Oct 17, 2016 07:17 UTC
  • Ulimwengu wa Spoti, Okt 17

Hujambo mpenzi msikilizaji wa Radio Tehran na hususan shabiki wa spoti na karibu tuangazie matukio muhimu ya michezo yaliyojiri ndani ya siku saba zilizopita ndani na nje ya nchi.

Muirani atawazwa Mwanariadha Bora wa Kiume

Bingwa wa mchezo wa kunyayua uzani (vyuma vizito) wa Jamhuri ya Kislamu ya Iran, Siamand Rahman ameteuliwa kuwa mwanariadha bora wa kiume duniani katika orodha ya mwezi Septemba mwaka huu na Kamati ya Kimataifa ya Paralimpiki IPC. Mwanamichezo huyo wa Iran amepata asilimia 64 ya kura za umma na hivyo kutawazwa mshindi wa Tuzo ya Allianz ya IPC. Muogoleaji wa Colombia Carlos Serrano na mwenzake wa Belarus Ihar Boki wameibuka wa pili na tatu kwa usanjari huo. Rahman wa Iran alivunja rekodi ya dunia na kushinda medali ya dhahabu katika Mashindano ya Olimpiki ya Walemavu ya Rio Septemba 14 mwaka huu. Mwanariadha huyo mwenye umri wa miaka 28 alinyanyua uzani wa kilo 270 katika kategoria ya wanariadha walemavu wenye kilo zaidi ya 107 na kuvunja rekodi dunia kwenye mashindano hayo.

Kabaddi: Iran yazinyuka Japan, Kenya

Timu ya taifa ya mchezo wa Kabaddi ya Iran kwa upande wa wanaume siku ya Jumamosi iliigaragaza Japan pointi 38-34 katika mashindano ya Kombe la Dunia ya mchezo huo. Katika mgaragazano huo uliopigwa katika ukumbi wa TransStadia mjini Ahmadabad nchini India, timu hiyo ya Iran iliendeleza rekodi ya kutoshindwa katika mchezo huo tangu mashindano hayo yaanze, huku ikiwa tayari imezichabanga timu nne.

Kwa ushindi huo Iran inasalia kileleni mwa Kundi B ikiwa na pointi 20 huku Japan kwa sasa ikiridhika na nafasi ya pili ikiwa na pointi 10 kutokana na migaragazano mitatu iliyocheza. Tayari vijana wa Jamhuri ya Kiislamu wameibuka washindi katika michezo minne, ukiwemo mchezo kati yake na Kenya. Timu zingine zinazoshiriki mashindano hayo ya dunia ni Bangladesh, Korea Kusini, Uingereza, Thailand, Marekani, Poland, Argentina na Australia.

Soka: Iran yaichachawiza Korea Kusini siku ya Tasua

Na ni kupashe kwa kifupi tu kuwa, timu ya taifa ya wanaume ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilipata ushindi mwingine wa matumaini katika duru ya tatu ya michuano ya kufuzu Kombe la Dunia mwaka 2018, baada ya kuizaba Korea Kusini bao 1-0 siku ya maombolezo ya Tasua Jumanne jioni. Katika mchuano huo uliopigwa katika uwanja wa taifa wa Azadi chini ya anga ya majonzi na maombolezo ya kukumbuka kuuawa shahidi Imam Hussein AS, vijana wa Iran walijinyakulia pointi 3 muhimu kwa kuwagaragaza mahasimu wao  Taeguk Warriors katika kipute cha Kundi A. Licha ya vijana wa Timu Melli kuanza mchuano huo kwa kasi, lakini taratibu walianza kupoteza umiliki wa mpira. Licha ya wachezaji hao wa Iran kupoteza fursa nyingi za wazi, lakini kiungo Sardar Azmoun anayekipiga katika klabu ya Russia ya Rostov alifanikiwa kucheka na nyavu za mahasimu kunako dakika ya 25, baada ya kuandaliwa pasi safi na Ramin Rezaeian. Juhudi za Korea Kusini kulipiza kisasi hazikufua dafu na mchuano huo ukamalizika kwa kwa ushindi muhimu wa bao 1-0 kwa vijana wa Iran ya Kiislamu.

Kenya yatamalaki Amsterdam Marathon

Wanariadha wa Kenya wamefanya vyema katika mbio za Amsterdam Marathon na kutia kibindoni medali kochokocho.

