Ijumaa, tarehe 14 Novemba, 2025
Leo ni Ijumaa tarehe 23 Jamadil Awwal 1447 Hijria sawa na 14 Novemba 2025.
Siku kama ya leo miaka 492 iliyopita, ardhi ya Ecuador inayopatikana huko Amerika ya Kusini iligunduliwa na wavumbuzi wa Kihispania na kuunganishwa na ardhi zilizokuwa zikidhibitiwa na Uhispania.
Ecuador ilikoloniwa na Uhispania kwa karne tatu. Hata hivyo mwaka 1822 wananchi wapigania ukombozi wa nchi hiyo chini ya uongozi wa Simon Bolivar walifanikiwa kurejesha uhuru wa nchi hiyo na Ecuador ikajiunga na Shirikisho la Colombia Kubwa.

Miaka 309 iliyopita katika siku kama ya leo, Gottfried Wilhelm Leibnitz mwanahisabati na mwanafalsafa wa Kijerumani aliaga dunia mjini Hanover Ujerumani akiwa na umri wa miaka 70. Wilhelm Leibnitz alianza kuzisoma kwa bidii na juhudi elimu za falsafa na hisabati akiwa na umri wa miaka 15 alifanikiwa kupata shahada za juu kabisa katika masomo hayo.
Elimu na ufahamu mkubwa na mchango aliotoa katika elimu ya hisabati pamoja na vitabu alivyoandika kuhusiana na elimu hizo, ni mambo yaliyomfanya Gottfried Wilhelm Leibnitz awekwe katika faharasa ya wasomi maarufu wa falsafa na hisabati nchini Ujerumani.
Katika siku kama ya leo miaka 228 iliyopita inayosadifiana na tarehe 14 Novemba mwaka 1897, alizaliwa Charles Lyell mtaalamu wa masuala ya ardhi na mwanasayansi wa Scottland. Lyell alikuwa mtu wa kwanza kuweka misingi na kanuni sahihi za kielimu katika masuala ya geolojia.
Baada ya kufanya utafiti mkubwa hatimaye aliandika kitabu cha mijadala mitatu kuhusiana na misingi ya elimu ya utambuzi wa ardhi alichokipa jina la Principles of Geology.
Siku kama ya leo miaka 136 iliyopita, Jawaharlal Nehru mmoja kati ya viongozi wakubwa wa harakati ya mapambano ya India dhidi ya mkoloni Mwingereza alizaliwa huko Allahabad kaskazini mwa India.
Nehru alianza mapambano dhidi ya mkoloni Mwingereza baada ya kujiunga na harakati ya kitaifa ya ukombozi wa India. Jawaharlal Nehru alitiwa mbaroni mara kadhaa na kufungwa jela kutokana na mchango na nafasi yake kubwa katika mapambano hayo. Baada ya Mahatma Ghandi kujiunga na harakati ya kitaifa ya India, wanaharakati hao wakiongoza mapambano ya kupigania uhuru ya wananchi wa India walitoa pigo kubwa kwa mkoloni Mwingereza. Hatimaye India ilipata uhuru Agosti 15 mwaka 1947.
Miaka 136 iliyopita katika siku kama ya leo, alizaliwa Dakta Taha Hussein mwandishi na mwanafasihi mtajika wa Misri.
Msomi huyo mashuhuri alipofuka macho akiwa mtoto. Hata hivyo kipaji chake cha hali ya juu kilimuwezesha kuendelea na masomo na hadi kufikia mwaka 1918 alikuwa amekamilisha masomo yake ya shahada ya uzamivu katika vyuo vikuu vya Misri na Ufaransa.
Dakta Taha Hussein mbali na kuwa kipofu, aliweza pia kushika nyadhifa za juu ndani na nje ya Misri na kipindi fulani alikuwa Waziri wa Utamaduni wa Misri.
Leo tarehe 14 Novemba ni Siku ya Kimataifa ya Kupambana na Kisukari.
Ni vyema kuashiria hapa kuwa, kuanza na kustawi kwa miji, kubadilika muundo na mtindo wa chakula na kupungua harakati na mazoezi sahihi ya mwili kumetayarisha mazingira ya kuongeza kiwango cha sukari ya damu na ugonjwa wa kisukari. Ugonjwa huu ni miongoni mwa magonjwa yanayoongezeka duniani kila mwaka.
Siku hii ya tarehe 14 Novemba, ni siku ya kuzaliwa "Sir Frederick Grant Banting", mgunduzi wa insulini, na ilipewa jina la Siku ya Kisukari Duniani kwa mara ya kwanza mnamo 1991 kwa ushirikiano na Shirikisho la Kimataifa la Kisukari (IDF) na Shirika la Afya Duniani (WHO).
Madhumuni ya kupewa jina hilo ni kuongeza uelewa wa umma kuhusu sababu, matatizo, kinga na matibabu ya ugonjwa huo unaoongezeka kkila siku.
