Nov 01, 2016 02:48 UTC
  • Jumanne, tarehe Mosi Novemba, 2016

Leo ni Jumanne tarehe Mosi Safar 1438 Hijria sawa na tarehe Mosi Novemba 2016.

Siku kama ya leo miaka 1401 iliyopita, awamu ya mwisho ya vita kati ya jeshi la Imam Ali bin Abi Twalib (as) na Muawiya bin Abi Sufiyan ilianza katika eneo la Siffin kandokando ya Mto Furati (Euphrates) nchini Iraq. Baada ya Imam Ali bin Abi Twalib (as) kushika hatamu za uongozi Muawiya alikataa kumpa mkono wa utiifu na akaamua kuanzisha vita dhidi ya serikali yake.

Ramani ya eneo la Siffin

Tarehe Mosi Safar miaka 1377 iliyopita, msafara wa familia ya Mtume Muhammad (SAW) ambayo ilichukuliwa mateka katika vita vya Karbala, uliwasili katika mji wa Sham ambao ulikuwa makao makuu ya utawala wa Yazid bin Muawiya. Wakiwa Sham, Ahlul Bait wa Mtume (SAW) hususan Bibi Zainab (as) na Imam Sajjad (as) walitoa hutuba tofauti katika msikiti wa Sham wakifichua maovu ya Yazidi, kiongozi dhalimu wa Bani Umayyah. Vilevile Ahlul Bait wa Mtume (SAW) walifikisha kwa watu ujumbe wa harakati ya mashahidi wa Karbala kwa njia nzuri kiasi kwamba watu wa Sham walielewa ukweli kuhusu jinai za jeshi la Yazid na kuzua hasira dhidi ya mtawala huyo. Hali hiyo ilimfanya Yazidi aliyetoa amri ya kuuawa Imam Hussein (as) na wafuasi wake, akane uhakika huo na kumtwisha lawama hizo Ubaidullah bin Ziyad, aliyekuwa gavana wa mji wa Kufa, Iraq.

Msafara wa mateka wa Karbala

Siku kama ya leo, miaka 94 iliyopita utawala wa kifalme nchini Uturuki ulihitimishwa rasmi na Ataturk. Baada ya kumalizika kwa Vita vya Kwanza vya Dunia, sanjari na kudhoofika na kupoteza ushawishi wake utawala huo, Atatürk aliamua kuvunja utawala wa kifalme wa Othmania na kisha kutwa uongozi. Hata hivyo haikuwa rahisi kwa Mustafa Kemal Atatürk kumaliza utawala wa kifalme wa Othmania ambao ulikuwa umekita mizizi nchini humo. Mwanzoni alibakisha cheo cha ukhalifa wa Waislamu na tarehe Mosi mwaka 1922 Miladia, akavunja rasmi utawala wa kifalme huku cheo cha ukhalifa kikisalia tu kama cheo cha heshima. Suala hilo liliharakisha kuporomoka kwa utawala wa kifalme wa Othmania uliodumu kwa kipindi cha miaka 600. Baada ya kuporomoka utawala huo, uliundwa utawala wa Jamhuri hapo tarehe 29 Oktoba mwaka 1923.

Kemal Atatürk

Na siku kama ya leo miaka 62 iliyopita, vilianza vita vya ukombozi wa Algeria baada ya kuundwa Harakati ya Ukombozi wa Algeria chini ya uongozi wa Ahmed ben Bella. Baada ya kupita miaka 132 ya utawala wa kikoloni wa Ufaransa nchini Algeria, hatimaye mwaka 1962 mapambano ya ukombozi ya wananchi Waislamu wa Algeria yalizaa matunda na nchi hiyo kujipatia uhuru wake. Baada ya kutangazwa uhuru wa Algeria, Ahmed ben Bella alikuwa rais wa kwanza wa nchi hiyo. Utawala wa Ahmed ben Bella ulidumu kwa miaka mitatu tu, kwani ilipofika 1965 alipinduliwa na Kanali Houari Boumediene aliyekuwa waziri wake wa ulinzi.

Ahmed ben Bella

 

Tags