Alkhamisi, 07 Agosti, 2025
Leo ni Alkhamisi 13 Mfunguo Tano Safar 1447 Hijria mwafaka na 7 Agosti 2025.
Siku kama ya leo miaka 1144 iliyopita alifariki dunia mtaalamu wa Hadithi wa Kiislamu, Abu Abdulrahman Ahmad bin Shuaib Nasai, maarufu kwa jina la Sheikhul Islam.
Nasai alizaliwa mwaka 220 Hijria katika mojawapo ya vijiji vya Khorasan huko kaskazini mwa Iran na akaelea nchini Misri akiwa kijana. Huko alipata elimu ya fiqhi na Hadithi na akaanza kufunza taaluma hizo. Baadaye Sheikhul Islam Nasai aliekele Damascus, Syria ambako alibainisha sifa na maadili ya Watu wa Nyumba ya Mtume Muhammad (amani ya Mwenyezi Mungu iwe juu yake na Aali zake) na kupigwa mara kadhaa na wapinzani wa Ahlul Bait. Hatimaye alielekea Hijaz na kuishi mjini Makka.
Nasai ameandika vitabu kadhaa kikiwemo kile cha "Khasaisu Amirul Muuminina Ali" na kile cha "Sunanun Nasai" ambacho ni miongoni mwa vitabu mashuhuri vya Hadithi vya Kiislamu.

Siku kama ya leo miaka 65 iliyopita sawa na Agosti 7 1960 nchi ya Ivory Coast ilifanikiwa kujipatia uhuru kutoka kwa mkoloni Mfaransa.
Wareno waliidhibiti nchi hiyo iliyoko magharibi mwa Afrika katika karne ya 16, lakini ulipofika mwaka 1891 Ufaransa iliidhibiti nchi hiyo, licha ya upinzani mkubwa wa wananchi wa Ivory Coast.
Hatimaye ulipofika mwaka 1960, Ivory Coast ikiwa pamoja na nchi nyingine kadhaa za Kiafrika zilizokoloniwa na Mfaransa zilijipatia uhuru wao.

Siku kama ya leo miaka 43 iliyopita mwafaka na tarehe 7 Agosti 1982, yalitiwa saini makubalino ya kuondoka vikosi vya Harakati ya Ukombozi ya Palestina (PLO) mjini Beirut Lebanon kati ya Marekani, Lebanon na PLO.
Makubaliano hayo yalitiwa saini kufuatia shambulio kubwa lililofanywa na jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel nchini Lebanon mwezi Juni 1982 kwa shabaha ya kuwafukuza wapiganaji wa PLO nchini Lebanon.
Ijapokuwa kuondoka wanamgambo wa PLO nchini Lebanon kulitoa pigo kubwa kwa harakati hiyo, lakini miaka ya baadaye Wazayuni maghasibu walikabiliwa na kipigo kikali kutoka kwa wanamapambano wa harakati ya muqawama ya Lebanon, Hizbullah, na kulazimika kuondoka kwa madhila katika ardhi ya nchi hiyo mwaka 2000.

Siku kama ya leo miaka 17 iliyopita vikosi vya jeshi la Georgia vikisaidiwa na serikali ya Marekani vililishambulia eneo linalopigania kujitenga la Ossetia ya Kusini huko kaskazini mwa nchi hiyo.
Mamia ya raia wasio na hatia wala ulinzi waliuawa na kujeruhiwa kwenye mashambulio hayo. Siku moja baadaye, wanajeshi wa Russia waliingilia kati na kuamua kuwaunga mkono wapiganaji wanaopigania kujitenga wa Ossetia ya Kusini na kulilazimisha jeshi la Georgia kurudi nyuma. Vikosi vya jeshi la Russia vilifanikiwa kuiteka bandari muhimu ya Patumi na kusonga mbele karibu na Tiblis mji mkuu wa nchi hiyo.
Jeshi la Russia liliondoka huko Georgia Agosti 12 kwa upatanishi wa Rais wa Ufaransa, na Moscow ikayatambua rasmi kuwa huru maeneo mawili yaliyokuwa yakipigania kujitenga yaani Ossetia ya Kusini na Abkhazia. ****
Katika siku kama ya leo miaka 84 iliyopita, Rabindranat Tagore, mwandishi, mshairi na mwanafalsafa wa India aliaga dunia.
Alizaliwa mwaka wa 1861 huko Calcutta (Kolkata) mashariki mwa India. Tagore sambamba na kuwa mwanaharakati amilifu katika harakati ya kitaifa ya India ya kupigania uhuru kutoka kwa Uingereza, pia alikuwa akiandika mashairi na nathari.
Mshairi huyu wa Kihindi alichanganya maelezo maridadi ya asili na mawazo ya kidini na kifalsafa katika mashairi na nathari zake. Mnamo 1913, Rabindranat Tagore alitunukiwa Tuzo ya Nobel ya Fasihi.
