Jumapili, 14 Septemba, 2025
Leo ni Jumapili 21 Mfunguo Sita Rabiul-Awwal 1447 Hijria mwafaka na 14 Septemba 2025 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 636 iliyopita, utawala wa Othmania uliidhibiti na kuikalia kwa mabavu ardhi ya Serbia. Tukio hilo lilijiri wakati wa operesheni za utawala huo za kuzitia katika miliki yake ardhi za Ulaya. Ushindi huo ulipatikana katika kipindi cha ufalme wa Sultan Murad wa Kwanza Mfalme III wa utawala huo. Licha ya kuweko uasi wa wananchi wa Serbia, lakini ardhi yao iliendelea kuwa chini ya udhibiti wa Ufalme huo kwa karibu karne tano.

Katika siku kama ya leo miaka 213 iliyopita, moja kati ya ajali kubwa za moto ulimwenguni ilitokea katika mji mkuu wa Russia Moscow. Moto huo uliwashwa kwa makusudi. Ilikuwa imepita siku moja tu, tangu mji huo uvamiwe na kukaliwa kwa mabavu na majeshi ya Napoleone Bonaparte, wakati mji huo ulipochomwa moto kwa amri ya mtawala wa wakati huo wa mji huo. Lengo la mtawala huyo lilikuwa kuyafanya majeshi ya Bonaparte yashindwe kutumia suhula za mji huo. Moto huo mkubwa uliteketeza na kuharibu kabisa robo tatu ya mji wa Moscow.

Katika siku kama ya leo miaka 204 mji wa Iravan ulidhibitiwa na vikosi vya Russia wakati wa kujiri vita vya pili kati ya Iran na Russia. Mji huu uliangukia mikononi mwa Warusi katika zama za utawala wa Fat'h Ali Shah Qajar na kukabidhiwa kwa Russia. Natija ya kushindwa huko kukawa ni kusainiwa mkataba wa Turkmenchay ambao kwa mujibu wake sehemu kubwa ya ardhi ya kaskazini mwa Azerbaijan na Caucasia ilitenganishwa na ardhi ya Iran na kuunganishwa na Russia.

Siku kama ya leo miaka 65 iliyopita, hati ya Jumuiya ya Nchi Zinazozalisha Mafuta kwa Wingi Duniani (OPEC) ilitiwa saini na nchi za Iran, Saudia, Iraq, Kuwait na Venezuela. Jumuiya hiyo ilianzishwa kwa lengo la kukabiliana na makampuni makubwa ya mafuta ya Magharibi ambayo yalikuwa yakisimamia uvumbuzi, uchimbaji na uuzaji wa bidhaa hiyo kimataifa na kuainisha bei ya bidhaa hiyo muhimu kwa maslahi yao binafsi na kwa madhara ya nchi zalishaji. Licha ya kwamba awali jumuiya hiyo haikuwa na nguvu wala ushawishi wowote, lakini ilikuja kupata nguvu zaidi baada ya nchi kadhaa zikiwemo, Algeria, Libya, Nigeria, Qatar, Imarat, Gabon, Indonesia na Ecuador ambazo ni wazalisha wa mafuta kujiunga nayo.
