Dec 02, 2016 02:58 UTC
  • Jumatano, 30 Novemba, 2016

Leo ni Jumatano tarehe 30 Safar 1438 Hijria sawa na 30 Novemba 2016.

Katika siku ya mwisho ya mwezi wa Safar miaka 1235 iliyopita, aliuawa shahidi Imam Ali bin Mussa ar Ridha AS, mmoja kati ya wajukuu wa Mtume Mtukufu SAW. Mtukufu huyo alizaliwa mwaka 148 Hijria katika mji wa Madina na alichukua jukumu la kuongoza Umma wa Kiislamu baada ya kuuawa shahidi baba yake, yaani Imam Mussa al Kadhim AS. Mnamo mwaka 200 Hijria, Maamun, Khalifa wa Bani Abbasi, alimtaka Imam Ridha AS aelekee kwenye makao ya Khalifa huyo yaliyokuwa katika mji wa Marwi, kusini mashariki mwa Turkemenistan ambayo ilikuwa sehemu ya Khorasan Kuu. Ijapokuwa kidhahiri Maamun alimfanya Imam Ridha kuwa mrithi wake, lakini kwa njia hiyo alikusudia kuimarisha zaidi nguvu za utawala wake. Utukufu na daraja ya juu ya kielimu na kimaanawi aliyokuwa nayo Imam Ridha na ushawishi wake uliokuwa ukiongezeka siku hadi siku ndani ya fikra na nyoyo za watu, vilimtia woga na hofu Maamun, na hivyo akaamua kufanya njama za kumpa sumu na kumuua shahidi Imam Ridha katika siku kama leo. Imam AS amesema:"Mja bora zaidi ni yule ambaye kila anapofanya jema hufurahia, na kila anapokosea huomba msamaha, inapomfikia neema hushukuru, anapokumbana na masaibu husubiri na wakati anapoghadhibika husamehe"

Haram ya Imam Ridha (as)

Siku ya mwisho ya mwezi Safar miaka 1437 iliyopita kulitokea tukio la Lailatul Mabiit na kuanza kwa hijra ya Mtume kutoka Makka kwenda Madina. Suala la hijra na kutoka Makka kuhamia Madina liliainishwa katika Baia ya Pili ya Aqaba. Makafiri wa Kikuraishi wa Makka walipopata habari hiyo walichukua uamuzi wa kumuua Mtume Muhammad (saw) na kwa sababu hiyo waliafiki pendekezo lililotolewa na Abu Jahl juu ya namna ya kutekeleza njama hiyo chafu. Kwa mujibu wa pendekezo hilo, kila ukoo kati ya koo zote za kabila la Kuraish lilitakiwa kumchagua kijana mmoja na wote kwa pamoja wavamie nyumba ya Mtume (saw) wakati wa usiku na kumuua akiwa amelala kitandani. Hata hivyo Mwenyezi Mungu SW alimjulisha Mtume wake kuhusu njama hiyo ya Makuraish na kumuamuru ahamie Madina usiku huo. Ili kuwapotosha makafiri wa Makka, Mtume (saw) alimtaka Imam Ali bin Abi Twalib (as) alale kitandani kwake. Usiku huo unajulikana katika historia kwa jina la Lailatul Mabiit kwa maana ya usiku ambao Ali bin Abi Twalib alikubali kuhatarisha maisha yake na kulala kwenye kitanda cha Mtume Muhammad (saw) huku akijua kwamba Makuraishi watavamia nyumba hiyo na kumkata kwa mapanga mtukufu huyo.  

لَیلَة المبیت

Siku kama hii ya leo miaka 78 iliyopita Ayatullah Sayyid Hassan Mudarres, mwanazuoni mwanamapambano na mpigania ukombozi wa Kiirani aliuawa shahidi na vibaraka wa Reza Khan, mtawala dhalimu wa Iran wa wakati huo katika mji wa Kashmar kaskazini mashariki mwa Iran. Ayatullah Sayyid Hassan Mudarres aliamua kuanzisha mapambano dhidi ya utawala huo baada ya kujionea dhulma na ukandamizaji wa mtawala Reza Khan nchini Iran. Alifanya jitihada kubwa za kutekelezwa sheria za Kiislamu hapa nchini na kuiokoa Iran kutoka kwenye makucha na udhibiti wa wakoloni. Kwa msingi huo mtawala kibaraka wa wakati huo wa Iran, Reza Khan Pahlavi alimuona kuwa adui mkubwa na kuchukua uamuzi wa kumuua.

Siku kama ya leo miaka 28 iliyopita aliaga dunia ustadh na karii mashuhuri wa Qur'ani Abdul Basit Muhammad Abdul Samad katika mji mkuu wa Misri, Cairo. Alianza kujifunza Qur'ani Tukufu akiwa bado mtoto mdogo na alipewa tuzo ya kuhifadhi na kusoma Qur'ani akiwa na umri wa miaka 12. Kipindi fulani Ustadh Abdul Basit alitumia muda wake mwingi kusafiri katika nchi za Kiislamu na kuwahamasisha watu kusoma kitabu cha Mwenyezi Mungu. Ustadh Abdul Basit ameacha kanda nyingi za Sauti ya kiraa yake ya Qur'ani Tukufu ambazo bado zinawavutia wasomaji wengi wa Qur'ani.

Abdul Basit Muhammad Abdul Samad

Miaka 181 iliyopita katika siku kama ya leo alizaliwa mwandishi mashuhuri wa Kimarekani, Mark Twain. Katika kipindi cha utotoni na ujanani, Twain alikumbana na mikasa mingi ambayo baadaye ilikuwa maudhui kuu ya vitabu vyake. Mark Twain ameandika vitabu vingi vya visa vya watoto na mabarobaro kikiwemo kile cha "Mikasa ya Tom Sawyer" (The Adventures of Tom Sawyer) na "Mwana Mfalme na Ombaomba" (The Prince and the Pauper).

Mwishoni mwa umri wake Mark Twain alikumbwa na umaskini na alifariki dunia mwaka 1910 baada ya vifo vya watoto wake wawili wa kike.

Mark Twain

Siku kama ya leo miaka 199 iliyopita, alizaliwa Theodor Mommsen mwanahistoria na mtafiti wa Ujerumani. Baada ya kumaliza masomo, Mommsen alijishughulisha na utafiti kuhusiana na vitabu tofauti na athari zilizobakia za tamaduni za zamani. Miongoni mwa vitabu vyake maarufu zaidi ni kitababu kinachoitwa 'Historia ya Roma ya Kale' ambacho ni kitabu kamili cha historia kuhusiana na mji wa Roma. Mwanahistoria huyo wa Ujerumani alitunukiwa tuzo ya Nobel katika fasihi hapo mwaka 1902 Miladia na kufariki dunia mwaka mmoja baadaye, akiwa na umri wa miaka 86.

Theodor Mommsen

Na siku kama ya leo miaka 349 iliyopita, alizaliwa mjini Dublin mji mkuu wa Ireland, Jonathan Swift mwandishi mashuhuri. Swift alishiriki pakubwa katika harakati za ukombozi wa Ireland. Baadaye, alianza kujishughulisha na kazi ya uandishi, ambapo alielezea maisha yake magumu katika kitabu cha kupigiwa mfano na kizuri kwa jina la ‘Simulizi ya Gulliver’. Swift alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 78.

Jonathan Swift