Hadithi ya Uongofu (58)
Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu alaykum wapenzi wasikilizaji popote pale mlipo. Karibuni kujiunga nami tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha hadithi ya Uongofu. Sehemu hii ya 58 ya mfululizo huu itakunukulieni majimui ya hadithi nyingine kuhusiana na shetani pamoja na njia za kukabiliana na kiumbe huyu mlaaniwa. Karibuni.
Kwa hakika shetani hutumia mbinu mbalimbali ili kuhakikisha kwamba, anamuondoa mwanadamu katika njia sahihi na nyoofu na kumvuta upande wa dhalala na maasi. Licha ya kuwa mbinu za shetani ni tofauti na za aina kwa aina kulingana na mazingira, lakini lengo kuu huwa ni kuwapotosha wanadamu na kuwafanya wawe mbali kabisa na njia ya Mwenyezi Mungu. Katika mazingira kama haya, njia pekee ya kupata uongofu na kumshinda shetani ni kujipamba kwa taqwa na uchaji Mungu. Mwenyezi Mungu anasema katika aya ya 201 ya Surat al-A'raaf kwamba:
Hakika wale wamchao Mungu, zinapowagusa pepesi za Shet'ani, mara huzindukana na hapo huwa wenye kuiona haki.
Katika vita vyake na mwanadamu na ile aweze kuibuka na ushindi, shetani hutumia mbinu na nyenzo mbalimbali. Moja ya nyenzo hizo ni ghadhabu na hasira. Kwa kumghadhibisha na kufanya mwanadamu akasirike, shetani hufanikiwa kufikia katika malengo yake na hivyo katika mazingira kama hayo anaweza kumtoa katika njia ya haki. Hii inatokana na kuwa, mtu akiwa katika hali ya hasira na ghadhabu yawezekana akafanya jambo lolote ile ambalo ni kinyume na mafundisho ya Uislamu. Ni kutokana na sababu hiyo, ndio maana kuna hadithi nyingi mno ambazo zinakokoteza na kuwataka waumini kudhibiti hasira zao na mara wanapopandwa na hasira basi watafute njia ya kuhakikisha kwamba, wanaondokana na hali hiyo. Kwa hakika shetani anaihesabu hasira au ghaidhi kama moja ya mitego yake muhimu ya kufikia malengo yake. Shetani anasema:
Ghadhabu ni wenzo wangu wa kuwindia, kwayo ninawanasa waja wazuri wa Mwenyezi Mungu na ninawaweka mbali na pepo yako na ninawavuta kuelekea motoni.
Siku moja Bwana Mtume saw alipita katika eneo moja akawaona mkusanyiko wa watu na baina yao kuwa mtu mwenye nguvu ambaye alikuwa akinyanyua jiwe kubwa lililokuwa likijulikana kama jiwe la mabingwa na akiwaonyesha watu jinsi alivyokuwa na nguvu za kubeba vitu vizito. Alikuwa akilinyanyua na kuliweka chini jiwe hilo zito na kuwafanya watu wapigwe na butwaa na wengine kupaza sauti za kumshangilia.
Mtume saw akauliza, mkusanyiko huu ni wa nini? Akaelezwa kuwa, ni wa ubebaji vitu vizito wa bingwa yule mwenye nguvu. Mtume saw akasema, je nikuelezeni mtu mwenye nguvu zaidi ni nani? Mtu mwenye nguvu zaidi ni yule ambaye anapotukanwa na kuvunjiwa heshima anastahamili, anayeishinda nafsi inayotaka kuasi, mwenye kushinda msukumo wa kulipiza kisasi na ambaye anamshinda shetani wa nafsi yake na shetani wa matusi. Aidha Imam Ali bin Abi Twalib as anasema kuwa: Shujaa zaidi miongoni mwa watu ni yule anayeyashinda matakwa na matamanio yake ya nafsi. Kadhalika Mtume saw amenukuliwa akisema kwamba: Ghadhabu au ghaidhi inatokana na shetani, na shetani ameumbwa kwa moto na moto huzimwa kwa kutumia maji. Hivyo basi iwapo mmoja wenu atapandwa na hasira, anapaswa kutia udhu ili moto wa ghadhabu uzimike na kutulia. Aidha katika hadithi nyingine, mbora huyo wa viumbe amenukuliwa akisema kwamba: "Je nikujulisheni amali na jambo ambalo kama mtalifanya shetani atajitenga na nyinyi na kuwa mbali nanyi umbali wa mashariki na magharibi? Akajibiwa, ndio ewe mjumbe wa Mwenyezi Mungu: Kufunga Saumu hupelekea sura ya shetani kuwa nyeusi na kutoa sadaka huvunja kiuno cha shetani. Kufanya urafiki na Mwenyezi Mungu na kutoa msaada kwa ajili ya amali njema, hukata mgongo wa shetani na kuomba maghufira (kufanya istighfaar) hupasua moyo wa shetani." Kwa hakika baadhi ya amali na matendo mazuri ya mwanadamu humuumiza mno shetani kiasi kwamba, hupiga mayowe na hutaabika na kukonda.
