Jumapili, Februari 12, 2017
Leo ni Jumapili tarehe 14 Jamadal-Awwal 1438 Hijria, sawa na tarehe 12 Februari 2017 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 213 iliyopita, alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 80 Immanuel Kant, mwanafalsafa na msomi mashuhuri wa nchini Ujerumani. Kant alizaliwa mwaka 1724 Miladia katika familia ya kidini huku sehemu kubwa ya umri wake akiitumia katika kusoma, kufundisha na kuandika vitabu katika fani mbalimbali za kielimu kama vile, hisabati, nujumu, mantiki na falsafa. Ameacha athari nyingi baadhi ikiwa ni pamoja na 'Misingi ya Falsafa' 'Ukosoaji wa Akili ya Kivitendo' na 'Ukosoaji wa Akili ya Nadharia.'
Siku kama ya leo miaka 208 iliyopita alizaliwa mtaalamu wa elimuviumbe wa Uingereza, Charles Darwin. Darwin alifanya utafiti kuhusu namna ya kutokea viumbe mbalimbali na alifanya safari ya muda mrefu katika pembe mbalimbali za dunia kwa ajili ya kukamilisha uchunguzi wake wa kielimu. Baada tu ya kurejea aliandika kitabu maarufu cha "On the Origin of Species". Kwa mujibu wa nadharia ya Darwin ambaye ndiye aliyeanzisha mfumo wa Darwinism, chanzo cha viumbe vya leo ni viumbe vidogovidogo ambavyo vilibadilika kutokana na mazingira tofauti kwa miaka mingi na kufikia hali ya sasa.
Siku kama ya leo miaka 199 iliyopita nchi ya Chile ilijipatia uhuru wake kutoka kwa mkoloni Muhispania. Chile ilikaliwa kwa mabavu na Uhispania mnamo mwaka 1536. Mwaka 1788, Mfalme Charles III aliyekuwa mfalme wa Uhispania aliangalia upya makoloni yake na hivyo akaamua kuikabidhi nchi hiyo kwa Peru. Harakati ya kwanza ya kupigania uhuru nchini Chile ilianza mwaka 1814 Miladia. Katika harakati hizo wapiganaji waliokuwa wanataka kujitenga walishindwa vibaya na askari wa serikali ya kikoloni. Hata hivyo mwaka 1817 Miladia, José de San Martín, raia wa Argentina akishirikiana na maelfu ya wapiganaji alianzisha harakati dhidi ya makoloni ya Mfaransa ikiwemo Peru na Chile. Kwa uungaji mkono wa raia wa Chile hatimaye alifanikiwa kuwatimua wakoloni wa Uhispania na nchi hiyo kupata uhuru wake mwaka mmoja baadaye yaani mwaka 1818 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 125 iliyopita alifariki dunia Haj Mula Ismail Sabzawar, mtaalamu wa hadithi na hatibu mkubwa wa karne ya 13 Hijiria. Sabzawar alizaliwa kaskazini mashariki mwa Iran ya leo na kuanza kusomea elimu ya falsafa kwa mwalimu wake Haj Mula Hadi Sabzawar, mwanafalsafa mashuhuri wa nchi hii. Baadaye Haj Mula Ismail Sabzawari alielekea mjini Najaf Iraq kwa ajili ya kujiendeleza zaidi kielimu ambapo alitokea kuwa msomi mkubwa katika uga wa hadithi na falsafa. Ameandika vitabu vingi ikiwa ni pamoja na 'Majmaun-Nurain' na 'Nawaadirul-Athar.'
Siku kama ya leo miaka 112 iliyopita alifariki dunia Abdul-Ghaffar Tehrani, maarufu kwa jina la 'Najmud-Dawlah.' Awali Mirza Abdul-Ghaffar Tehrani alisoma masomo ya hisabati katika shule mbalimbali kama vile Darul-Funun ambapo pia alifanya utafiti mwingi katika uga huo. Baadaye Najmud-Dawlah alikuwa mwalimu katika chuo hicho kwa miaka mingi. Ameacha athari nyingi kama vile 'Bidaayatu-Hisab' na 'Usulul-Handasat.'
Siku kama ya leo miaka 69 iliyopita aliuawa shahidi mwasisi wa harakati ya Ikhwanul Muslimin na mwanamapambano mashuhuri wa Misri Ustadh Hassan al Banna. Hassan al Banna aliuawa shahidi katika njama iliyopangwa na Uingereza kwa ushirikiano na Mfalme Faruq wa Misri. Alianza mapambano yake dhidi ya ukoloni na vibaraka wake akiwa chuo kikuu ambapo alianzisha harakati ya kupambana na sera za kupinga dini ya Kiislamu za Uingereza kwa kuasisi hatakati ya Ikhwanul Muslimin hapo mwaka 1928. Harakati hiyo ilikuwa kwa kasi na kuenea katika nchi za Syria, Jordan, Lebanon, Palestina na katika baadhi ya nchi za kaskazini mwa Afrika. Serikali ya Misri ilipiga marufuku harakati ya Ikhwanul Muslimin mwaka 1948 na kuwafunga jela wanachama wake wengi na kisha kumuua shahidi kiongozi wake Sheikh Al Banna.
Na siku kama ya leo miaka 9 iliyopita aliuawa shahidi Imad Mughnia maarufu kwa jina la Haj Ridhwan, ambaye alikuwa miongoni mwa makamanda wa Hizbullah ya Lebanon, katika shambulizi la kigaidi lililofanyika mjini Damascus, Syria. Kamanda Mughnia aliuawa katika mlipuko wa bomu lililokuwa limetegwa na vibaraka wa Israel katika gari lake. Shahid Mughnia alijiunga na harakati za mapambano baada ya uvamizi wa Israel mjini Beirut. Baadaye kidogo alijiunga na harakati ya Hizbullah na kushika nyadhifa za juu katika harakati hiyo. Shahid Mughnia alikuwa na mchango mkubwa katika ushindi wa Hizbullah dhidi ya Israel katika vita vya siku 33 vya utawala huo nchini Lebanon mwaka 2006.