Jumatatu, 15 Disemba, 2025
-
Leo katika historia
Leo ni Jumatatu 24 Mfunguo Tisa Jamadithani 1447 Hiijria sawa na 15 Disemba 2025.
Siku kama ya leo miaka 903 iliyopita alifariki dunia Ahmad Bin Ali Baihaqi Sabzawari, mmoja wa maulama wakubwa wa elimu ya Qur’ani mjini Nishapur.
Ali Baihaqi Sabzawari, alitabahari katika elimu ya nahaw na lugha kutoka kwa maulama wakubwa wa enzi zake, huku akitafsiri aya za Qur’an Tukufu. Aidha alimu huyo alikuwa mahiri katika kisomo cha Qur’an Tukufu.
Ali Baihaqi Sabzawari ameacha vitabu mbalimbali ikiwemo: ‘Taajul-Maswadir’ na ‘al-Muhit Bi’ilmil-Qur’an.’

Katika siku kama ya leo miaka 193 iliyopita alizaliwa Alexandre Gustave Eiffel mhandisi na msanifu wa mnara mashuhuri wa Eiffel.
Umashuhuri wa Alexandre Gustave unatokana zaidi na usanifu na uhandisi wake wa mnara wa Eiffel mjini Paris ulioanza kujengwa tarehe Mosi Julai 1887 chini ya usimamizi wake.
Mnara wa Eiffel una urefu wa mita 324 ambapo katika zama zake ulikuwa mnara mrefu zaidi duniani. Alexandre Gustave Eiffel aliaga dunia tarehe 27 Desemba 1923 akiwa na umri wa miaka 91.
Siku kama ya leo miaka 173 iliyopita alizaliwa mwanafikizia wa Kifaransa Henri Becquerel.
Henri ambaye ndiye aliyevumbua nururishi au Radioactivity baada ya kufanya utafiti katika mada za urani na vitu vinginevyo, alianza kufanya jitihada za kupata vitu vinavyotoa miali ya X baada ya miali hiyo kugunduliwa na mwanafizikia wa Kijerumani, Wilhelm Conrad Röntgen 8 November 1895. Mwaka 1896 Becquerel aligundua nururishi inayoweza kuzalisha miali ya X.
Utafiti wa mwanafikizia huyo wa Kifaransa ulimfanya atunukiwe tuzo ya Nobel mwaka 1903. Msomi huyo alifariki dunia mwaka 1908.
Miaka 69 iliyopita mwafaka na siku hii ya leo alifariki dunia Walt Disney shakhsiya mashuhuri wa sekta ya filamu za watoto.
Disney alizaliwa mwaka 1901 huko Marekani. Walt Disney alihitimu masomo katika Chuo Kikuu cha Havard na kutunukiwa shahada ya udaktari katika sayansi ya uchoraji na uchongaji (Fine Art).
Disney alitoa mchango mkubwa katika kuimarisha sanaa ya filamu za katuni. Mara kadhaa alitunukiwa tuzo za Oscar katika uwanja huo wa kutengeneza filamu za katuni.
Miaka 50 iliyopita katika siku kama hii ya leo yaani tarehe 15 Disemba 1975, majeshi ya kikoloni ya Uhispania yalianza kuondoka Sahara Magharibi.
Polisario ni moja ya harakati za ukombozi wa Sahara Magharibi iliyowalazimisha Wahispania kukimbia eneo hilo.
Harakati hiyo iliundwa mwaka 1973 baada ya wanamapinduzi wa Sahara kuasisi makundi kadhaa ya kupigania ukombozi wa eneo hilo.

Siku kama ya leo tarehe 24 Jamadithani miaka 33 iliyopita, Ayatullahil Udhma Sayyid Muhammad Ridha Golpayegani, alimu, fakihi mkubwa na mmoja wa marajii wakubwa wa Kiislamu, alifariki dunia.
Alizaliwa Golpayegan, moja ya miji ya Iran na kusoma masomo ya dini kwa walimu stadi na waliokuwa wametabahari kielimu katika zama hizo, akiwemo Ayatullah Hairi.
Ayatullah Golpayegani alianza kufundisha katika Chuo Kikuu cha Kidini (Hawza) cha Qum-Iran baada ya kuasisiwa kwake. Mwanazuoni huyo mkubwa ameandika vitabu vingi katika nyuga mbalimbali.