Aug 12, 2016 06:33 UTC
  • Ijumaa tarehe 12 Agosti 2016

Leo ni ijumaa tarehe 10 Dhulqaada 1437 Hijria sawa na 12 Agosti 2016.

Miaka 17 iliyopita, Umoja wa Mataifa uliitangaza Agasti 12 kila mwaka, kuwa ‘Siku ya Vijana Duniani’ ili kueleza umuhimu wa vijana katika dunia ya sasa. Tabaka hili lenye utanashati la jamii ndiyo sababu ya maendeleo ya kila nchi kwa msingi huo vijana katika kila nchi wanapaswa kupewa umuhimu mkubwa. Kutokana na umuhimu wao vijana wanapaswa kulindwa na kusaidiwa na serikali hususan katika masuala ya ajira, makazi na kujenga familia. Katika upande mwingine kizazi cha leo cha vijana kinakabiliwa na changamoto nyingi za kimwili na kiroho ikiwa ni pamoja na ongezeko la matumizi ya dawa za kulevya, magonjwa ya kuambukiza kama Ukimwi na virusi vya HIV, intaneti na michezo ya computa ambayo inawatumbukzia vijana wengi katika ufuska na utovu wa maadili. Kutangazwa Siku ya Vijana Duniani kunaweza kusaidia juhudi za kuwakumbusha vijana umuhimu wao na kuzuia changamoto mbalimbali zinazolikabili tabaka hilo muhimu.  

Tarehe 12 Agosti mwaka 1949 hati ya makubaliano ya kimataifa ya kuwalinda majeruhi na mateka wa kivita ilipasishwa kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa huko Geneva, Uswisi. Hati hiyo ilibuniwa kufuatia miamala isiyo ya kibinadamu na jinai zilizokuwa zikifanywa dhidi ya majeruhi na mateka wa kivita wakati wa Vita vya Pili vya Dunia. Kwa mujibu wa makubaliano hayo, nchi zenye mateka zilitakiwa kuwasilisha orodha ya majina ya mateka kwa Shirika la Msalaba Mwekundu Duniani. Hata hivyo licha kuweko makubaliano hayo, lakini madola mengi duniani yamekuwa yakipuuza na kutojali haki za mateka na majeruhi wa kivita.

Siku kama hii ya leo miaka 40 iliyopita sawa na tarehe 12 Agosti 1976, kambi ya wakimbizi wa Palestina ya Tel al Zaatar iliyoko karibu na Beirut mji mkuu wa Lebanon, ilitekwa baada ya kuzingirwa kwa muda mrefu na wanamgambo wa Kimaroni wa nchi hiyo na wakazi wake wakauawa kwa umati. Kambi hiyo ilikuwa ikiwahifadhi maelfu ya wakimbizi wa Palestina na ilianza kuzingirwa mwanzoni mwa mwaka 1976 kwa uungaji mkono na uingiliaji wa utawala wa Kizayuni wa Israel. Utawala wa Kizayuni ulifanya hivyo kwa lengo la kushadidisha vita vya ndani huko Lebanon.