Hadithi ya Uongofu (51)
Assalaamu alaykum wapenzi wasikilizaji na karibuni katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu.
Kipindi chetu kilichopita kilizungumzia maudhui ya kuamrishana mema na kukatazana maovu. Tulisema kuwa, kuamrishana mema maana yake ni kila mmoja wetu kumtaka mwenziwe afanye mambo mema na kukatazama maovu maana yake ni kila mmoja wetu kumkataza mwenzake kutofanya mambo maovu na yasiyofaa. Kutokana na kuwa kutumia mbinu sahihi kwa ajili ya kutekeleza faradhi ya kuamrishana mema na kukatazana maovu ni jambo lenye umuhimu mkubwa, kipindi chetu cha leo ambacho ni sehemu ya 51 kitazungumzia maudhui hii. Kuweni nami hadi mwisho wa kipindi.
Moja ya njia za kuamrishana mema na kukatazana maovu ni kupitia maneno na mazungumzo na mtu anayefanya jambo hili anapaswa kuchunga baadhi ya masharti wakati anapozungumza na kumuamrisha mema na kumkataza maovu mwenzake. Mosi, anapaswa kuwa mpole na atumie maneno mazuri wakati anapomlingania mtu na kumkataza maovu. Hii ni kutokana na kuwa, msingi wa awali katika kulingania misingi ya Tawhidi na kumpwekesha Mwenyezi Mungu na kuamrishana mema na kukatazana maovu ni mapenzi, huba na ulaini. Kwa hakika kile ambacho hupelekea kupenya katika nyoyo za watu hata kama ni kichafu ni kinachopotosha ni kuamiliana na watu kwa huba, mapenzi na huruma na kuzichochea hisia za huba na mapenzi za wanadamu.
Katika aya ya 44 ya Surat Taha anawakumbusha Nabii Mussa na Harun AS ambao aliwapa jukumu la kwenda kumuongoza na kumpa hidaya Firauni kwamba, waongee naye kwa maneno mazuri na laini kwani asaa akanasihika au akaogopa.
Aya hiyoinasema: “Mwambieni maneno laini, huenda akazingatia au akaogopa.”
Kuhusiana na hilo Imam Ali bin Abi Twalib AS anasema:
Mrekebishe mtu anayetenda maovu kwa matendo yako mazuri; na wapeni miongozo watu wengine ya amali nzuri kwa kutumia maneno mazuri.
Imam Ja’afar Swadiq AS anabainisha masharti ya kuamrishana mema na kukatazana maovu kwa kusema:
“Mtu anaweza kuwa ni mwenye kuamrisha mema na kukataza maovu pale anapokamilisha sifa tatu. Mosi, akifanyie kazi kile anachomuamrisha mwingine akifanye; na ajiweke mbali na kile anachomkataza mtu mwingine. Pili, katika kuamrisha mema na kukataza maovu mtu anapaswa kufuata njia ya kati na kati. Na tatu, asitekeleze faradhi ya kuamrishana mema na kukatazana maovu kwa kumuonea huruma mtu au kwa kumdekeza.
Mtume saw anautaja ushirikiano katika mambo mazuri na ya kheri kwamba, ni sababu ya kushushiwa neema na ujazi na Mwenyezi Mungu. Anasema: Madhali watu wako katika kuamrishana mema na kukatazana maovu na wanasaidiana katika mambo ya kheri, watakuwa katika kheri. Lakini mara watakapoacha kufanya hivyo, basi watapokonywa neema na ujazi walionao.
Moja ya mbinu na njia zenye taathira mno katika kuamrisha mema na kukataza maovu ni tablighi na ufikishaji ujumbe kwa njia ya vitendo. Mtume SAW alikuwa akiitumia njia hii. Kabla ya mbora huyo wa viumbe kuwashajiisha watu wengine kufanya jambo fulani, yeye mwenyewe alikuwa wa kwanza kulifanya. Aidha Imam Ja’afar Swadiq AS anaitaja njia yenye taathira zaidi katika kuwalingania watu mambo ya kheri na amali njema kuwa, ni wito wa kivitendo na aliwaambia wanafunzi na wafuasi wake kwamba:
Msiwalinganie watu dini yenu kwa ulimi bali kwa amali njema, kufanya bidii, Swala na matendo mema, kwani vitendo hivi vyenyewe ni vilinganiaji.”
Wakati wa kuamrisha mema na kukataza maovu mbali na kuchunga lugha anayotumia mtu na kutumia upole na ulaini katika uzungumzaji wake, mhusika anapaswa kuwa mstahamilivu na kujiandaa vilivyo kuvumilia maneno ya ukosefu wa adabu ambayo yamkini akayasikia kutoka upande wa pili yaani kwa anayemlingania.
Inanukuliwa katika historia, mwarabu mmoja wa jangwani aliingia mjini Madina na kisha akaenda katika msikiti wa Mtume ili akachukue pesa kutoka kwa mbora huyo wa viumbe. Alipoingia msikiti alimuona Mtume SAW akiwa amekaa pamoja na maswahaba zake. Alieleza shida yake na Mtume SAW akampatia kiasi fulani cha pesa, lakini Bwana yule hakukinaika na akaiona pesa aliyopewa kuwa ni kidogo sana. Mbali na kutoa maneno makali na yasiyofaa, alimkosea adabu Mtume SAW. Maswahaba wa Mtume SAW waliudhika na kughadhibika mno na ilibakia kidogo wampige, lakini Mtume SAW aliwazuia.
