Oct 15, 2026 07:18 UTC
  • Alkhamisi, Oktoba 15, 2026

Leo ni Alkhamisi mwezi 4 Mfunguo Nane, Jumada al-Ula 1448 Hijria, sawa na tarehe 15 Oktoba, 2026 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 44 iliyopita yaani tarehe 23 Mehr 1361 kulingana na kalenda ya Hijria shamsia, Ayatullah "Ata'ullah Ashrafi Isfahani", mwakilishi wa Imam Khomeini (MA) na Imamu wa Sala ya Ijumaa katika mji wa Kermanshah magharibi mwa Iran, aliuawa shahidi kwenye mihrabu ya Msikiti na maajenti wa genge la kigaidi la Wanafiki, MKO. Wakati wa mapambano yaliyopelekea kupatikana ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran, Ayatullah Ashrafi Isfahani aliwaongoza wananchi wa Kermanshah katika mapambano dhidi ya utawala wa Shah na ndio maana alikamatwa na kutiwa gerezani mara nyingi. Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, mwanazuoni huyo mkubwa aliteuliwa na Imamu Khomeini kuwa Imamu wa Sala ya Ijumaa katika mji wa Kermanshah; na katika tarehe kama hii ya leo, maadui wa Uislamu walimuua shahidi kwenye mihrabu wakati alipokuwa akisalisha Sala ya Ijumaa. Baada ya kuuawa shahidi Ayatullah Ashrafi Isfahani, Imam Khomeini (MA) alisema: “Nilikuwa namfahamu marehemu, shahidi mtukufu Hajj Agha Ata’ullah Ashrafi kwa muda mrefu kwa usafi wake wa nafsi, utulivu wa roho na moyo wake uliotulia, aliyepambana vilivyo na hawaa na matamanio ya nafsi na akiwa amepambika kwa ilmu, maarifa mengi yenye manufaa na matendo mema.

&&&

Siku kama ya leo miaka 484 iliyopita alizaliwa Abulfat'h Jalal al-Din Muhammad Akbar, mfalme aliyekuwa na utawala wenye nguvu wa silsila ya Teimurian nchini India. Alikuwa maarufu kwa jina la Akbar Shah na alitawazwa kuwa mfalme akiwa na umri wa miaka 13 baada ya kufariki dunia baba yake, Homayun. Kwa kipindi cha miaka mitano aliongoza nchi akiwa na cheo cha naibu mfalme chini ya usimamizi wa Bairam Khan. Baada ya kushika madaraka kikamilifu alianza kupanua wigo wa utawala wake katika maeneo ya Bengal, Kashmir, Sindh, Punjab, Ahmednagar na Kandahar. Mfalme Abulfat'h Jalal al-Din Muhammad Akbar alikomboa kisiwa cha Dakan huko kusini mwa India kutoka mikononi mwa Wareno. Akbar Shah alifariki dunia mwaka 1605.

&&&

Siku kama ya leo miaka 176 iliyopita alizaliwa mwanafalsafa wa Kijerumani Friedrich Wilhelm Nietzsche. Baada ya kuhitimu masomo, Nietzsche alianza kufundisha katika Chuo Kikuu cha Basel. Mwanafalsafa huyo alikuwa akipinga dini na misingi ya kimaadili; na katika falsafa na mitazamo yake alikuwa akiamini nadharia ya "Superman", kwa maana ya mtu mwenye uwezo kupita kiasi. Nietzsche alikuwa akiamini kwamba, mtu mwenye uwezo kupita kiasi au Superman ni matokeo ya irada na matashi ya mwanadamu na huwa juu ya mema na mabaya yote. Mwanafalsafa huyo ameandika vitabu kadhaa ikiwa ni pamoja na Beyond Good and Evil, The Birth of Tragedy na Thus Spoke Zarathustra. Katika kipindi cha mwishoni mwa uhai wake Friedrich Wilhelm Nietzsche alichanganyikiwa kifikra na alifariki dunia mwaka 1900.

&&&

Miaka 33 iliyopita katika siku kama ya leo, nchi ya Bosnia Herzegovina ilijitangazia uhuru kutoka kwa Yugoslavia. Jamhuri ya Bosnia Herzegovina kijiografia ipo kusini mwa bara la Ulaya na inapakana na nchi za Croatia na Yugoslavia.

Baada ya kumalizika Vita vya Pili vya Dunia Bosnia Herzegovina iliunganishwa na nchi ya Yugoslavia. Bosnia Herzegovina kama zilivyokuwa nchi zingine ikiwemo Serbia, Croatia na Slovenia nayo pia ilipigania uhuru na kufanikiwa kujikomboa katika siku kama ya leo.

&&&

Na leo tarehe 15 Oktoba ni Siku ya Vipofu Duniani. Suala la usalama wa vipofu na haki zao za kijamii daima lilikuwa likipewa umuhimu maalumu katika jumuiya za kimataifa na kwa msingi huo mwaka 1950 Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) na Baraza la Kimataifa la Vipofu zilikutana na kupasisha sheria ya Fimbo Nyeupe na kuitangaza tarehe 15 Oktoba kuwa ni Siku ya Fimbo Nyeupe au Siku ya Kimataifa ya Usalama wa Vipovu. Miongoni mwa vipengee vya sheria hiyo ni pamoja na haki ya vipofu kutumia suhula zote za hali bora ya kimaisha katika jamii, kuwahamasisha watu wa jamii hiyo kushiriki katika masuala ya serikali na kupewa ajira serikalini, kulinda haki za vipofu wakati wa kuvuka barabara na kadhalika.../