Oct 14, 2026 02:49 UTC
  • Jumatano, Oktoba 14, 2026

Leo ni Jumatano mwezi Tatu Mfunguo Nane Jamadul-Awwal 1448 Hijria ambayo inasadifiana na 14 Oktoba 2026 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 212 iliyopita, yaani Oktoba 14, 1814, mkutano wa kihistoria wa Vienna ulifanyika kwa lengo la kujadili “Ulaya ya baada ya Napoleon Bonaparte”.  Baada ya kujiuzulu na kubaidishwa Bonaparte mwezi Aprili mwaka 1814, mkutano wa kihistoria wa Vienna ulianza kufanyika katika siku kama ya leo katika mji mkuu huo wa Austria ili kuchukua maamuzi kuhusu ardhi zilizokaliwa kwa mabavu na Ufaransa katika kipindi cha vita vya Bonaparte. Wakati wa kuendelea mkutano huo, Napoleone Bonaparte alikimbia kutoka mahala alipokuwa amebaidishiwa; na mwishoni mwa mwezi Februari mwaka 1815 kwa mara nyingine tena akashika hatamu za uongozi kwa muda mfupi, kipindi ambacho kiliondokea kuwa mashuhuri kwa jina la “Utawala wa Siku 100”. Aliposhika tena hatamu za uongozi alijianda kuwashambulia maadui zake.

***

Katika siku kama ya leo miaka 156 iliyopita sawa na tarehe 3 Mfunguo Nane Jamadul-Awwal 1292 Hijria, alifariki dunia Ayatullah Mirza Abu Abdillah Sheikhul-Islam Zanjani, alimu na malenga aliyekuwa na uwezo mkubwa wa Waislamu.  Alizaliwa mwaka 1224 Hijiria mjini Zanjan, moja ya miji ya Iran na akiwa kijana alielekea mjini Isfahan kwa ajili ya masomo. Akiwa mjini Isfahan alijiunga na chuo cha hauza ambacho kilikuwa moja ya vituo vyenye itibari katika elimu ya kidini wakati huo ambapo alifikia elimu ya juu na kisha kurejea nyumbani baada ya kuhitimu masomo yake.  Sambamba na kujishughulisha na kazi ya ufundishaji Ayatullah Mirza Abu Abdillah Sheikhul-Islam Zanjani, aliandika vitabu vingi ambavyo baadhi yake ni 'Hujjatul-Abraar' na 'Hidayatul-Muttaqin'.

***

Miaka 111 iliyopita katika siku kama ya leo kwa mujibu wa kalenda ya Hijria, alifariki dunia Ayatullah Sayyid Ismail Swadr, alimu na mujtahidi wa ngazi ya juu mjini Kadhimiya, Iraq.  Alisoma masomo ya awali ya dini ya Kiislamu kwa kaka yake na kisha akaelekea mjini Najaf, Iraq kwa ajili ya kujiendeleza zaidi katika uwanja huo. Akiwa mjini Najaf alijifunza elimu ya sheria za Kiislamu (fiqhi), elimu ya akhlaq na elimu nyingine tofauti za kidini.  Baada ya kufariki dunia mwalimu wake mkubwa Ayatullah Mirza Shirazi, Ayatullah Sayyid Ismail Swadr alichukua jukumu la ufundishaji mjini Karbala, Iraq.

***

Katika siku kama ya leo miaka 93 iliyopita, yaani tarehe 14 Oktoba, 1933, kwa amri ya Kansela wa wakati huo wa Ujerumani Adolf Hitler, nchi hiyo ilijitoa katika Shirikisho la Mataifa (The League of Nations). Kuingia madarakani Hitler akiwa Kansela wa Ujerumani kulizusha wasiwasi mkubwa katika kila kona ya Ulaya kutokana na mipango yake ya kijeshi. Baada ya kumalizika Vita vya Kwanza vya Dunia na kutiwa saini mkataba wa amani wa Warsaw ambao ulidhibiti sana zana za kijeshi za Ujerumani, Hitler na viongozi wengine wa Kinazi walikasirishwa mno na hatua hiyo.

