Dec 10, 2025 02:32 UTC
  • Jumatano, Disemba 10, 2025

Leo ni Jumatano tarehe 19 Mfunguo Tisa Jamadithani 1447 Hijria sawa na Disemba 10 mwaka 2025 Milaadia.

Siku kama ya leo miaka 827 iliyopita alifariki dunia Ibn Rushd Andalusi, msomi mkubwa wa falsafa wa Kiislamu.

Abul-Walid Muhammad Bin Ahmad Bin Rushd, ambaye alikuwa miongoni mwa wasomi wakubwa wa elimu ya falsafa wa Kiislamu katika karne ya 6 Hijiria, alikuwa pia mtaalamu katika elimu za fiqhi, Hadithi, fasihi, mantiki na elimu nyingine za wakati huo.

Ibn Rushd aliyekuwa akiishi Andalusia (Uhispania ya leo) alikuwa mtu wa karibu kwa mfalme na miongoni mwa makadhi wa eneo moja la utawala wa kifalme. Mwanafalsafa huyo mkubwa wa Kiislamu ameandika vitabu vingi kikiwemo cha 'Bidaayatul-Mujtahid' 'Falsafatu Ibn Rushdi' na 'al-Kulliyaat'. 

Siku kama ya leo miaka 195 iliyopita, alizaliwa Bi Emily Dickinson malenga wa Kimarekani.

Bi Emily alijiendeleza na masomo yake katika ngazi ya Chuo Kikuu nchini Marekani. Aidha alivutiwa na fasihi ya lugha na kutunga mashairi baada ya kufahamiana na baadhi ya waandishi mashuhuri wa Kimarekani.

Malenga huyo wa Kimarekani aliweza kutunga beti karibu elfu mbili za mashairi, ambapo sehemu tatu tu za mashairi hayo zilichapishwa wakati wa uhai wake na zilizosalia zikachapishwa baada ya kuaga kwake dunia.   

Miaka 129 iliyopita katika siku kama hii ya leo alifariki dunia mwanakemia maarufu wa Sweden, Alfred Bernhard Nobel. Nobel alizaliwa mwaka 1833 na kuhamia nchini Russia wakati wa ujana wake.

Alfred Nobel alifanikiwa kuvumbua dynamite au baruti baada ya kufanya utafiti mkubwa kwa miaka kadhaa katika uwanja wa sayansi ya kemia. Hata hivyo mada hiyo badala ya kutumiwa kwa matumizi ya amani, ilianza kutumiwa kama kifaa cha kivita. Ni kwa sababu hiyo, ndipo Nobel akatoa pendekezo la kutolewa tuzo kila mwaka kwa shakhsia aliyefanya juhudi kubwa katika uwanja wa kuimarisha amani na usalama duniani.

Tuzo hiyo ambayo imepewa jina la mwasisi wake yaani Nobel mwenyewe, hutolewa katika nyanja tano za fizikia, kemia, tiba, fasihi na amani ya kimataifa kwa wasomi waliofanya jitihada kubwa za kuleta amani na mafanikio ya kielimu, uvumbuzi, na mambo mengine makubwa duniani. Hata hivyo uteuzi wa washindi wa Tuzo ya Nobel hususan ile ya amani duniani umeathiriwa na ushawishi wa baadhi ya madola makubwa na kuiondoa tuzo hiyo katika mkondo wa asili wa mwanzilishi wake.   

Katika siku kama hii ya leo miaka 77 iliyopita, yaani tarehe 10 mwezi Disemba mwaka 1948, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipasisha Azimio la Kimataifa la Haki za Binadamu na kuidhinisha haki za kimsingi na kijamii za binadamu.

Azimio hilo la haki za binadamu lilitayarishwa kwa maelekezo ya Umoja wa Mataifa kupitia jopo la wawakilishi wa nchi kadhaa duniani. Kipengee nambari moja cha azimio hilo kinasisitiza kuwa binadamu wote ni sawa.

Licha ya kupasishwa azimio hilo, leo hii vitendo na siasa za madola ya Magharibi hasa Marekani vinakinzana wazi na azimio hilo. Leo hii pia baadhi ya madola hayo ya Magharibi yamekuwa yakilitumia suala la haki za binaadamu kama wenzo wa kuyashinikiza mataifa mengine.

Miaka 41 iliyopita katika siku kama ya leo, Baraza Kuu la Mapinduzi ya Kiutamaduni liliundwa nchini Iran kwa amri ya Imam Ruhullah Khomeini mwasisi na mwanzilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Baada ya ushindi wa mapinduzi ya Kiislamu, makundi mbalimbali ya upinzani yalikuwa yakikwamishwa mwenendo wa masomo katika vyuo vikuu na shule mbalimbali hapa nchini. Kulikuwepo waalimu na wahadhiri wengi wapotofu ambao walikuwa wakifanya kazi katika vyuo vikuu na shule hapa nchini na hakukuwa kumefanyika mabadiliko yoyote ya ratiba, mbinu za ufundishaji, malezi na masomo. Matokeo yake ikawa ni kufungwa kwa muda vyuo vikuu.

Baada ya vyuo vikuu kufungwa, Imam Khomeini alitoa amri ya kuundwa Baraza la Mapinduzi ya Kiutamaduni kwa shabaha ya kuboresha masuala ya utamaduni katika shule na vyuo vikuu.