Alkhamisi, tarehe 20 Novemba, 2025
-
Leo Katika Historia
Leo ni Alkhamisi tarehe 29 Jamadil Awwal 1447 Hijria sawa na 20 Novemba 2025.
Siku kama ya leo miaka 168 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Hijria alifariki dunia Abdul Baqi bin Sulaiman Farooqi anayehesabiwa kuwa miongoni mwa wataalamu na malenga wa lugha ya Kiarabu.
Alikuwa na kipawa cha kutunga mashairi ya kuvutia tangu akiwa kijana. Abdul Baqi alikuwa miongoni mwa wapenzi wa kizazi cha mtukufu Mtume Muhammad (saw) na alidhihirisha mapenzi yake hayo katika mashairi yake.
Miongoni mwa vitabu vya msomi huyo ni pamoja na kile alichokipa jina la "Al Baqiyatus Swalihat."

Siku kama ya leo miaka 127 iliyopita, alizaliwa Edwin Hubble, mtaalamu wa elimu ya nyota wa Kimarekani.
Awali alijiunga na chuo kikuu kusomea sheria kwa pendekezo la baba yake, hata hivyo baada ya kuhitimu alipendelea sana kusomea masuala ya nyota. Hivyo akaamua kusomea taaluma hiyo.
Katika harakati hiyo Edwin Hubble aliufanyia utafiti mkubwa mrundikano mkubwa wa mawingu na pia vumbi na gesi angani. Kadhalika alithibitisha kupishana sayari nje ya mfumo wa Milky Way, kama ambavyo pia aliamini nadharia ya kupanuka kwa dunia. Edwin Hubble alifariki dunia mwaka 1953 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 115 iliyopita alifariki dunia mwandishi mashuhuri wa Kirusi, Leo Tolstoy.
Mwandishi huyo alizaliwa mwaka 1828 na aliondokewa na baba na mama yake akiwa bado mdogo. Alifanya safari za kitalii na uchunguzi katika jamii nyingi za Ulaya na mambo aliyoyashuhudia katika safari hizo yalimfanya achukie ustaarabu wa kimaada wa nchi za Magharibi.
Tolstoy alilipa umuhimu mkubwa suala la kuwapa elimu na malezi watoto wadogo na alikuwa akijitahidi mno kusaidia matabaka ya watu maskini na wasiojiweza.
Leo Tolstoy ameandika vitabu vingi kikiwemo kile cha "Kiyama", "Kipindi cha Utotoni" na riwaya ya "Vita na Amani".

Tarehe 20 Novemba miaka 105 iliyopita mapambano makubwa ya wananchi wa Iraq dhidi ya wakoloni wa Kiingereza yalishindwa.
Baada ya Vita vya Kwanza vya Dunia na kusambaratika utawala wa Kiothmania, serikali za Ufaransa na Uingereza ziligawana ardhi za utawala huo katika Mashariki ya Kati. Kwa msingi huo Uingereza ilichukua Iraq na kukabiliwa na mapambano makali ya wananchi tangu hapo mwanzoni.
Mapambano hayo yaliongozwa na wanazuoni wa Kiislamu waliotoa wito wa kufukuzwa wakoloni wa Kiingereza na kuundwa serikali huru itakayozingatia sheria za Kiislamu.

Siku kama ya leo miaka 90 iliyopita, aliuawa shahidi Sheikh Izzuddin Qassam ambaye alikuwa miongoni mwa viongozi wa harakati ya mapambano ya ukombozi wa wananchi wa Palestina dhidi ya uvamizi wa Wazayuni maghasibu na ukoloni wa Uingereza.
Baada ya kukamilisha masomo yake ya awali huko Syria, Sheikh Qassam aliendeleza masomo yake katika Chuo Kikuu cha al Azhar huko Misri. Wananchi wa Palestina walianza mapambana dhidi ya mkoloni Mwingereza mwaka 1930 chini ya uongozi wa Sheikh Izzuddin Qassam.
Hata hivyo baada ya kupita miaka kadhaa Wazayuni maghasibu walishirikiana na wakoloni wa Kiingereza na kumuuwa kigaidi kiongozi huyo wa harakati ya mapambano ya Palestina.

Katika siku kama ya leo miaka 75 iliyopita majeshi ya Marekani na China yalipambana uso kwa uso kwa mara ya kwanza kabisa katika vita vya Korea.
Mapigano hayo yalitokana na himaya na uungaji mkono wa Marekani kwa Korea Kusini na uungaji mkono wa China na Urusi kwa Korea Kaskazini.
Vita vya Korea vilisababisha hasara kubwa mno kwa pande zote mbili. Vita hivyo vilisimama kutokana na upatanishaji wa Umoja wa Mataifa na hadi sasa Korea Kaskazini na Kusini zimebakia nchi mbili zilizojitenga.

Katika siku kama ya leo miaka 39 iliyopita, Sayyid Mahdi Hakim aliyekuwa mjumbe muhimu wa Baraza Kuu la Kiislamu la Iraq na mwana wa Ayatullah Sayyid Muhsin Hakim mmoja wa marajii wakubwa wa Kiislamu aliuawa shahidi na makachero wa utawala wa Saddam Hussein dikteta wa zamani wa Iraq, huko Khartoum mji mkuu wa Sudan.
Sayyid Mahdi Hakim alikuwa mmoja wa wanafunzi wa shahidi Ayatullah Sadr na mmoja wa wapinzani wakuu wa utawala wa Saddam Hussein.