***

Siku kama ya leo miaka 73 iliyopita, Wazayuni wa Israel walivamia kijiji cha Qibya kilichoko katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na kufanya jinai kubwa za kutisha. Katika mashambulizi na uvamizi huo ulioendelea katika kijiji hicho kwa muda wa siku mbili, Wazayuni walitekeleza mauaji na ukatili mkubwa dhidi ya raia wa Kipalestina wasio na hatia. Mbali na Wazayuni hao kuwaua na kuwajeruhi kwa umati raia wa Kipalestina zaidi ya 42, askari wa Israel waliokuwa wakiongozwa na Waziri Mkuu wa zamani wa Israel, Ariel Sharon, walibomoa makumi ya nyumba na shule za kijiji hicho. Mauaji hayo ya halaiki ni miongoni mwa mifano ya ugaidi wa utawala ghasibu wa Israel hususan wa Waziri Mkuu wa zamani wa utawala huo, Ariel Sharon.

Katika siku kama ya leo miaka 27 iliyopita alifariki dunia kiongozi wa zamani wa Tanzania, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Nyerere ambaye anajulikana kuwa baba wa taifa wa Tanzania, alizaliwa tarehe 13 Aprili 1922 katika kijiji cha Butiama mkoani Mara. Aliingia katika ulingo wa siasa 1955 akiongoza chama cha (Tanganyika African Nation Union) TANU. Mwaka 1961 Nyerere akawa Waziri Mkuu wa Tanganyika na mwaka mmoja baadaye akawa rais wa Tanganyika. Kutokana na juhudi zake mwaka 1964 Tanganyika na Zanzibar ziliungana na kuunda nchi moja ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Nyerere aliendelea kuongoza Jamhuuri ya Muuungano wa Tanzania hadi mwaka 1985 ambapo aliachia hatamu za uongozi. Pamoja na hatua yake hiyo Nyerere aliendelea kuwa na ushawishi mkubwa katika siasa za Tanzania hadi alipofariki dunia katika siku kama ya leo. 

***

Na miaka 3 iliyopita katika siku kama ya leo kwa mujibu wa kalenda ya Hijria Shamsia, Dariush Mehrjui, mmoja wa waongozaji, waandishi wa miswada ya filamu na watayarishaji maarufu wa filamu nchini Iran, alifariki dunia. Alizaliwa tarehe 17 Azar 1318 Hijria ya Shamsia, mjini Tehran. Akiwa na umri wa miaka 20, alihamia California nchini Marekani kwa ajili ya kuendelea na masomo. Mwaka 1344 Hijria ya Shamsia, alipata shahada ya kwanza katika lugha ya Kifaransa kutoka Chuo Kikuu cha UCLA, na mwaka huo huo alipewa jukumu la kuwa mhariri mkuu wa jarida la Pars mjini Los Angeles. Baada ya mwaka mmoja alirejea Iran. Kutokana na kuvutiwa kwake na taaluma ya sinema, aliamua kuanza shughuli zake za kisanii kama mwongozaji wa filamu. Mehrjui anatambuliwa kuwa miongoni mwa watu muhimu walioasisi wimbi jipya la sinema ya Iran. Katika zaidi ya miongo mitano ya shughuli zake za kisanii, aliongoza zaidi ya filamu 20, zikiwemo filamu maarufu kama “Gav” (Ng’ombe), “Hamoun”, “Ejareh-Neshinha”, “Mehmanie Maman” na “Santouri.” Dariush Mehrjui aliwahi mara kadhaa kutajwa miongoni mwa waongozaji bora zaidi katika historia ya sinema ya Iran, na alishinda tuzo nyingi kutoka katika tamasha mbalimbali za kimataifa. Dariush Mehrjui pamoja na mke wake waliuawa usiku wa tarehe 22 Mehr 1402 Hijria ya Shamsia, sawa na Oktoba 14, 2023, katika nyumba yao ya kifahari iliyoko Karaj, karibu na Tehran.

***