Hadithi ya Uongofu (54)
Ni wasaa na wakati mwingine wapenzi wasikilizaji wa kuwa nanyi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. Kipindi chetu cha juma hili ambacho ni sehemu ya 54 ya mfululizo huu kitakunukulieni baadhi ya hadithi kuhusiana na nafsi na aina zake. Kuweni nami hadi mwisho wa kipindi hiki.
Qur'ani Tukufu inalitambua suala la kufuata matamanio ya nafsi kwamba, ni sababu kuu ya kuporomoka mwanadamu na imebainisha jambo hilo katika aya nyingi. Mtume SAW anaitaja nafsi kuwa ndio adui mkubwa zaidi miongoni mwa maadui wa mwanadamu. Aidha katika dua zake mbele ya Mwenyezi Mungu alikuwa akisema kuwa, anajilinda na Mwenyezi Mungu kwa shari ya nafsi.
Kwa hakika Mwenyezi Mungu ameiumba nafsi ya mwanadamu ikiwa na hali ya kati na kati; na hali hii ya kati na kati akaijaalia pamoja nayo hiari na mamlaka ya kufanya mambo ili iweze kupiga hatua katika njia ya kuelekea katika ukamilifu wake. Hivyo basi hiari iko pamoja na kiumbe mwanadamu kwamba, akuze na kuimarisha engo ya kuwa kwake ni mnyama au engo ya upande wa Kimwenyezi Mungu. Imam Ali bin Abi Twalib AS amezungumzia katika hadithi nyingi sifa za nafsi. Mojawapo ya wasifu wa Imam Ali AS kwa nafsi ni pale anapoitaja kwamba, ni johari yenye thamani kubwa katika kumjenga mwanadamu. Mtukufu huyo anasema:
Nafsi ni johari yenye thamani ambayo kila ambaye ataichunga na kuiepusha na kuingia katika uchafu na dhambi, basi itamfikisha katika daraja ya ukamilifu zaidi; lakini kila ambaye ataiacha na kuitelekeza na kutoishughulikia basi humdhalilisha na kumuangusha."
Pindi nafsi ya mwanadamu inapoondoka katika hali ya kati na kati kutokana na mghafala na kuzama katika ladha mbaya za kinyama, katika hali hiyo nafsi huondoka na kuanguka kutoka katika nafasi yake ya kweli na kuporomoka huku huwa chimbuko la dhambi na matendo machafu na yasiyostahiki.
Katika hali kama hii nafsi hii ndiyo ile inayoitwa kwamba ni "Ammaratun Bissuui" yaani nafsi yenye kuamrisha mno maovu. Imam Ali AS anasema katika kuisifia nafsi hii kwamba: Daima nafsi siku zote huamrisha kutenda maovu. Kila mwenye kuiamini basi itamfanyia khiyana…. Na kila ambaye ataridhika nayo na akatoa jibu chanya kwa takwa la nafsi, basi humuongoza na kumuingiza katika matendo mabaya kabisa.
Kwa hakika nafsi yenye kuamrisha mno maovu yaani Nafsun Ammaratun Bissui ni mithili ya mnafiki ambaye amejipendekeza na kujionyesha kwamba, ni rafiki mzuri na mwenye kuguswa na mambo ya mwenzake na ambaye anamtakia kheri mwenzake, ilhali sivyo. Pindi nafsi hii inapomhadaa mtu na kumdhibiti, basi humuelekeza mwanadamu kwa nguvu zake zote upande wa hilaki na maangamio.
Neno nafsi katika Qur'ani Tukufu limetumika kwa sura tofauti tofauti. Nafsi ndio ule utambulisho wa mwanadamu na kitu ambacho hakitengani naye. Nafsi ina nguvu, hali ya kumili, muelekeo, na mahitaji mbalimbali. Kwa mujibu wa asili na fitra ya mwanadamu, nafsi hii ni yenye kutafuta ukamilifu na huwa ni yenye kuelekea upande wa ukamilifu. Wakati mwanadamu anapofanya kosa na kufahamu kosa lake hujitia kosa lake na kujilaumu kwa nini ametenda jambo hilo ambalo ni kosa. Hali hii ndio ile inayojulikana kama dhamira ya kimaadili au Nafsun Lawwamah yaani Nafsi inayojilaumu.