Mwanariadha wa Kenya Daniel Wanjiru akivuka utepe kwenye mbio za Amsterdam Martahon 2016

Wanariadha Daniel Wanjiru, Sammy Kitwara na Marius Kimutai wameibuka wa kwanza, wa pili na wa tatu kwa usanjari huo, katika mashindano hayo ya kimataifa yaliyofanyika Jumapili nchini Uholanzi. Wanjiru alimaliza wa kwanza kwa kutumia masaa mawili, dakika tano na sekunde 21.

Wakenya wengine waliong'ara katika mbio hizo za nyika ni Laban Korir, Ezekiel Chebii, Felix Kandie, Goeffrey Kirui na Benard Kipyegon.

Wule Wasihun na Abera Kuma wa Ethiopia walimaliza katika nafasi za 9 na 10 kwa utaratibu huo.

Mbio za kushiriki Kombe la Dunia 2018

Michuano ya mataifa ya Afrika ya kusaka tiketi ya kushiriki Kombe la Dunia nchini Russia mwaka 2018 imepamba moto huku matumaini ya baadhi ya timu hizo za Kiafrika kusonga mbele yakizidi kufifia. Mafarao wa Misri waliwanyorosha vijana wa Jamhuri ya Kongo mabao 2-1 katika mchuano uliochezewa mjini. Misri wanaongoza katika Kundi E baada ya mshindani wake mkuu katika kundi hilo yani Ghana, kutoka sare ya bao 1-1 vijana wa The Cranes ya Uganda. Wachezaji nyota wa Misri Mohamed Salah na Abdalla El Said ndio waliipatishia ushindi timu yao. Kongo ndio walianza kuliona lango la Misri katika dakika ya 24 ya mchezo kupitia mchezaji Férébory Doré, baada ya kupewa pasi nzuri na Thievy Bifouma, mchezaji wa klabu ya Angers ya Ufaransa. Mafarao wa Misri walicharuka na kabla ya kipindi cha kwanza kumalizika, walifanya mambo kuwa 1-1. Dakika nne kabla ya kipindi cha kwanza kumalizika, mchezaji Mohamed Salah alifungwa bao hilo kwa kichwa, baada ya kupokea pasi kutoka kwa Abdul Shafy katika dakika ya 41. Bao la pili la Misri lilifungwa baada ya Mohamed Salah wa klabu ya AS Roma ya Italia kutoa pasi nzuri kwa Abdalla El Said.

Kwengineko Tunisia ilipata ushindi muhimu ugenini wa mabao 2-0, ilipotoana kijasho na Guinea. Siku ya Jumamosi vijana wa Kondo DR waliinyeshea mvua ya magoli Libya, kwa kuisasambua mabao 4-0 ugani Matyrs. Kwengineko vijana wa Super Eagle ya Nigeria waliwavaa wenyeji wao vijana wa Chipolopolo ya Zambia mabao 2-1 wakati Algeria ikiupigia nyumbani ilikuwa inalazimishwa sare ya bao 1-1 na Cameroon.

Ligi ya EPL

Tunafunga kwa kuangazia matokeo ya michuano iliyopigwa mwishoni mwa wiki katika Ligi Kuu ya Soka ya Uingereza. Mabingwa watetezi wa Ligi ya Premia Leicester City walicharazwa mabao 3-0 na Chelsea katika uwanja wa nyumbani Stamford Bridge, na kuupa maana msemo kuwa 'mcheza kwao hutuzwa'. Hiki kinakuwa ni kipigo cha nne ugenini kwa timu hiyo iliyotwaa ubingwa wa ligi msimu uliopita. Mabao ya Chelsea yalifungwa na Diego Costa, Eden Hazard na Victor Moses.

Arsenal ikishangilia bao

Nao wabeba bunduki wa Arsenal wakafanikiwa kuondoka na ushindi licha ya kusalia na wachezaji 10 uwanjani katika mgaragazano na vijana wa mjini Swansea. Theo Walcott alifunga mawili upande wa Arsenal kabla ya Gylfi Sigurdsson kukomboa moja upande wa Swansea. Mesut Ozil aliwarejesha Arsenal mabao mawili mbele baada ya kufikia krosi ya kabla ya nguvu mpya Borja Baston kufunga la pili upande wa Swansea.

Uwanjani Etihad, vijana wa Pep Guardiola walitoka sare 1-1 na Everton. Mechi iliyoshangaza wengi ni ya Bournemouth ambao wamepata ushindi mkubwa wa mabao 6-1 dhidi ya Hull City.

……………….………..........….TAMATI…………….………………