Tunakiendeleza kipindi chetu kwa kisa kifuatacho:
Siku moja shetani alikuwa amesimama katika moja ya kona za Masjid al-Haram mjini Makka, ilihali Mtume saw alikuwa akifanya tawafu katika nyumba ya Mwenyezi Mungu al-Kaaba. Baada ya Mtume saw kumaliza kufanya amali ya tawafu, alimuona shetani akiwa amesimama kando huku akiwa amepauka, amekonda na dhaifu. Mtume saw akasema, Ewe mlaaniwa! Imekuwaje umekuwa na hali hiyo ya udhaifu na kutaabika?
Shetani akasema: Nimechoka na umma wako huu. Mtume akamuliza, kwani umma wangu umekufanya nini? Akasema: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu kuna sifa kadhaa katika umma wako ambazo kadiri ninavyojitahidi niwapokonye sifa hizo, siwezi. Mtume saw akasema: Hizo sifa ambazo zimekutaabisha na kukuudhi ni zipi?
Shetani akasema: Mosi ni kuwa, kila wanapokutana wanatoleana salamu na Salaam ni moja ya majina ya Mwenyezi Mungu. Hivyo kila mwenye kutoa salaam huepushwa na kila balaa na masaibu. Na kila mwenye kujibu salamu Mwenyezi Mungu humjumuisha katika rehma Zake.
Pili ni kuwa, wakati wanapokutana hupeana mikono ambapo kwa kitendo hicho hupata thawabu nyingi huku huku rehma za Mwenyezi Mungu zikiwa pamoja nao madhali mikono yao haijatengana.
Tatu, hutamka Bismillahi kabla ya kuanza kazi yoyote ile. Aidha huanza kula chakula kwa Bismillahi na hivyo kutonishirikisha katika chakula chao na kunifanya nijitenge na kuwa mbali.
Jambo la nne ni kuwa, wakati wowote wanapozungumzia kufanya kazi Fulani katika mustakabali husema, "Inshallah Mungu akipenda" na hivyo kuridhia kadari na majaaliwa ya Mwenyezi Mungu. Kwa muktadha huo mimi siwezi kushuhudia kazi zao zikiharibika na ndio maana nataabika na kuteseka.
Jambo la tano ni kuwa, kuanzia asubuhi mpaka usiku ninafanya bidii ya kuwavuta katika madhambi, lakini wakati wa usiku wao hutubia na Mwenyezi Mungu huwasamehe madhambi yao; na kwa utaratibu huo bidii yangu ya kuwatia katika dhalala na upotofu huenda bure.
Jambo la sita na ambalo ni muhimu kuliko yote haya ni wakati wanaposikia jina lako likitajwa, basi hupaza sauti na kukuswalia na kukutakia rehma. Mimi nafahamu heshima na kuwa pamoja na Mtume kuna athari kiasi gani. Hivyo mimi siwezi kuvumilia kuona watu wa umma wako wakipatiwa thawabu na ujira wote huu. Na Mwisho ni kuwa wakati wanapowaona Ahlul Bayt wako huonyesha mapenzi na huba kwao na huu ndio ule ujira unaoelezwa katika aya ya 23 ya Surat Shuura pale Mwenyezi Mungu anaposema:
Sema: Sikuombeni malipo yoyote kwenu ila mapenzi katika ndugu (yaani kizazi cha Bwana Mtume saw); na hii ni moja aya amali bora kabisa.
Mtume saw akawageukia Masahaba zake na kusema: Kila mtu atakayekuwa na moja ya sifa hizi basi ni katika watu wa peponi.
Muda wa kipindi hiki umefikia tamati hivyo sina budi kukomea hapa kwa leo. Tukutane tena wiki ijayo.
Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabakaraatuh