Jan 13, 2026 04:12 UTC
  • Jumanne, 13 Januari, 2026

Leo ni Jumanne tarehe 23 Rajab 1447 Hijria sawa na tarehe 13 Januari 2026.

Tarehe 13 Januari miaka 576 iliyopita alizaliwa baharia na mvumbuzi wa Kireno, Bartholomew Diaz.

Baada ya kusafiri katika Bahari ya Atlantic kuelekea kusini mwaka 1488, Diaz alidai kuwa amegundua Rasi ya Tumaini Jema au (Cape of Good Hope) katika sehemu ya kusini zaidi ya bara la Afrika.

Miaka kumi baadaye baharia mwenzake, Vasco Da Gama, naye pia alifanikiwa kugundua njia ya baharini kuelekea India kupitia eneo hilo.

Siku kama ya leo miaka 335 iliyopita aliaga dunia George Fox mwanamageuzi wa Kikristo wa nchini Uingereza.

Fox alizaliwa 1624 katika familia ya kidini. George Fox alishindwa kustahamili mgongano uliokuwako katika maneno na vitendo vya makasisi na wafuasi wa Ukristo na vilevile vita vya watawala wa zama hizo.

Akiwa na umri wa miaka 19, Fox alikata shauri kufanya utafiti kwa ajili ya kutafuta ukweli. George Fox alikuwa akiamini kwamba, kuna ulazima wa kurejea katika mafundisho asili ya Ukristo na kujiepusha na umwagaji damu na wakati huo huo kusimama kidete kukabiliana na dhulma. Hata hivyo, Fox nae pia alitumbukia katika makosa kwenye itikadi zake. Pamoja na hayo, fikra zake zilipingana na mafundisho ya Ukristo katika zama hizo.

Mara kadhaa George Fox alitiwa mbaroni na kutupwa jela na mamia ya wafuasi wake walikuwa wakiteswa gerezani. Harakati yake ya kupigania mabadiliko ya kidini iliendelea baada ya kuaga kwake dunia na harakati hiyo ingalipo.   

Miaka 85 iliyopita katika siku kama hii mkutano wa kihistoria wa nchi waitifaki za Ulaya katika Vita vya Pili vya Dunia ulifanyika mjini London, Uingereza.

Mkutano huo ulifanyika kufuatia pendekezo la Waziri Mkuu wa wakati huo wa Uingereza Winston Churchill, lengo kuu lilikuwa kuratibu siasa za wakuu wa nchi za Ulaya katika medani za vita dhidi ya nchi mbili za Ujerumani na Italia.

Nchi za Uingereza, Uholanzi, Ubelgiji, Ufaransa, Ugiriki, Norway, Luxembourg na Denmark zilishiriki katika mkutano huo. ***

Siku kama ya leo miaka 47 iliyopita mapigano makali kati ya polisi wa utawala wa Shah na wananchi wa Iran yalitokea wakati yalipofanyika maandamano makubwa ya wananchi katika miji kadhaa ya Iran. Wananchi wengi wanamapambano waliuawa shahidi na wengine kujeruhiwa katika maandamano hayo.

Katika siku hiyo pia wanachuo na wakazi wa mji wa Tehran ambao walikuwa wamekusanyika kwa wingi mbele ya Chuo Kikuu cha Tehran walitangaza upinzani wao dhidi ya utawala wa Shah na wakitaka kurejea Tehran Imam Khomeini Mwenyezi Mungu amrehemu, kutoka uhamishoni huko Paris nchini Ufaransa.   

Katika siku kama ya leo miaka 45 iliyopita, shambulio la kwanza la kemikali la jeshi la utawala wa wakati huo wa Iraq chini ya uongozi wa dikteta Saddam lilitekelezwa dhidi ya Iran ikiwa ni chini ya miezi minne tu tangu Iraq ianzishe vita vya kichokozi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Shambulio hilo la kinyama ambalo lilitekelezwa kilomita 50 magharibi mwa mji wa Ilam magharibi mwa Iran, lilipelekea kuuawa shahidi na kujeruhiwa raia kadhaa. Jeshi la utawala wa Baath, likipata himaya na misaada ya madola ya Magharibi na Umoja wa Kisovieti, lilitumia mara chungu nzima silaha zilizopigwa marafuku dhidi ya raia na wapiganaji wa Iran katikakipindi chote cha vita vyake vya kichokozi dhidi ya taifa hili.

Takribani watu elfu kumi waliuawa shahidi na laki moja na elfu 30 walijeruhiwa kufuatia mashambulizi hayo ya silaha zilizopigwa marufuku.