Jumamosi, 23 Agosti, 2025
Leo ni Jumamosi 29 Mfunguo Tano Safar 1447 Hijria mwafaka na 23 Agosti 2025 Miladia.
Tarehe Mosi Shahrivar katika kalenda ya mwaka wa Hijria Shamsia ni siku ya kumuenzi Hassan bin Abdullah maarufu kwa jina la Abu Ali Sina na siku ya daktari. Abu Ali Sina alizaliwa tarehe 3 Safar mwaka 370 Hijria katika eneo la Balkh na kujifunza elimu za zama hizo akiwa bado kijana hadi alipopata umashuhuri mkubwa katika taaluma mbalimbali na kutambuliwa kuwa gwiji wa zama hizo. Alikuwa miongoni mwa wanafalsafa, maurafa na matabibu wakubwa. Ibn Sina alihifadhi Qur'ani yote alipokuwa na umri wa miaka 10. Alijifunza utabibu baada ya kupata elimu za mantiki, hisabati, nujumu, falsafa pamoja na elimu nyinginezo. Alianza kuandika vitabu akiwa na umri wa miaka 21 na miongoni mwa vitabu vyake maarufu ni Qanun, Shifaa na Isharaat.
Tarehe 29 Safar miaka 1130 iliyopita aliaga dunia Abu Abdullah Muhammad bin Jabir bin Sinan ambaye alikuwa mwanahesabati mkubwa na mashuhuri wa Kiislamu. Muhammad bin Sinan alikuwa miongoni mwa wanafalsafa, wanajimu na wataalamu wakubwa na gwiji wa nyota wa Kiislamu. Hakuwa na mfano katika elimu ya hisabati katika zama hizo. Msomi huyo wa Kiislamu alizaliwa nchini Misri na alitumia muda wa miaka 40 kufuatilia sayari na nyota. Abu Abdullah bin Sinan alifanikiwa kuainisha wakati halisi wa mwaka wa jua na ameandika vitabu kadhaa kama vile Taadilul Kawakib na Miqdarul Ittisalat.
Siku kama ya leo, miaka 81 iliyopia mji wa Paris ulikombolewa kutoka kwenye uvamizi wa Ujerumani. Miezi 15 baada ya kushtadi moto wa Vita vya Pili vya Dunia na katika kuendeleza njama zake za kutaka kujitanua, dikteta Adolph Hitler aliyaamuru majeshi ya nchi hiyo kuushambulia mji wa Paris kwa lengo la kutaka kuudhibiti mji huo. Tarehe tano Juni mwaka 1940, Hitler alitoa amri ya kuharibiwa kikamilifu muundo wa majeshi ya Ufaransa na siku tatu baadaye yaani tarehe nane Juni mwaka 1940, vikosi vya Wanazi vilikishinda kikosi cha ulinzi cha Ufaransa katika eneo la kaskazini mashariki mwa taifa hilo, na hivyo kutoa mwanya kwa jeshi la Ujerumani kuingia nchini Ufaransa.

Siku kama ya leo miaka 22 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 23 Agosti 2003, alifariki dunia Michael Kijana Wamalwa, Makamu wa Rais wa Kenya. Wamalwa alizaliwa 25 Novemba 1944 katika kijiji cha Sosio karibu na Kimilili, wilayani Bungoma. Michael Kijana Wamalwa alikuwa mtoto wa mwanasiasa na mbunge machachari William Wamalwa. Mwaka 2002, Wamalwa akiwa pamoja na wanasiasa wengine mashuhuri nchini Kenya, wakiongozwa na Mwai Kibaki wa chama cha National Rainbow Coalition NARC, walifanikiwa kuung'oa madarakani utawala wa chama cha KANU uliotawala nchi hiyo kwa zaidi ya miongo minne. Kijana Wamalwa alizikwa kwenye shamba lake lililoko Kitale.
