Dec 04, 2025 03:58 UTC
  • Alkhamisi 4 Disemba, 2025

Leo ni Alkhamisi tarehe 13 Jamadithani 1447 Hijria sawa na Disemba 4 mwaka 2025.

Tarehe 13 Jumadithani mwaka 64 Hijria kwa mujibu wa nukuu mashuhuri zaidi ya wanahistoria, alifariki dunia Fatima bint Huzam al Kilabiyya, maarufu kwa laqabu ya Ummul Banin, mke mwema na mcha Mungu wa Imam Ali bin Abi Twalib (as). 

Wanahistoria wamehitilafiana juu ya siku aliyozaliwa na baadhi wanasema alizaliwa mwaka wa 5 baada ya Hijra ya Mtume (saw). Imam Ali bin Abi Twalib alimuoa bibi huyu mwema baada ya kufariki dunia Bibi Fatima Zahra (as). 

Ummul Banin anatoka katika kizazi cha mashujaa wakubwa wanaopigiwa mfano baina ya Waarabu. Baada ya kuolewa, mtukufu huyo alimuomba Imam Ali ampe laqabu ambayo atakuwa akiitumia kumwitia badala ya jina lake la Fatima ambalo alichelea kwamba, litakuwa likiwakumbusha wajukuu wa Mtume mama yao, yaani Fatimatu Zahraa (as).

Aliwapenda sana Ahlul Bait wa Mtume na historia inahadithia jinsi alivyowatuma wanae wote wanne kwenda kulinda familia ya Mtume hususan Imam Hussain katika ardhi ya Karbala. Watoto wote wanne wa Hadhrat Ummul Banin, wakitanguliwa na Abul Fadhl al Abbas, waliuawa shahidi wakiwa pamoja na kaka yao, Hussein, katika medani ya Karbala.

Ummul Banin alifariki dunia katika siku kama ya leo mjini Madina na kuzikwa katika makaburi ya Baqi'.

Kaburi la Hadhrat Ummul Banin, Baqi' Madina

Siku kama ya leo miaka 1017 iliyopita alifariki dunia Ibn Haytham, mwanafizikia, mwanahisabati na mwanazuoni mkubwa wa Kiislamu katika mji wa Cairo. 

Ibn Haytham alizaliwa mwaka 354 Hijria katika mji wa Basra kusini mwa Iraq. Alibobea katika elimu za fizikia, tiba, falsafa na unajimu. Mwanazuoni huyo wa Kiislamu ameandika vitabu vingi vya hisabati, nujumu na tiba. 

Moja ya vitabu vyake muhimu ni al-Manadhir ambacho kimetafsiriwa katika lugha ya Kiingereza na kinatumika katika elimu ya nujumi.   

Ibn Haytham

Miaka 126 iliyopita, katika siku kama hii ya leo, kwa mara ya kwanza chanjo ya homa ya matumbo au Typhoid ilitumiwa kwa mwanadamu ili kukabiliana na maradhi hayo ambayo husababisha kuhara damu.

Awali chanjo hiyo ilivumbuliwa na mtafiti mmoja wa Kifaransa na baadaye ilikamilishwa na tabibu wa Kiingereza kwa jina la Almroth Edward Wright. 

Siku kama ya leo miaka 73 iliyopita, mkutano wa pande tatu yaani Marekani, Uingereza na Ufaransa ulifanyika katika kisiwa cha Bermuda kaskazini mwa Amerika Kusini.

Mbali na nchi hizo tatu kujadili uhusiano baina yao, zilichukua maamuzi muhimu na kuratibu namna ya kukabiliana na siasa za Shirikisho la Umoja wa Sovieti huko Berlin.

Katika zama hizo sehemu ya magharibi ya mji wa Berlin, Ujerumani ilikuwa chini ya udhibiti wa Marekani, Uingereza na Ufaransa na sehemu ya mashariki ilikuwa chini ya udhibiti wa Umoja wa Sovieti.

Kupamba moto hitilafu za namna ya kuuendesha mji huo, ndiko kulikopelekea kujengwa ukuta maarufu wa Berlin mnamo mwaka 1961.      *****

Siku kama ya leo miaka 35 iliyopita, mkutano wa kwanza wa Kiislamu kuhusiana na Palestina ulifanyika hapa mjini Tehran.

Mkutano huo ulifanyika katika fremu ya mfungamano wa walimwengu na mapambano ya Intifadha ya Palestina na kukabiliana na wimbi la kuhajiri Mayahudi kuelekea Palestina inayokaliwa kwa mabavu.

Ajenda kuu ya mkutano huo ilikuwa kuchunguza chanzo cha mapambano ya Intifadha ya wananchi Waislamu wa Palestina, Mapinduzi ya Kiislamu ya wananchi hao pamoja na taathira ya matukio ya Mashariki ya Kati kwa taifa la Palestina. 

Miaka 14 iliyopita katika siku kama hii, tarehe 13 Azar 1390 Hijiria Shamsiya mamlaka ya kijeshi ya Iran ilitangaza kuidhibiti ndege ya kijasusi ya Marekani isiyo na rubani au drone aina ya RQ-170 mashariki mwa nchi.

Ndege hii iliyokuwa imepaa kutoka nchini Afghanistan, iliangukia kwenye mtego wa vitengo vya vita vya kielektroniki vya Iran katika umbali wa kilomita 200 ndani ya Iran na kudhibitiwa na wataalamu wa Iran.

Ndege hiyo ya RQ-170 ni mojawapo ya ndege za kisasa zaidi zisizo na rubani za jeshi la Marekani. 

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kwa kuchukua udhibiti wa ndege ambayo ina uwezo wa kukwepa rada, ilionyesha uwezo wake katika uwanja wa vita vya kielektroniki na kusababisha mshangao mkubwa miongoni mwa wataalamu wa kijeshi wa Marekani. Baada ya miaka mitatu, wataalamu wa Iran waliweza kunakili teknolojia ya uundaji wake na miaka mitatu baadaye walitengeneza mfano wake.   

Ndege ya RQ-170