Aug 22, 2025 02:34 UTC
  • Ijumaa, Agosti 22, 2025

Leo Ijumaa tarehe 28 Safar mwaka 1447 Hijria, sawa na Agosti 22 mwaka 2025.

Siku kama ya leo miaka 1436 iliyopita inayosadifiana na tarehe 28 Safar mwaka 11 Hijria, alifariki dunia Mtume Mtukufu Muhammad (saw) akiwa na umri wa miaka 63.

Kutokana na kuwa na tabia ya ukweli na uaminifu tangu alipokuwa na umri mdogo, Mtume Mtukufu (saw) alipata umashuhuri kwa jina la "Muhammad Mwaminifu".

Akiwa na umri wa miaka 40 Mwenyezi Mungu SW alimteua kuwa Mtume Wake ili aweze kuwalingania watu ibada ya Mungu Mmoja na kuondoa ukabila, dhulma na ujinga. Watu wa dini, madhehebu na mirengo tofauti na hata wale wasiokuwa na dini kabisa wamesema mengi kuhusu shakhsia adhimu ya Nabii Muhammad (saw).

Mwandishi wa Ulaya, Stanley Lane Poole ameandika kwamba, Mtume Muhammad alipendwa na watu wote na kila aliyemuona, na kwamba hajawahi kuona wala hatamuona tena mtu mithili yake.

Siku kama ya leo miaka 1397 iliyopita, yaani sawa na tarehe 28 Safar mwaka 50 Hijiria, aliuawa shahidi Imam Hassan bin Ali bin Abi Twalib al Mujtaba (as), mjukuu wa Mtume Mtukufu (saw).

Imam Hassan (as) ni mtoto wa Bibi Fatima al Zahra na Imam Ali bin Abi Talib (as), na alizaliwa mwaka wa 3 baada ya Mtume (saw) kuhamia mjini Madina. Mtukufu huyo aliishi miaka saba ya mwanzo wa umri wake pamoja na babu yake Mtume Muhammad (saw) ambapo aliweza kunufaika na mafunzo na maarifa ya dini Tukufu ya Kiislamu. Imam Hassan alichukua jukumu zito la kuongoza Umma wa Kiislamu akiwa na umri wa miaka 37 baada ya kuuawa shahidi baba yake, Imam Ali (as).

Baada ya kufariki dunia Imam Ali (as) Waislamu walimpa baia Imam Hassan kwa ajili ya kuwaongoza, ambapo hata hivyo baada tu ya kuteuliwa kwenye nafasi hiyo alikabiliwa na njama pamoja na ukwamishaji mambo wa Muawiyah bin Abi Sufiyan. Hatimaye Imam Hassan aliandaa jeshi aliloachiwa na baba yake kwa ajili ya kumkabili Muawiya, ingawa muovu huyo (Muawiya) alitumia hila za kila namna kuwanunua wafuasi wa Imam Hassan ambao hatimaye walimkimbia na kumwacha peke yake mjukuu huyo wa Mtume wa Allah.

Imam Hassan aliuawa shahidi siku kama ya leo kwa kupewa sumu katika njama iliyopangwa na Muawiya bin Abi Sufyan. 

Katika siku kama ya leo miaka 398 iliyopita vilijiri vita vya mwisho vya La Rochelle kati ya Wakatoliki na Waprotestanti wa Ufaransa.

Vita hivyo vilianza baada ya Waprotestanti kuchochewa na Uingereza. Wakatoliki ambao walikuwa wakiungwa mkono na vikosi vya jeshi la serikali ya Ufaransa chini ya uongozi wa Richelieu, Kansela mashuhuri wa nchi hiyo, walipigana vita na Waprotestanti ambao walikuwa wakipigania maeneo yao katika bandari ya La Rochelle.   

Vita hivyo vilimalizika baada ya mwaka mmoja kwa kupata ushindi Wakatoliki na kutekwa La Rochelle.

Miaka 327 iliyopita katika siku kama ya leo, mkataba wa pande tatu wa Russia, Poland na Denmark ulitiwa saini dhidi ya Sweden.

Wafalme wa nchi hizo tatu walikuwa na lengo la kumuangusha Karl XII mfalme kijana wa Sweden ili kuikalia kwa mabavu nchi hiyo. Ni kwa msingi huo ndipo miaka miwili baadaye mnamo mwezi Aprili mwaka 1700 nchi wanachama wa mkataba huo wa pande tatu zikaamua kuishambulia Sweden, hata hivyo jeshi la mfalme Karl XII likakabiliana vilivyo na kutoa pigo kwa nchi vamizi.

Baada ya kufikia mapatano na Denmark, mwaka 1704 akaishambulia Poland na kuikalia kwa mabau. Hata hivyo mashambulio ya Sharel dhidi ya Russia hayakuzaa matunda.   

Siku kama ya leo miaka 165 iliyopita Paul Gottlieb Nipkow mmoja wa wavumbuzi wa televisheni alizaliwa huko Ujerumani.

Nipkow alikulia katika familia maskini, lakini juhudi na irada kubwa ilimuwezesha kuendeleza masomo yake ya fizikia hadi chuo kikuu. Paul Gottlieb Nipkow alifanya utafiti mkubwa na hatimaye alifanikiwa kuvumbua transimita ya televisheni.

Chombo hicho kilichobuniwa na Nipkow kiliweza kurusha mawimbi ya televisheni katika umbali wa mita 30 na baadaye transimita iliyotengenezwa na mvumbuzi huyo wa Kijerumani ilikamilishwa na wabunifu wengine. 

Na miaka 161 iliyopita katika siku kama hiii ya leo, mkataba wa kihistoria wa Geneva ulitiwa saini baina ya nchi kadhaa za Ulaya, Asia na Amerika.

Lengo la mkataba huo lilikuwa ni kuwasaidia majeruhi katika medani za vita.  Kwa mujibu wa mkataba huo, timu za madaktari, watoaji misaada na zana zao zinapaswa kutoegemea upande wowote na zisishambuliwe bali zibakie katika amani wakati wa vita. Mbunifu wa mkataba huo alikuwa Henry Dunant raia wa Uswisi.