Jumanne 20 Disemba, 2016
Leo ni Jumanne tarehe 20 Mfunguo Sita Rabiul Awwal 1438 Hijria sawa na tarehe 20 Disemba 2016.
Siku kama ya leo miaka 81 iliyopita, Sheikh Izzuddin Qassam ambaye alikuwa miongoni mwa viongozi wa harakati ya mapambano ya ukombozi wa wananchi wa Palestina dhidi ya uvamizi wa Wazayuni maghasibu na ukoloni wa Uingereza, aliuawa shahidi. Baada ya kukamilisha masomo yake ya awali huko Syria, Sheikh Qassam aliendeleza masomo yake katika Chuo Kikuu cha al Azhar huko Misri. Wananchi wa Palestina walianza mapambana dhidi ya mkoloni Mwingereza mwaka 1930 chini ya uongozi wa Sheikh Izzuddin Qassam. Hata hivyo baada ya kupita miaka kadhaa Wazayuni maghasibu walishirikiana na wakoloni wa Kiingereza na kumuuwa kigaidi kiongozi huyo wa harakati ya mapambano ya Palestina.

Miaka 65 iliyopita katika siku kama ya leo, nchi ya Oman ilipata uhuru kufuatia makubaliano yaliyosainiwa kati ya nchi hiyo na Uingereza. Oman ina historia kongwe na hadi kabla ya kudhihiri Uislamu, nchi hiyo kuna wakati iliwahi kuwa chini ya mamlaka ya Iran. Nchi hiyo iliwekwa chini ya mamlaka ya Waislamu baada ya kuaga dunia Mtume Muhammad (saw). Karibu karne moja baadaye kundi la Khawarij lilianzisha ghasia na uasi huko Oman na kuitawala nchi hiyo kwa karne kadhaa. Baadaye Oman ikakoloniwa na Ureno na Waingereza.

Siku kama ya leo miaka 48 iliyopita, aliaga dunia John Steinbeck mwandishi wa riwaya wa Kimarekani baada ya kuishi kwa miaka 66. Alizaliwa mwaka 1902. Katika ujana wake Steinbeck alijishughulisha na kazi mbalimbali na hatimaye akaichagua taaluma ya uandishi. Mwandishi huyo alionesha kipaji cha hali ya juu alichokuwa nacho katika uwanja wa uandishi. Machungu ya Steinbeck katika maisha yake yalimuandalia uwanja wa kubainisha katika maandishi yake masaibu na machungu ya watu wasiojiweza. Miongoni mwa vitabu vyake ni Travels with Charley, East of Eden, A Russian Jornal na Burning Bright.

Miaka 988 iliyopita alifariki dunia Abu Tayyib Tabari, faqihi na mwandishi wa Kiislamu huko Baghdad. Abu Tayyib alizaliwa mwaka 348 Hijria huko Amol, moja kati ya miji ya kaskazini mwa Iran. Tabari alifanya safari katika nchi mbalimbali kwa lengo la kutafuta elimu. Abu Tayyib Tabari aliishi na kufundisha huko Baghdad ambapo alikuwa miongoni mwa maulamaa wakubwa za zama zake hizo. Faqihi Tabari alikuwa hodari katika taaluma ya fasihi na utunzi wa mashairi. Msomi huyo mkubwa wa Kiislamu ameandika vitabu mbalimbali na miongoni mwa vitabu hivyo ni "Jawab fi Sima'a" na "al Ghinaa wa Al Taaliqatil Kubra fil Furu'u".

Na leo tarehe 30 Azar mwaka wa Hijria Shamsia ni siku ya usiku mrefu zaidi wa mwaka ambao hapa nchini Iran unaitwa Usiku wa Yalda. Usiku huo wa Yalda au Usiku wa Chelleh ndio usiku mrefu zaidi wa mwaka katika nusu ya kaskazini mwa dunia. Usiku huo huwa baina ya kipindi cha kuzama jua tarehe 30 mwezi wa Azar ambayo ni siku ya mwisho ya kipindi cha mapukutiko (Fall) hadi kuchomoza jua katika siku ya kwanza ya mwezi Dei ambayo huwa siku ya kwanza ya kipindi cha baridi kali (Winter) Wairani na mataifa mengine mengi hufanya sherehe maalumu katika usiku huu wa Yalda. Usiku huo katika nusu ya kaskazini mwa dunia husadifiana na mabadiliko ya kimaumbile na tangu wakati huo mchana huanza kuwa mrefu zaidi kuliko usiku.
