamani baada ya kuondoka mwaka 2012. Ripoti zinasema kurejea kwake Old Trafford huenda kukawa ni usajili mkubwa sana kwa klabu hiyo msimu huu na hata kupita ule wa Gareth Bale mwaka 2013 alipouzwa kwa kima cha Pauni Milioni 85 katika klabu ya Real Madrid. Habari zinasema kuwa mchezaji huyo nguli wa soka yumkini akanunuliwa kwa Zaidi ya pauni milioni 100. Tukiachana na ya Man U na Pogba, kwengineko Arsenal iliitandika Manchester City mabao 3-2 katika mechi ya kirafiki siku ya Jumapili katika uwanja wa Göteborg. City ndio waliokuwa wa kwanza kucheka na nyavu za Gunners kupitia goli la kiungo Sergio Aguero katika dakika ya 30.
Dakika tano baada ya mapunziko, Wabeba Bunduki walisawazisha mambo na kuwa 1-1 kupitia bao la Alex Iwobi. Theo Walcott aliipa Gunners bao la pili katika dakika ya 73 kabla ya Chuba Akpom kuipa Arsenal la ushindi katika dakika ya 86.
Hata hivyo mambo hayakuishia hapo, dakika mbili baadaye, City walijikusanya na kupata bao la pili kupitia mchezaji Iheanacho, muda mfupi kabla ya mchuano kuisha.
………………………………TAMATI………………………….