Oct 13, 2026 03:32 UTC
  • Leo Katika Historia
    Leo Katika Historia

Leo ni Jumanne mwezi Pili Mfunguo Nane Jamadul-Awwal 1448 Hijria ambayo inasadifiana na 13 Oktoba 2026 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 2565 iliyopita mji wa kihistoria wa Babel ulitekwa na Kurosh, mwasisi wa utawala wa kizazi cha Hakhamaneshi nchini Iran. Ili kuweza kuudhibiti mji huo ambao ulikuwa na ngome kubwa na imara, Kurosh aliamuru kubadilishwa mkondo wa Mto Tigris uliokuwa ukipita katikati ya mji wa Babel. Kwa utaratibu huo askari wa Kurosh walitumia njia ya zamani ya maji ya mto huo kuingia na kisha kuuteka mji wa Babel. Mji huo ulioko kusini mwa eneo la Mesopotamia katika Iraq ya sasa, ulikuwa katika kilele cha maendeleo na nguvu kubwa katika kipindi hicho.

***

Miaka 1057 iliyopita katika siku kama ya kwa mujibu wa kalenda ya Hijria, alifariki dunia malenga wa Kiirani, Abu Is'haq Kesa-i Marvazi. Kipindi cha ujana wake kiliambatana na kumalizika kwa kipindi cha utawala wa Wasamani na mwanzoni mwa zama za utawala wa Waghaznavi. Kwa sababu hiyo malenga huyu Mfarsi alitunga mashairi kadhaa kuhusu tawala hizo mbili. Fauka ya hayo Marvazi alitunga beti kadhaa za mashairi ya kumsifu Mtume Muhammad na (SAW) na kizazi chake, hasahasa Imam Ali bin Abi Twalib (as). Kesa-i Marvazi mbali na kusifika kwa utunzi wa mashairi, lakini pia alitoa waadhi na hikma kupitia mashairi yake ya Kifarsi. Malenga huyu mkubwa wa Kiirani ameacha diwani ya mashairi.

***

Katika siku kama ya leo miaka 100 iliyopita yaani tarehe 21 Mehr 1305 Hijria Shamsia mshairi mashuhuri wa Iran, Profesa Muhammad Taqi Shurideh Shirazi, alifariki dunia. Muhammad Taqi Shurideh Shirazi, mwana wa Abbas, alizaliwa mwaka 1236 Hijria Shamsia katika mji wa Shiraz. Akiwa na umri wa miaka saba, alipoteza uwezo wa kuona kutokana na ugonjwa wa ndui. Hata hivyo, kwa kuwa alikuwa na kipaji kikubwa cha akili na kipawa cha ushairi, ndani ya muda mfupi alipata umaarufu mkubwa kupitia mashairi yake, ambayo yalisambaa na kujulikana sana miongoni mwa watu. Baadaye, Muhammad Taqi alielekea Tehran. Hatimaye, mshairi huyo wa Shiraz alifariki akiwa na umri wa miaka 69, na akazikwa karibu na kaburi la mshairi mashuhuri Saadi Shirazi.

***

Miaka 79 iliyopita, katika siku kama ya leo ya tarehe Pili Jamadul-Awwal, mwaka 1369 Hijria Mwanazuoni mcha-Mungu, Sheikh Ali Akbar Nahavandi, alifariki dunia. Ali Akbar bin Mulla Muhammad Hussein Nahavandi, ambaye asili yake ilikuwa kutoka Nahavand, alizaliwa katika mji wa Mashhad. Alisoma mjini Tehran chini ya Sheikh Haj Mirza Hassan Ashtiani, na baadaye akaelekea Najaf, Iraq, ambako alisoma chini ya wanazuoni mashuhuri, akiwemo Haj Mirza Habibullah Rashti na Shariat Isfahani. Mwaka 1328 Hijria, Nahavandi alielekea katika mji mtakatifu wa Mashhad, ambako aliamua kuishi na kuendelea na shughuli zake za kielimu na kidini. Miongoni mwa vitabu na athari alizoacha ni Al-Bayan al-Rafi' fi Ahwal Khwaja Rabi', Gulzar-e Akbari, na Lalehzar. Hatimaye, mwanazuoni huyo mcha-Mungu alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 90, na akazikwa katika mji mtakatifu wa Mashhad.

***

Katika siku kama hii ya leo miaka 62 iliyopita bunge la kimaonyesho la Iran lilipasisha sheria iliyowapa washauri wa kijeshi wa Marekani nchini kinga ya kutofikishwa mahakamani iwapo wangepatikana na hatia ya aina yoyote (Capitulation Accord). Kwa mujibu wa sheria hiyo, wahalifu wa Kimarekani wangehukumiwa nchini kwao kama watatenda jinai nchini Iran, na mahakama za Iran hazikuwa na haki ya kushughulikia kesi zao. Sheria hiyo ilitambuliwa kuwa dharau kwa taifa la Iran na iliyokiuka wazi kujitawala kwa nchi. Kwa msingi huo hayati Imam Ruhullah Khomeini (MA) siku kadhaa baada ya kupasishwa sheria hiyo bungeni alitoa hotuba ya kihistoria akieleza taathira zake na kumshambulia vikali Mfalme Shah na Marekani. Baada ya hotuba hiyo Imam Khomeini alikamatwa na kupelekwa uhamishoni. ***