Feb 17, 2017 15:42 UTC
  • Mieleka: Iran yaidhalilisha Marekani na kutwaa Kombe la Dunia

Timu ya taifa ya mieleka ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetwaa Kombe la Dunia katika mchezo za mieleka mtindo wa Freestyle mwaka huu 2017, baada ya kuipigisha magoti Marekani katika ngoma ya fainali leo Ijumaa.

Shangwe na nderemo zilihinikiza hewani katika ukumbi wa michezo wa Imam Khomeini mjini Kermanshah, magharibi mwa nchi, baada ya wanamieleka wa Iran kuwapeleka mchakamchaka mahasimu wao wa Marekani na kuteta taji hilo walilolishinda mwaka jana 2016, kwa jumla ya alama 5-3.

Mwanamieleka wa Kiirani mwenye umri wa miaka 27, Hassan Sabzali Rahimi alimchachafya Mmarekani Anthony Ramos katika kategoria ya wanamieleka wa kiume wenye kilo 57, mtindo wa Freestyle, na kumbwaga alama 6-0.

Namna Muirani alivyomdhalilisha Mmarekani

Muirani mwingine Meysam Nasiri alimpeleka mbio Mmarekani Frank Aniello Molinaro na kumzamisha kwa alama 5-4 katika safu ya wanamieleka wenye kilo 65 wakati ambapo Mostafa Hosseinkhani alikuwa anamelemea Mmarekani mwengine James Green kwa alama 2-0 katika kategoria ya kilo 70. Ushindi mwingine mnono ulitwaliwa na Muirani Komeil Ghasemi katika kitengo cha kilo 125, baada ya kumdondosha raia wa Marekani, Nick Gwiazdowski, na kumshinda kwa alama 5-0.

Azerbaija imemaliza katika nafasi ya tatu baada ya kuitandika Uturuki jumla ya alama 7-1 huku Russia ikifunga orodha ya 5 bora katika mashindano hayo ya kimataifa.

Muirani akipambana na Mmarekani

Mashindano hayo ya dunia ya 2017 Freestyle World Cup yalianza Alkhamisi (Februari 16) na kumalizika leo Ijumaa (Februari 17).

 

Tags