Jumatatu, Septemba 26, 2016
Leo ni Jumatatu tarehe 24 Dhulhija 1437 Hijria sawa na Septemba 26, 201.
Siku kama ya leo miaka 1428 iliyopita kwa mujibu wa nukuu mashuhuri ya kihistoria Mtume Muhammad (SAW) akiwa pamoja na binti yake Bibi Fatima (AS), mkwewe Ali bin Abi Twalib (AS) na wajukuu wake wawili Hassan na Hussain (AS) waliondoka mjini Madina kwenda kufanya mdahalo na viongozi wa Wakristo wa eneo la Najran juu ya dini ya kweli. Tukio hilo linaelezwa na Mwenyezi Mungu SW katika aya za 60 na 61 za sura ya Aal Imran. Wakati viongozi wa Najran walipoona Mtume amekuja katika mdahalo huo akiwa na watu wanne tu wa Nyumba yake tukufu walipigwa na mshangao na kuelewa kwamba, dua ya mtukufu huyo ya laana kwa atakayesema urongo itakubaliwa. Katika hali hiyo askofu wa Najran alisema: "Ninaziona nyuso ambazo iwapo zitamuomba Mwenyezi Mungu aung'oe mlima mkubwa zaidi mahala pake basi dua yao itajibiwa papo hapo. Kwa msingi huo si sahihi kufanya mdahalo na watu hawa watakatifu kwani yumkini kizazi chetu chote kikaangamia." Baada ya hapo askofu huyo wa Najran alimuomba Mtume (SAW) kufanya suluhu na kusamehe. Tukio hilo la kihistoria lilidhihirisha haki na ukweli wa dini tukufu ya Kiislamu na utukufu na nafasi aali ya Ahlubait wa Mtume Muhammad (SAW).
Siku kama ya leo miaka 35 iliyopita wapiganaji shujaa wa Iran walifanikiwa kuvunja mzingiro wa mji wa Abadan katika operesheni ya haraka na iliyokuwa imeratibiwa vyema dhidi ya ngome za jeshi la Saddam Hussein. Operesheni hiyo ilitekelezwa na wapiganaji wa Iran kufuatia agizo la kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu Imam Khomeini Mwenyezi Mungu amrehemu. Mji wa Abadan ulioko kusini magharibi mwa Iran ulizingirwa na majeshi ya Saddam kwa kipindi cha karibu mwaka mmoja tangu mwanzoni mwa uvamizi wa Iraq dhidi ya Iran na ilikuwa vigumu kuweza kuukomboa kutokana na kuwa na ngome nyingine. Hata hivyo wapiganaji shupavu wa Iran walifanikiwa kuvunja mzingiro huo kwa ushujaa mkubwa katika operesheni ya kijeshi iliyopewa jina la "Thaminul Aimmah." Mafanikio hayo ulikuwa ushindi wa kwanza wa jeshi la Kiislamu la Iran katika historia ya vita vilivyoanzishwa na Saddam Hussein dhidi ya Jamhuri changa ya Kiislamu.
Siku kama ya leo miaka 109 iliyopita, inayosadifiana na 26 Septemba 1907, nchi ya New Zealand iliyoko mashariki mwa Australia ilipata uhuru. Visiwa vya New Zealand vilikoloniwa na Uingereza mwaka 1769 na karne ya 19 Miladia, ilishuhudia ukoloni dhidi ya nchi hiyo ukishadidi sambamba na wimbi kubwa la wahajiri wa Kiingereza waliokuwa wakielekea katika nchi hiyo.
Katika siku kama ya leo miaka 128 iliyopita, alizaliwa Thomas Stearns Eliot mshairi na mwanafasihi mashuhuri wa Uingereza. Malenga huyo ambaye ni mashuhuri kwa jina la S. T. Eliot alitoa nudhumu yake ya kwanza ya mashairi mwaka 1922 iliyokuwa na jina la "The Waste Land" na kupata umashuhuri mkubwa. Mwanafasihi huyo wa Kiingereza aliaga dunia mwaka 1965.
siku kama ya leo miaka 56 iliyopita, inayosadifiana na 26 Septemba 1960, Makamu wa Rais wa Marekani Richard Nixon na Seneta John F. Kennedy wa Massachusetts walikabiliana katika mdahalo wa kwanza wa televisheni wakati wakiwania tiketi ya kuingia ikulu ya White House. John Kennedy aliibuka na ushindi katika uchaguzi wa rais uliofanyika mwaka huo.