Nafsun Lawwamah ni nafsi ambayo iko safi na ambayo imesimama juu ya fitra na sifa safi za kibatini kiasi kwamba, kama nafsi hiyo itahisi kwamba, usafi huo na hali yake hiyo ya kati na kati imeondoka, basi nafsi hii hukumbwa na wasiwasi na kukosa hali ya utulivu na katika hali hii hufanya bidii ya kurejea katika nafasi yake kwa kufanya toba na unyenyekevu mbele ya Mwenyezi Mungu na kuondoka katika kinamasi cha dhambi.
Mtume SAW katika kumuusia Abdallah bin Mas-ud mmoja wa masahaba zake na mmoja wa wafasiri wakubwa wa Qur'ani amesema:
Fanya amali njema na mambo mema mengi, kwani mtenda mema na mtenda maovu wote watajuta. Mtenda mema atasema falaula ningelikuwa nimetenda mema zaidi huku muovu naye akijuta kwa kusema, nilizembea. Kwa hakika maneno haya yanaunga mkono aya ya pili ya Surat al-Qiyamah inayosema:
Na ninaapa kwa nafsi inayo jilaumu!
Kwa baadhi ya watu nafsi inayojilaumu ni yenye nguvu na imara mno huku kwa baadhi ya watu nafsi hii ni dhaifu mno na isiyojiweza.
Alaa Kulli haal, nafsi hii yaani Annafsun Lawwamah yaani nafsi inayojilaumu pale inapokosea, ipo kwa kila mwanadamu isipokuwa kama itakuwa haifanyi tena kazi kutokana na mtu kukithiri katika kutenda dhambi. Kwa maana kwamba, pindi mja anapozama katika kutenda dhambi, nafsi inayojilaumu hufa na kutofanya tena kazi.
Imam Muhammad Jawad AS anasema: Mwanadamu mwenye kufuata matamanio na hawaa ya nafsi, anakuwa amempa fursa adui yake aweze kufikia matarajio yake.
Wakati nafsi inapohifadhi na kulinda utulivu mbele ya panda shuka za maisha na kubadilisha shaka na kuwa yakini, basi nafsi hiyo hufikia katika daraja ya kuitwa kuwa ni Annafsu al-Mut'mainnah yaani Nafsi iliyotua.
Nafsi iliyotua ni nafsi ambayo hupata utulivu wa kweli na uhakika kupitia kumtaja na kumdhukuru Mwenyezi Mungu na kumzingatia Mola Muumba kufanya mambo ambayo yanamridhisha Allah SWT.
Kwa muktadha huo, nafsi hii huyatambua masuala kama utajiri na umasikini, au manufaa na madhara ya dunia kwamba, ni katika mitihani ya Mwenyezi Mungu. Endapo nafsi hii yaani Annafsu al-Mut'mainnah itazama katika neema na raha pamoja na starehe za dunia, haiwezi kukumbwa na hali ya kukengeuka, kutumbukia katika ufisadi na kutaka ukubwa, au kujikweza na kuwa na kuburi na hali ya kujiona. Endapo mja mwenye nafsi hii atatiwa majaribuni na kukumbwa na beluwa na baa la umasikini na hali ya kukosa, basi hayo hayamfanyi akufuru; bali daima na katika mazingira ya aina yoyote yale huwa katika njia ya kumuabudu Mwenyezi Mungu na kulinda uja; na katu si mwenye kuengeuka njia ya kati na kati maishani. Nafsi hii pia huwa na uhakika kamili na ahadi za Mwenyezi Mungu huku ikiwa na uhakika na njia ya haki iliyoichagua.
Mwenyezi Mungu anaihutubu nafsi hii katika Qur'ani Tukufu akisema:
Ewe nafsi iliyo tua! Rejea kwa Mola wako Mlezi hali ya kuwa mwenye kuridhia na mwenye kuridhiwa.
Imam Ali bin Abi Twalib AS anasema kuhusiana na nafsi hii kwamba:
Hakuna kitu katika mgongo wa ardhi chenye thamani mno mbele ya Mwenyezi Mungu kuliko nafsi yenye yenye kutii maamrisho ya Mwenyezi Mungu.
Wapenzi wasikilizaji kwa leo tunakomea hapa kutokana na kumalizika muda wa kipindi chetu, tukutane tena wiki ijayo.
Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh..