Jul 24, 2025 02:46 UTC
  • Alkhamisi, tarehe 24 Julai, 2025

Leo ni Alkhamisi tarehe 28 Muharram 1447 Hijria inayosadifiana na tarehe 24 Julai 2025.

Siku kama ya leo miaka 791 iliyopita mji wa Baghdad uliokuwa makao makuu ya watawala wa Kiabbasi, ulitekwa na Hulagu Khan.

Hulagu alimuua mtawala Musta'sim na kukomesha kabisa utawala wa kizazi cha Bani Abbasi uliotawala maeneo mengi ya ulimwengu wa Kiislamu kwa kipindi cha miaka 500. Katika unyama huo mkubwa, Hulagu Khan alifanya ukatili mkubwa na kuua nusu ya watu wasiokuwa na hatia wa mji wa Baghdad. 

Hulagu Khan pia alichoma moto nyumba na majengo mengi ya kihistoria ikiwemo maktaba kubwa ya Baghdad na idadi kubwa ya vitabu vyenye thamani kubwa vya maktaba hiyo viliteketea au kutumbukizwa katika mto Tigris. ***

Hulagu Khan

Siku kama ya leo miaka 243 iliyopita Simón Bolívar mwanasiasa na mwanamapinduzi maarufu wa Amerika ya Kusini alizaliwa huko Caracas mji mkuu wa Venezuela.

Simon Bolivar alikomboa ardhi kubwa ya Amerika ya Kusini kutoka katika makucha ya ukoloni wa Kihispania. Vilevile alikuwa na mchango mkubwa katika mapinduzi ya Caracas na kufanikiwa kuiteka Bogota huko katikati mwa Colombia. Simon Bolivar aliteuliwa kuwa Rais na Congress iliyokuwa imeundwa kwa shabaha ya kuasisi Colombia Kubwa na alifanikiwa kuzikomboa ardhi za Colombia, Venezuela na Panama. Mwaka 1822, mapambano ya ukombozi yaliyokuwa yakiongozwa na Bolivar yalienea pia hadi Ecuador na nchi hiyo ikajiunga na Colombia Kubwa, baada ya kupata uhuru.  ***

Simon Bolivar

Miaka 223 iliyopita katika siku inayosadifiana na ya leo, alizaliwa mwandishi maarufu wa Kifaransa Alexandre Dumas.

Dumas aliandika riwaya nyingi kuhusiana na mapinduzi na historia ya Ufaransa kwa kustafidi na hadithi alizosimuliwa na baba yake ambaye alikuwa jenerali wa jeshi pamoja na kumbukumbu binafsi za wananchi kuhusu mapinduzi yalitokea nchini Ufaransa. ***

Alexandre Dumas.

Siku kama ya leo miaka 104 iliyopita Jumuiya ya Mataifa iliipatia mamlaka rasmi serikali ya Uingereza ya kuzidhibiti Palestina, Iraq na eneo la mashariki mwa Jordan, huku usimamizi wa Syria na Lebanon ukipewa serikali ya Ufaransa.

Hata hivyo Paris na London ziliafikiana katika Vita vya Kwanza vya Dunia na baada ya hapo juu ya kugawana utawala wa kifalme wa Othmania na uamuzi huo wa Jumuiya ya Mataifa ulihalalisha suala hilo. ***

Miaka 81 iliyopita katika siku kama ya leo, kikosi cha anga cha jeshi la Uingereza kiliishambulia vikali bandari muhimu ya Hamburg huko kaskazini mwa Ujerumani wakati wa Vita vya Pili vya Dunia.

Mashambulizi ya anga ya Ujerumani na Uingereza yalianza mwanzoni mwa Vita vya Pili vya Dunia na kushadidi zaidi baadaye. Kwa kadiri kwamba raia wengi wa nchi mbili hizo waliuawa katika mashambulizi hayo.

Makumi ya maelfu ya raia wa kawaida waliuawa kwa umati katika mashambulizi ya kikosi cha anga cha Uingereza dhidi ya bandari ya Hamburg mbali na kuangamizwa taasisi kadhaa za kijeshi na kiuchumi.   ***

Katika siku kama ya leo miaka 62 iliyopita, baada ya kutiwa mbaroni Imam Khomeini na vyombo vya usalama vya utawala wa Shah, maulamaa kadhaa na marajii kutoka Qum na Mash'had na miji mingine ya Iran walifunga safari na kuelekea Tehran.

Mbali na kuandika barua wakithibitisha daraja ya Umarjaa ya Imam Khomeini walitoa wito wa kuachiliwa huru mwanazuoni huyo. Hatua hiyo sambamba na kuendelea upinzani wa wananchi dhidi ya kutiwa mbaroni Imam Khomeini, kuliulazimisha utawala wa Shah kumhamisha kiongozi huyo kutoka jela na kumpeleka katika nyumba moja ili kuwatuliza maulama na wananchi hao. Siasa hizo za kutuliza mambo hazikuwa na taathira na kwa msingi huo utawala wa Shah, ukiwa na lengo la kuweka pengo baina ya Imam Khomeini na wafuasi wake, uliamua kumpeleka uhamishoni mwanazuoni huo nchini Uturuki na mwaka mmoja baadaye nchini Iraq.