Baadaye Mtume SAW alimchukua Mwarabu yule wa jangwani na kwenda naye nyumbani kwake na kisha akampatia kiasi fulani cha pesa. Baada ya Bwana yule kuona maisha ya kawaida kabisa ya Bwana Mtume SAW pamoja na muamala wake mzuri, ajisikia vibaya. Mwarabu yule alitambua kwamba, maisha ya Bwana MtumeSAW ni tofauti kabisa na maisha ya anasa na starehe ya wafalme na watawala wengine na hakukuwa na mali, dhahabu na vitu vya fakhari na anasa katika nyumba ya Mtume. Ni kutokana na hali hiyo akaridhika na alichopewa na akamshuruku Mtume. Siku nyingine Mwarabu yule wa jangwani akaja tena msikitini lakini mara hii kwa takwa la Mtume SAW na akayakariri maneno yale yale ya kushukuru aliyoyasema akiwa na Mtume SAW. Masahaba wa Mtume SAW wakacheka.
Mtume SAW akawaambia hadhirina: Mfano wangu na watu kama hawa ni mithili ya kile kisa cha bwana ambaye ngamia wake alikata Kamba na akawa anakimbia. Watu wakidhani kwamba, wanamsaidia Bwana yule wakawa wanapiga makele na huku wakimkimbiza ngamia yule. Ngamia yule alizidi kukata mbuga na kuzidi kukimbia. Mwenye ngamia akawapigia mayowe watu na kuwambia, tafadhalini msishughulishwe na ngamia huyo na mwacheni kama alivyo, kwani mimi mwenyewe ninafahamu ni jinsi gani nitamtamfunga kamba ngamia wangu…. Sasa kama siku ile ningelikuacheni mfanye kama mnavyotaka, bila shaka mngeamiliana vibaya na bwana huyu na mngelimuua akiwa kafiri. Lakini sikuruhusu hilo na badala yake nilitumia njia ya upole na ulaini kumtuliza."
Kuheshimu shakhsia za watu wengine ni miongonui mwa mambo ya dharura wakati wa kutekeleza faradhi ya kumarisha mema na kukataza maovu. Mwenyezi Mungu anasema katika aya za 41 na 42 za Surat Maryam:
Na mtaje katika Kitabu Ibrahim. Hakika yeye alikuwa mkweli, Nabii. Alipo mwambia baba yake: Ewe baba yangu! Kwa nini unaabudu visivyo sikia, na visivyo ona, na visivyo kufaa chochote?
Kwa hakika aya hizi zinabainisha upeo wa hali ya juu wa unyenyekevu wa Nabii Ibrahim AS katika kumlingania Mungu mmoja ami yake. Katika upande mwingine kutumia sentesi za kuhoji badala ya kutoa amri na kukataza ni aina fulani ya adabu na heshima. Aidha katika upande mwingine Nabii Ibrahim AS anamtanabahisha ami yake kwa kubainisha sababu ya kumkataza kuabudu masanamu. Kisa kifuatacho kimenukuliwa katika Kitabu cha Bihar al-Anwar.
Inasimuliwa kwamba, mzee mmoja alikuwa akitia udhu, lakini hakuwa akifahamu njia sahihi ya kutia udhu. Yaani alikuwa akichukua udhu isivyo. Imam Hassan na Imam Hussein AS wajukuu wa Bwana Mtume SAW walikuwa wangali wadogo na walimuona mzee yule akitia udhu kimakosa. Hivyo wakaazimia kumfundisha mzee yule utiaji udhu kwa njia sahihi. Lakini kama wangemwendea moja kwa moja mzee yule na kumwambia babu hujui kutia udhu na udhu wako sio sahihi, huenda hatua yao hiyo ingekuwa ni kumdhalilisha mzee wa watu na yamkini hatua hiyo ingemfanya yule mzee asikubali kama amefanya kosa. Mbali na hayo, hatua kama hiyo ingeacha kumbukumbu chungu kwa mzee yule kutokana na kukoselewa kimacho macho tena na watoto wadogo.
Maimamu Hassan na Hussein AS wakakata shauri wamfundishe babu yule kutia udhu lakini kwa njia isiyo ya moja kwa moja. Hivyo walimuendea mzee yule na kumwambia wanaomba awahukumu nani kati yao anatia udhu kwa njia sahihi. Kisha wote wawili wakachukua udhu kwa njia sahihi na hakukuwa na tofauti yoyote baina yao katika utiaji udhu.
Hapo ndipo mzee yule alipotanabahi na kufahamu kwamba, njia sahihi ya kutia udhu ni kama walivyotia udhu vijana wale wadogo na akafahamu lengo hasa la vijana hao ambalo lilikuwa ni kumfundisha yeye namna ya kutia udhu lakini kwa njia ya heshima na isiyo ya moja kwa moja. Mzee yule akawambia Hassan na Hussein, udhu wenu nyote wawili uko sahihi na umekamilika. Mimi mzee ndiye ambaye hadi sasa nilikuwa sifahamu namna ya kutia udhu kwa njia sahihi. Nyinyi mmeweza kunitanabahisha na kunifundisha kwa hukumu ya huba mliyonayo kwa umma wa babau yenu. Ninakushukuruni sana.
Kwa leo tunakomea hapa. Tukutane tena wiki ijayo.
Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh..