Dec 27, 2016 08:20 UTC
  • Jumanne, Disemba 27, 2016

Leo ni Jumanne tarehe 27 Mfunguo Sita Rabiul Awwal 1438 Hijria sawa na Disemba 27, 2016 Milaadia.

Tarehe 27 Rabiul Awwal miaka 1075 iliyopita alizaliwa mshairi na mwandishi mashuhuri wa Kiarabu, Abul Alaa al Maarry katika mji wa Maarrat al-Nu'man karibu na mji wa Halab (Aleppo) nchini Syria. Abul Alaa alifariki dunia mwaka 449 Hijria katika mji huo huo ulio umbali wa kilomita 33 kusini mwa Idlib. Baadaye alielekea Baghdad kwa ajili ya kukamilisha elimu ya juu. Licha ya kuwa kipofu tangu utotoni, lakini Abul Alaa alitokea kuwa mshairi mashuhuri na hodari wa zama zake. Miongoni mwa vitabu vyake mashuhuri la "Risalatul Ghufran" na "al Aamali."

Abul Alaa al Maarry

Siku kama ya leo miaka 9 iliyopita Bi Benazir Bhutto kiongozi wa Chama cha Wananchi cha Pakistan (PPP) aliuawa kwa kufyatuliwa risasi na mlipuko wa bomu uliofanywa na magaidi huko Rawalpindi kaskazini mashariki mwa Pakistan. Mbali na Bi Benazir Bhutto, watu wengine karibu 20 wafuasi wa chama cha PPP waliuawa pia katika mlipuko huo. Bhutto alikuwa Waziri Mkuu wa Pakistan kwa mara ya kwanza mwaka 1988 baada ya kuenguliwa madarakani serikali ya kijeshi iliyokuwa ikiongozwa na Jenerali Muhammad Zia ul Haq.

Benazir Bhutto

Katika siku kama ya leo miaka 8 iliyopita, jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel lilianzisha hujuma kubwa na ya pande zote dhidi ya watu wa Ukanda wa Gaza magharibi mwa Palestina inayokaliwa kwa mabavu. Wakazi wa eneo hilo waliwakasirisha viongozi wa Kizayuni kutokana na kupambana kwao kishujaa dhidi ya uchokozi na mashambulizi ya Wazayuni na pia hatua yao ya kuiunga mkono serikali halali ya Palestina iliyokuwa ikiongozwa na harakati ya Hamas. Ni kwa sababu hiyo ndio maana Ukanda wa Gaza ukawekwa chini ya mzingiro wa kiuchumi wa utawala haramu wa Israel kwa karibu mwaka moja na nusu kabla ya mashambulizi hayo, mzingiro ambao unaendelea kuwasababishia Wapalestina wa eneo hilo matatizo chungu nzima kama vile ukosefu wa chakula na dawa.

Mashambulizi ya Israel dhidi ya watu wa Ukanda wa Gaza

Miaka 71 iliyopita katika siku kama ya leo, Mfuko wa Fedha wa Kimataifa (IMF) ulianzishwa. Miongoni mwa yaliyokuwa malengo muhimu ya mfuko huo, ni kuandaa nafasi zaidi za ajira, udhibiti wa thamani ya sarafu za kigeni na kuhakikisha kwamba, kunakuweko na ukuaji wenye uwiano katika masoko ya kimataifa. Makao Makuu ya Mfuko wa Fedha wa Kimataifa yako mjini New York Marekani.

Mfuko wa Fedha wa Kimataifa (IMF)

Siku kama ya leo miaka 71 iliyopita, kufuatia kumalizika kwa Vita vya Pili vya Dunia, mkataba wa kihistoria wa Moscow wa kuiigawa Korea ulitiwa saini. Mkataba huo ulitiwa saini na wawakilishi wa nchi tatu za Uingereza, Marekani na Umoja wa Sovieti. Kwa mujibu wa mkataba huo, Peninsula ya Korea ambayo hadi katika zama hizo ilikuwa nchi moja, iligawanywa katika sehemu mbili. Kwa utaratibu huo, kulitokea nchi mbili za Korea ya Kaskazini na Kusini, mgawanyiko ambao ungalipo hadi leo.

Korea mbili za Kaskazini na Kusini

Miaka 194 iliyopita katika siku kama ya leo, alizaliwa Louis Pasteur, tabibu na mwanakemia wa Kifaransa. Akiwa shuleni alisoma kwa bidii na jitihada kubwa. Baada ya kumaliza masomo yake alifanikiwa kupata shahada ya uzamivu katika kemia na kuanza kufundisha katika Chuo Kikuu cha Strasbourg huku akijihusisha pia uhakiki na utafiti kuhusiana na masuala mbalimbali ya kielimu.

Louis Pasteur

Miaka 37 iliyopita katika siku kama ya leo, inayosadifiana na tarehe 7 Dey mwaka 1358 Hijria Shamsia, Imam Khomeini (MA)  mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, alitoa amri ya kuanzishwa harakati ya kupambana na ujinga wa kutojua kusoma na kuandika. Imam Khomeini alitoa amri kwa wananchi wote wa Iran kushirikiana bega kwa bega kwa shabaha ya kumtokomeza adui ujinga. Hivi sasa kiwango cha watu wanaojua kusoma na kuandika nchini Iran kimeongezeka sana, na kufikia hatua kwa Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa UNESCO kuiondoa Iran kwenye orodha ya nchi zisizojua kusoma na kuandika na kuiweka kwenye kundi la nchi zenye watu wengi wenye kujua kusoma na kuandika.

Siku kama ya leo Miaka 48 iliyopita, Ayatullah Sayyid Muhsin Hakim, mkuu wa kituo cha kidini cha Najaf aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 92. Baada ya kuaga dunia Ayatullah Burujerdi ambaye alikuwa mar'ja' mashuhuri katika ulimwengu wa Kiislamu, Ayatulah Hakim alichukua nafasi yake na kufuatwa na Waislamu wengi na hasa wa Iraq, kuhusiana na masuala ya kifik'hi. Alipambana vikali na kila kundi au watu waliojaribu kuharibu jina la Uislamu. Fatua yake mashuhuri ya kupinga fikra ya ukomunisti dhidi ya mafundisho ya dini ilileta mabadiliko makubwa nchin Iraq. Fatua hiyo pia ilimpelekea kutoa amri ya kupigana jihadi dhidi ya utawala haramu wa Israel. Ujenzi wa maktaba, shule na vituo vya kidini na kiutamaduni pamoja na uandishi wa vitabu kama vile Mustamsak Urwat al-Wuthqah na Nahjul Faqaha ni miongoni mwa vitabu mashuhuri vilivyoandikwa na mwanazuoni huyo mashuhuri wa Kiislamu.

Ayatullah Sayyid Muhsin Hakim

 

Tags