Sep 15, 2025 04:02 UTC
  • Jumatatu, 15 Septemba, 2025

Leo ni Jumatatu 22 Mfunguo Sita Rabiul Awwal 1447 Hijria sawa na 15 Septemba 2025.

Siku kama ya leo miaka 1443 iliyopita, yaani tarehe 22 Rabiul-Awwal mwaka wa 4 Hijiria, kulianza vita kati ya Waislamu na Mayahudi wa kabila la Bani Nadhir baada ya watu wa kabila hilo kufanya njama za kutaka kumuua Mtume Muhammad (saw).

Bani Nadhir ni moja ya makundi matatu ya Mayahudi waliokuwa wakiishi katika vitongoji vya mji wa Madina, ambao kwa mujibu wa mkataba waliotiliana saini na Mtume (SAW), hawakutakiwa kuchukua hatua yoyote iliyo dhidi ya mtukufu huyo na Waislamu kwa ujumla.

Baada ya Mayahudi kuvunja mkataba huo, Mtume Muhammad (SAW) aliwaamuru waondoke Madina. Hata hivyo Mayahudi hao ambao tayari walikuwa wamepewa ahadi za kuungwa mkono na wanafiki wa mji huo, hawakuwa tayari kutii amri hiyo. Ni kwa sababu hiyo, ndipo mtukufu Mtume kwa kushirikiana na Waislamu akazizingira ngome za watu hao kwa muda wa siku kadhaa na kuwalazimisha kuondoka katika maeneo yao. 

Mabaki ya Ngome ya Bani Nadhir

Miaka 204 iliyopita yaani tarehe 15 Septemba 1821, nchi za Nicaragua, Honduras, el-Salvador, Guatemala na Costa Rica zilijitangazia uhuru kutoka kwa Uhispania.

Baada ya Napoleone Bonaparte mtawala wa Kifaransa kuikalia kwa mabavu Uhispania na kudhoofika serikali ya kijeshi ya Madrid, nchi kadhaa za Latin America zikiwemo Nicaragua, Honduras, el-Salvador, Guatemala na Costa Rica zilijitangazia uhuru. Baada ya nchi hizo tano kujitangazia uhuru ziliunda Muungano wa Amerika ya Kati.

Baada ya muungano huo kuvunjika mwaka 1838, nchi wanachama kila moja ilianza kujitawala na kujiendeshea mambo yake yenyewe.   

Siku kama ya leo miaka 67 iliyopita, kwa mara ya kwanza katika historia ya elimu ya tiba, virusi vinavyosababisha ugonjwa hatari wa trakoma au mtoto wa jicho viligunduliwa. Kugunduliwa virusi hivyo kulienda sambamba na njia za kupambana na ugonjwa huo wa mtoto wa jicho, ambapo maelfu ya watu walikuwa wakipofuka katika pembe mbalimbali duniani kutokana na maradhi hayo. Virusi vya trakoma viligunduliwa na matabibu wawili wa Kiingereza.

Na siku kama hii ya leo miaka 26 iliyopita sawa na tarehe 24 mwezi Shahrivar mwaka 1378 Hijria shamsiya, alifariki dunia kwa maradhi ya moyo Dakta Abdulhussein Zarinkub mwanahistoria na mtafiti mashuhuri wa Kiirani. Dakta Abdulhussein alizaliwa mwaka 1301 Hijria Shamsiya katika mji wa Burujerd magharibi mwa Iran. Mwaka 1327 Hijria Shamsiya Dakta Zarinkub alitunukiwa shahada ya digrii katika taaluma ya historia na baadae akaendelea na masomo yake katika taaluma hiyo na kutunikiwa shahada ya udaktari. Mbali na historia msomi huyo wa Kiirani alipenda sana masomo ya fasihi ya lugha ya Kifarsi na irfani ya Kiislamu. Aidha aliandika vitabu na makala nyingi na moja kati ya vitabu vyake ni kile alichokiita "Alfajiri ya Uislamu."