Feb 11, 2017 06:01 UTC
  • Jumamosi, Februari 11, 2017

Leo ni Jumamosi tarehe 13 Mfunguo Nane Jamad al-Awwal 1438 Hijria mwafaka na tarehe 11 Februari 2017 Miladia.

 

Japan

 

Miaka 2677 iliyopita katika siku kama ya leo, mfalme wa kwanza wa Japan maarufu kwa jina la Jimmu alishika madaraka ya nchi. Kwa utaratibu huo mfumo wa kale zaidi na uliobakia kwa kipindi kirefu wa kifalme duniani ambao unaendelea hadi sasa, ulianzishwa. Wafalme wa Japan huwa na cheo cha heshima tu na Waziri Mkuu ndiye kiongozi wa masuala ya nchi. ***

Siku kama ya leo miaka 1427 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria na kwa mujibu wa baadhi ya riwaya, Bibi Fatma Zahra binti ya Mtume Muhammad SAW alikufa shahidi baada ya kuishi maisha mafupi lakini yaliyojaa mafunzo makubwa ya kimaadili na kimaanawi. Baba yake ni Mtume Muhammad SAW na mama yake ni Bibi Khadija Bint Khuwaylid AS. Bibi Fatma alikuwa katika medani mbalimbali mwanzoni mwa Uislamu bega kwa bega na Mtume, Imam Ali bin Abi Talib AS pamoja na watoto wake wema, yaani Imam Hassan na Hussein AS viongozi wa mabarobaro wa peponi. Bibi Fatma alisifika mno kwa tabia njema, uchaji Mungu na elimu, na alikuwa mfano na kiigizo chema cha mwanamke. ***

Katika siku kama ya leo miaka 1366 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria, Ibrahim bin Malik Ashtar mmoja wa makamanda shujaa wa Uislamu aliuawa katika vita na jeshi la Bani Umayyah. Alikuwa mtoto wa Malik Ashtar Swahaba na kamanda wa jeshi la Imam Ali AS. Ibrahim alikuwa pamoja na baba yake katika kipindi cha ujana wake katika vita vya Siffin na alionesha ushujaa mkubwa mbele ya wanajeshi wa Muawiyyah. Hata hivyo, Ibrahim Malik Ashtari aling'ara zaidi katika harakati iliyoanzishwa na Mukhtar Thaqafi huko Kufah. Harakati hiyo ilianzishwa kwa lengo la kulipiza kizazi cha damu ya Imam Hussein bin Ali bin Abi Twalib AS pamoja na masahaba zake waliouawa katika tukio la Karbala mwaka 66 Hijria.***

Ibrahim bin Malik Ashtar

Miaka 38 iliyopita katika siku kama ya leo, serikali ya mpito ya Mapinduzi ya Kiislamu ilianza rasmi kazi zake katika siku za mwanzo kabisa za umri wa Mapinduzi ya Kiislamu hapa nchini. Wakati huo huo wananchi waliendeleza mapambano ya kuangamiza kikamilifu mabaki ya utawala wa Shah. Baadhi ya makundi ya wananchi yalichukua jukumu la kulinda taasisi muhimu za serikali katika miji mbalimbali. Wakati huo ulidhihiri udharura wa kuwepo chombo cha kushughulikia kadhia hiyo na kukabiliana na vibaraka na mabaki ya utawala wa Shah. Kwa msingi huo Mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu hayati Imam Khomeini alitoa amri ya kuundwa Kamati ya Mapinduzi ya Kiislamu.***

Siku kama ya leo miaka 27 iliyopita, Mzee Nelson Mandela kiongozi wa harakati za kupambana na ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini aliachiwa huru baada ya kufungwa jela kwa kipindi cha miaka 27. Mandela alikamatwa mwaka 1963 na kuhukumiwa kifungo cha maisha jela kwa sababu ya mapambano yake dhidi ya utawala wa kibaguzi wa Afrika Kusini. Mwaka 1991 alifikia makubaliano na makaburu wa nchi hiyo juu ya jinsi ya kukomesha utawala wa ubaguzi wa rangi na miaka kadhaa baadaye yaani mwaka 1994 alichaguliwa kuwa rais wa kwanza mzalendo wa Afrika Kusini. ***

Nelson Mandela

Na miaka 6 iliyopita katika siku kama ya leo, Hosni Mubarak aliyekuwa amejitangaza Rais wa maisha wa Misri aliondolewa madarakani kwa mapinduzi ya wananchi. Mubarak ambaye awali alikua makamu wa Rais wa Anwar Sadat wa Misri alishika madaraka ya nchi mwaka 1981 baada ya kuuawa kiongozi wa nchi hiyo. Saadat aliuawa kwa kumiminiwa risasi na Khalid Islambouli kutokana na kutia saini makubaliano ya Camp David na utawala ghasibu wa Israel na kusaliti malengo ya taifa la Palestina. Baada ya kushika madaraka Mubarak alifuata nyayo za Sadat na hadi anang'olewa madarakani alikuwa kibaraka na mtekelezaji mkubwa wa siasa za Marekani na waitifaki wake katika eneo la Mashariki ya Kati na kaskazini mwa Afrika. ***

Hosni Mubarak

 

 

 

Tags