May 17, 2026 02:50 UTC
  • Jumapili tarehe 17 Mei 2026

Leo ni Jumapili tarehe 29 Mfunguo Pili Dhulqaada 1447 Hijria inayosadifiana na tarehe 17 Mei, 2026.

Siku kama ya leo miaka 1227 iliyopita, yaani siku ya mwisho ya mwezi Dhulqaada mwaka 220 Hijria Imam Muhammad Taqi (as) mmoja kati ya wajukuu wa Bwana Mtume Muhammad (saw) aliuawa shahidi. Mtukufu huyo alipewa jina la 'Jawad' likiwa na maana ya mtu mkarimu sana kutokana na ukarimu wake mkubwa.

Imam Jawad alizaliwa katika mwezi wa Ramadhani mwaka 195 Hijria na kuongoza Umma wa Kiislamu baada ya kuuawa shahidi baba yake, Imam Ridha (as). Kipindi cha maisha ya Imam Jawad kilikuwa kipindi cha kuchanua utamaduni wa Kiislamu na kuenea kwa fikra, itikadi na falsafa na kujitokeza mifumo ya fikra za Kimagharibi za Wagiriki na Warumi katika ulimwengu wa Kiislamu.

Imam alifanya juhudi kubwa kulea kizazi chenye maarifa na kueneza elimu na mafundisho sahihi ya Uislamu kama njia ya kukabiliana na fikra za kigeni sambamba na kufichua siri na maovu ya watawala wa Bani Abbas. Suala hilo liliwakasirisha mno watawala hao ambao hatimaye waliamua kumuua shahidi mjukuu huyo wa Mtume (SAW) katika siku kama hii ya leo.     *******

Miaka 277 iliyopita, katika siku kama hii ya leo alizaliwa Edward Jenner, tabibu wa Kiingereza aliyegundua chanjo ya ndui yaani (small pox). 

Tabibu huyo alifanikiwa kugundua chanjo ya ndui tarehe 14 Mei mwaka 1796 akiwa na umri wa miaka 45 wakati alipoelekea nchini India. Baada ya hapo ugonjwa huo wa ndui ulitibiwa kwa kutumia chanjo hiyo.

Maradhi hayo ambayo wakati huo yalikuwa yakichukua roho za watu bila ya huruma, yalitokomezwa kabisa duniani mwaka 1979. ***

Miaka 161 iliyopita katika siku kama ya leo, kulitiwa saini mkataba wa kwanza wa kimataifa katika uwanja wa mwasiliano huko Paris, Ufaransa.

Utiaji saini huo ulihudhuriwa na wawakilishi kutoka nchi 20 duniani. Kwa utaratibu huo kukawa kumepasishwa hati ya kuasisiwa Muungano wa Kimataifa wa Telegrafu. Ni kutokana na sababu hiyo ndio maana siku hii ikapewa jina la Siku ya Kimataifa ya Mawasiliano.

Mwaka 1932 kwa mujibu wa maamuzi yaliyofikiwa katika mkutano wa Madrid Uhispania, jina la Muungano wa Kimataifa wa Telegrafu au Internatioanl Telegraph Union lilibadilishwa na kuwa, Umoja wa Kimataifa wa Mawasiliano au  International Telecomunication Union (ITU) na vipengee pamoja na sheria za jumuiya hiyo zikapitiwa upya.

Kuanzia mwaka 1947, taasisi hiyo ikawekwa rasmi katika faharasa ya asasi zilizoko chini ya Umoja wa Mataifa.   *****

Katika siku kama ya leo miaka 87 iliyopita, dola la Uingereza ambalo Palestina ilikuwa chini ya mamlaka yake, lilitoa kitabu kilichopewa jina la "Kitabu Cheupe" (The White Paper) na hivyo kukawa kumepigwa hatua nyingine katika njia ya kuasisiwa utawala ghasibu wa Israel. Wapalestina ambao walikuwa wakifahamu vyema himaya ya Uingereza kwa Wazayuni, waliukataa mpango uliokuwa umependekezwa katika kitabu hicho kwa ajili ya kuipatia ufumbuzi kadhia ya Palestina.   ****

Siku kama ya leo miaka 17 iliyopita, alifariki dunia Ayatuhil Udhma Muhammad Taqi Behjat Foumani, mmoja wa Marajii Taqlidi na maurafaa wakubwa wa Kiislamu.

Alizaliwa mwaka 1294 Hijria Shamsia katika mji wa Fouman ulioko katika mkoa wa Gilan kaskazini mwa Iran. Baada ya kupata elimu ya msingi ya kidini, mwaka 1308 Hijria Shamsia alielekea katika Chuo Kikuu cha Kidini cha Najaf nchini Iraq kwa ajili ya elimu ya juu.

Ayatullah Bahjat alikuwa mashuhuri sana kutokana na uchamungu wake. Kitabus Swalat, Jamiul Masail na Wasilatun Najat ni baadhi ya vitabu mashuhuri vya msomi huyo.